KITUO Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT) Dar es Salaam kimegeuzwa ‘gesti’ kutokana na kuwapo kwa makazi holela ya watu wanaojihusisha na vitendo vya ngono na uchafu wa mazingira.
Wakazi hao wamegeuza chupa za maji za plastiki, mifuko ya plastiki ‘rambo’, magazeti na makaratasi ya aina mbalimbali kuwa vyoo kwa kuvitumia kuhifadhi haja kubwa na ndogo na kuzitupa ovyo kwenye eneo hilo wakikwepa kulipa Sh 200 kwa huduma ya choo.
Wakazi hao wamegeuza chupa za maji za plastiki, mifuko ya plastiki ‘rambo’, magazeti na makaratasi ya aina mbalimbali kuwa vyoo kwa kuvitumia kuhifadhi haja kubwa na ndogo na kuzitupa ovyo kwenye eneo hilo wakikwepa kulipa Sh 200 kwa huduma ya choo.
Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kuwa kundi la watu hao linahusisha rika na jinsi tofauti na
watu wenye familia na wasio na familia kutoka nchi mbalimbali zikiwamo za nchi jirani ambao hufanya vitendo hivyo usiku.
Sambamba na uchunguzi huo, maelezo ya wadau wa UBT kwa gazeti hili yamethibitisha kuwapo kwa hali hiyo, licha ya jitihada zinazofanywa na uongozi wa kituo na Jiji kuwaondoa.
Huku wakisisitiza kutotajwa gazetini, baadhi ya wadau hao walisema kwa nyakati tofauti, kuwa
watu hao wana akili timamu na wameishi katika eneo hilo kwa muda mrefu.
Huku wakiutupia lawama uongozi wa UBT kwa kukosa udhibiti makini milangoni na kuruhusu
waingie wenye shughuli maalumu pekee, wadau hao walisema wanafikiri adhabu zinazotolewa
kwa wakamatwao mara wafikishwapo mahakamani zimeshindwa kuwarekebisha na hivyo kushauri zifanyiwe marekebisho.
Kinachoendelea kituoni hapo Imeelezwa kuwa wakazi hao holela huingia eneo hilo kupitia
kwenye milango yenye walinzi na ‘kuzamia’.
Hata hivyo, wazoefu wa kuingia na kutoka katika kituo hicho, waliliambia gazeti hili kuwa tofauti na ilivyokuwa wakati kinaanzishwa, hivi sasa mtu haulizwi anakwenda kufanya nini kituoni humo, ilimradi amelipa, uhuru wa kuingia ni wake na wala hatafutwi asipotoka.
“Ndiyo sababu kunakuwa na watu wengi wasio na shughuli maalumu kituoni. Wakishaingia
hung’ang’ania kuishi humo kwa kujichanganya na abiria na hivyo kuendesha maisha holela,” alisema mmoja wa viongozi wa idara moja kituoni hapo kwa masharti ya kutotajwa pia.
Aliongeza kwamba watu hao pamoja na kuchafua mazingira, wamekuwa wakichochea vitendo
vya ngono za waziwazi kwa wakubwa na watoto, hususan wanaoranda kutafuta chochote cha
kula usiku.
Makundi yanayohusika
Idadi kubwa ya watu waliozungumza na gazeti hili walitetea watoto wa mitaani kuwa hawahusiki na uchafuzi wa mazingira ya kituo hicho kwa kiasi kikubwa kama ilivyo kwa utingo wa mabasi, walinzi wa magari, marafiki zao na baadhi ya mafundi wa magari
wanaolala kwenye magari hayo usiku.
Walisema kundi la wanaohamia hapo kujisitiri limo katika kuchafua mazingira, lakini wenye akili na kazi zao UBT kama vile utingo, mafundi, marafiki zao na wabeba mizigo wasiotaka
kwenda kwao ndio wanatumia zaidi chupa na makaratasi kujisaidia.
Utingo aliyeomba kuhifadhiwa jina pia aliunga mkono maelezo ya mbeba mizigo huyo na kusema ni kweli yanayosemwa yanatendeka, lakini si utingo wote wanaoshiriki.
Alisema, “kuna uchafu mwingi unafanyika hapa usiku na unahusisha zaidi wanaoishi humu ndani ya kituo kiholela. Kuna watu wanaishi hapa na familia zao na wanajipatia huduma zote kuanzia ngono na huduma za choo.
“Wewe njoo uweke kambi siku moja utajionea vituko, akina mama wakienda kona hii na watu
(wanaume) wao, watoto wao nao wanakwenda kona zingine na wanaowarubuni halafu asubuhi
wafanya usafi … ndio wanaoteseka”.
Ofisa anayeshughulika na masuala ya afya kituoni hapo alisema wamekuwa wakifanya kila
wawezalo kuhakikisha usafi unakuwapo mahali hapo, lakini wachache wasio na hofu ya maradhi ndio wanawaangusha.
“Siwezi kumtaja mtu, lakini hiyo ndiyo hali halisi. Nafikiri ni hulka ya uchafu tu aliyonayo mtu,
kwa sababu kuna matundu ya vyoo zaidi ya 25 hapa kituoni na sehemu za haja ndogo zipo pia kwa ajili ya wanaume. Tozo ni Sh 200,” alisema.
Hata hivyo, baadhi ya wanaohusishwa na uchafu huo walijitetea kwa gazeti hili wakidai wanafanya hivyo kwa sababu hawana fedha za kulipia huduma ya choo.
Msemaji Jiji ang’aka
Kwa upande wake, Msemaji wa Jiji la Dar es Salaam, Gatson Makwembe, alikiri kuwapo uchafuzi wa mazingira kutokana na makazi holela, lakini alikataa kuthibitisha taarifa za eneo hilo kugeuzwa gesti kwa maelezo kwamba gesti inayotambuliwa na Jiji hilo ni moja inayojiendesha kibiashara.
“Kuna gesti moja tu inayotambulika UBT na ni maalumu kwa wasafiri wanaotaka kulala, hili kundi lingine hatutaki kulitambua, kwa sababu kwanza linavunja sheria na maadili.
“Tunajua wapo watu wa rika tofauti wanaoishi ovyo ndani ya kituo, lakini ni vigumu kujua kama wanatenda hayo (ngono), ila tatizo la kugeuza chupa za maji kuwa vyoo tuna taarifa nalo na tunalichukulia hatua kulimaliza kwa ajili ya afya bora za watu,” alisema Makwembe.
Katibu wa Afya wa Jiji hilo, Benson Nallya, alishauri watumiaji wa maji na juisi zinazouzwa katika chupa mitaani wawe makini na usafi wa chupa hizo, kwa kuwa nyingi huokotwa kiholela na kuwa na uchafu usioonekana hata zikisafishwa.
Alisema, usafi wa mtu na Jiji unategemea ushirikiano wa wananchi wote na si viongozi pekee.
Katika hatua nyingine, Halmashauri ya Jiji imesema haina mpango wa kujenga vyoo vya bure
kwa sababu inaendesha kituo hicho kibiashara.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment