RAIA wa Kenya Andrew Kimani amebainika kuendesha shule ya awali na msingi isiyo na usajili
mkoani Dodoma yenye wanafunzi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.
Shule hiyo ya Msingi na Awali inaitwa St Marks. Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo ameitaka shule hiyo kuhakikisha inasajiliwa ifikapo Desemba mwaka huu.
Mulugo, ambaye yuko katika ziara ya kutembelea baadhi ya shule za sekondari na vyuo katika Manispaa ya Dodoma, pia aliagiza uongozi huo kabla ya kukamilisha usajili, uitishe kikao cha wazazi ili wawatafutie watoto wao sehemu ya kufanyia mtihani wa darasa la nne na la saba mwaka huu.
Mbali na agizo hilo, Mulugo aliutaka uongozi wa shule hiyo kupeleka sifa za walimu wote waliopo shuleni hapo serikalini, akiwamo Mwalimu Mkuu ambaye ni raia wa Kenya ili kujua kama wana sifa zinazostahili na kama wanacho kibali cha kufanya kazi nchini.
Msimamizi wa Shule hiyo, Mathias Magesa alikiri mbele ya Mulugo kuwa mmiliki wa shule hiyo si raia wa Tanzania; ni raia wa Kenya na hata elimu yake ya ualimu alisomea nchini Kenya.
No comments:
Post a Comment