ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 16, 2012

Mama Kanumba atoa ya moyoni

  Afarijika mwanae kuendelea kuombewa
Mama mzazi wa aliyekuwa msanii wa filamu nchini marehemu Steven Kanumba
Mama mzazi wa aliyekuwa msanii wa filamu nchini marehemu Steven Kanumba, amewataka wasanii wanachama wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (Shiwata) kuendeleza ushirikiano alioacha mwanae.

Akizungumza katika ibada ya kumuombea mwanae iliyoandaliwa na (Shiwata) jana jijini Dar es Salaam, Mama Kanumba, alisema amefarijika kuona wasanii wanaendelea kumuombea mtoto wake kila kona ya nchi.

"Nawashukuru Shiwata kwa moyo wa upendo na ushirikiano mlioonyesha kwa familia yangu, naomba muendeleze ushirikiano mliokuwa nao wakati mwanangu akiwa nanyi, endeleeni kushirikiana," alisisitiza Mama Kanumba.



Katika ibada hiyo iliyoongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Elim Pentekoste Ilala Bungoni jijini Dar es Salaam, Mchungaji Livingstone Mwaitela, alisema wasanii na familia ya Kanumba, wasisononeke kwa sababu Mungu alimpenda zaidi mtoto wao huyo.

Alisema wasanii waendelee kumkumbuka mwenzao kwa kubadili mambo yasiyompendeza Mungu badala yake wajiandae kwa kufanya mambo ambayo yanampendezesha na kujiweka tayari siku akiwaita wawe tayari.

Mwenyekiti wa Shiwata, Caasim Taalib, alisema Kanumba alikuwa mwanachama wao namba 648 akiwa mmoja wa waliojitokeza kutafuta eneo kwa ajili ya kujenga nyumba za wasanii kutoka Bagamoyo, Kisarawe na hatimaye kufanikiwa kupata eneo Mkuranga.

Marehemu Kanumba alifariki dunia Aprili 5, mwaka huu wakati akikimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kuanguka nyumbani kwake Sinza, jijini Dar es Salaam kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kufuatia ugomvi na anayetajwa kuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu.

Lulu, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam Jumatano iliypita akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya Kanumba.

Kesi hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Augustina Mmbando, lakini Lulu alitakiwa kutojibu chochote kuhusu tuhuma zinazomkabili kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji ambapo upelelezi ukikamilika, itahamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania,Kanda ya Dar es Salaam

Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Aprili 23, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Afadhali watu wanavyoanza kukubali kuwa mungu ndio mtoaji na ndio mchukuaji...... Tungoje hiyo tarehe 23 tuone mambo yataendaje, huruma tu kwa huyo dada manake mpaka kutoka hapo ni labda baada ya miaka kadhaa kama mnavyojua tena kesi zetu kila siku kuahirishwa na zikipangwa tena ni baada ya miezi kadhaa. Tuombe tu sheria itendeke. Kwa kweli hivi ni vilio viwili tuzidi kuwaombea wote pls. Thanks, mdau ohio

Anonymous said...

Pole sana mama mpaka leo siamini SK hatunae