
Shabiki mashuhuri wa klabu ya Simba, Magoma Moto, akiashiria kuonyesha kadi nyekundu ikiwa ni moja ya mbwembwe zake anazofanya kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Simba inapokuwa uwanjani. Picha na Jackson Odoyo.
TIMU ya Simba imewasili mjini Setif ikitokea Bejaia kwa basi kwa ajili ya kucheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho la Soka la Afrika CAF dhidi ya ES Setif.
Simba iliwasili mjini Bejaia kwa ndege ikitokea Algiers na kupokelewa kwa shangwe na wanafunzi wa Kitanzania ambao wanasoma katika Chuo Kikuu cha Bejaia.
Timu hiyo iliwasili Bejaia muda wa saa 4:30 asubuhi sawa na saa 6:30 kwa saa za Tanzania na kuingia Setif saa saa 7:30 mchana, ambapo ni sawa na saa 9:30 za Tanzania.
Msafara wa basi lililokuwa limebeba wachezaji wa Simba uliongozwa na
polisi huku njia ya kutoka Bejaia kwenda Setif ikiwa ni ya milima yenye barafu na upande mmoja ikiwa ipo Bahari ya Meditteranian.
Simba iliwasili jana mjini Setif huku mvua ikinyesha na kupokelewa pia na vijana wa Kitanzania wanaosoma katika mji wa Setif na mji mwingine mkubwa wa Constantine ingawa hawakuwa wengi.
Simba imefikia katika hoteli ya Zidane, ambapo baada ya wachezaji kupata chakula cha mchana walikwenda kufanya mazoezi jioni kwenye Uwanja wa 8 May 1945.
Hata hivyo, tangu kuwasili hapa Algeria, wachezaji na viongozi wa Simba wamekuwa makini na chakula na imekuwa mara kwa mara ikitafuta njia tofauti za kupata chakula tofauti na wanachokikuta hotelini.
Jana baada ya kuwasili katika mji wa Setif uongozi wa Simba uliamua wachezaji kwenda kula chakula katika hoteli nyingine.
Pia Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alimpigia simu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu ambaye anatarajiwa kuja leo na kumuambia aje na kilo 30 za mchele pamoja na kilo tano za maharage kwa ajili ya kuandaa chakula cha wachezaji wa Simba na kuachana na vyakula vya waarabu.
Kaburu anatarajiwa kutua leo nchini Algeria akiwa na watu wengine tisa wakitokea Doha kwa ajili ya kushuhudia pambano hilo la Simba dhidi ya Setif litakalochezwa kesho.
Akizungumzia safari yao mpaka kufika mjini Setif, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba na Mkuu wa Msafara wa Simba, Danny Manembe alisema safari ilikuwa ndefu ila wanashukuru wamefika salama ukiacha vikwazo vingi walivyokumbana navyo.
"Tumefika Setif tumekuta hali ya hewa ya baridi kama tulivyotarajia, hivyo hali ya baridi haitatusumbua sana kwa sababu ni kama ile ya Njombe au Arusha au imezidi siyo sana," alisema Manembe.
Wachezaji wa Simba walionekana hawana wasiwasi katika muda wote wa safari mpaka kufika Setif ila wengi wao hawakupenda kitendo cha Simba kulala Algiers, ambapo wao walitaka timu ingekuja moja kwa moja Setif na kupumzikia Setif badala ya kupumzika Algiers.
Katika hatua nyingine, wachezaji wa Simba wanaofahamu Lugha ya Kifaransa walionekana muhimu baada ya kuteremka kwenye ndege kutokana na kuwasaidia wachezaji wenzao kujaza fomu mbalimbali zilizoandikwa kwa Kifaransa nchini Algeria.
Lugha kubwa zinazozungumzwa nchini Algeria ni Kifaransa na Kiarabu na wachezaji wachache wa Simba waliokuwa wakiwasaidia wenzao kujaza fomu hizo ni Patrick Mafisango, Gervais Kago na Felix Sunzu.
"Huwa mnamcheka Kago hajui kiswahili, sasa ni zamu yenu kumnyenyekea," alisema Mwinyi Kazimoto.
Baada ya Simba kutoka ndani ya uwanja wa ndege wa Algiers ilipata msaada mkubwa wa mawasiliano kutoka kwa wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma hapa Algeria ambao walikuwa wakiwatafsiria mambo mbalimbali.
Naye mmoja wa Watanzania wanaoishi nchini Algeria amewashauri mashabiki wa Simba na Yanga kuwa kitu kimoja wakati wanapocheza mechi za kimataifa na kuacha kushangilia timu za kigeni.
Mtanzania huyo amesema timu za Algeria zina ushindani wa hali ya juu zikiwa zinacheza zenyewe kwa zenyewe, lakini moja ya timu zao ikiwa inacheza na timu kutoka nchi nyingine mashabiki wa soka Algeria huungana na kuishangilia timu kutoka nchini mwao.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment