ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 27, 2012

Vitambulisho vya Taifa vyakamilika



MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imesema awamu ya kwanza ya Vitambulisho vya Taifa imekamilika na vitaanza kutolewa mapema mwezi ujao. 

Imesema kuwa uzinduzi wa kutoa vitambulisho hivyo ulikuwa ufanyike jana katika maadhimisho ya sherehe za miaka 48 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini ilishindikana kutokana na shughuli nyingi na ukubwa wa tukio hilo. 

Ofisa Habari wa NIDA, Rose Mdami alisema uzinduzi huo unatarajiwa kufanywa na Rais Jakaya Kikwete ambapo wiki ijayo watazungumza na waandishi wa habari na kuelezea utaratibu mzima utakavyokuwa. 

“Ni kweli ilikuwa tuzindue utoaji wa vitambulisho hivyo kwa awamu ya kwanza leo (jana) kwa kuwa tayari vimekamilika, lakini kutokana na ukubwa wa sherehe hizi na wingi wa shughuli, 
imeshindikana... tutazindua mapema mwezi ujao,” alisema Mdami. 


Mwishoni mwa mwaka jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dickson Maimu alisema awamu ya kwanza ya utoaji vitambulisho hivyo ingefanyika jana kwa watumishi wa Serikali ambao tayari wamesajiliwa. 

Maimu alisema katika utekelezaji wa mradi huo, Mamlaka itatoa vitambulisho katika makundi matatu; Watanzania, wageni wakazi na wakimbizi. 

Alisema baada ya wafanyakazi wa Serikali, watafuatiwa wanafunzi, wafanyabiashara na hatimaye Watanzania wote watafikiwa na huduma hiyo muhimu kwa Taifa bila gharama yoyote. 

Hata hivyo, alihadharisha kuwa, pamoja na kuwa huduma hiyo ni bure, lakini mwananchi atakayepoteza kitambulisho chake atalazimika kukilipia. 

Maimu alisema mradi mzima unatarajiwa kugharimu Sh bilioni 350 na lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na kitambulisho hicho ifikapo mwaka 2015. 

Alisema vitambulisho hivyo pia vitasaidia kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura na kuipunguzia mzigo Serikali katika kuboresha daftari hilo kila wakati uchaguzi unapowadia. 

Pia vinatarajiwa kusaidia kuongeza wigo wa ukusanyaji wa kodi na kuongeza kipato cha Serikali. 

“Tutatoa vitambulisho hata kwa mwizi, kwa sababu moja ya faida kuu za mradi huu ni kudhibiti suala la usalama wetu kwa kila pointi. Ndiyo maana dhana kuu ya mfumo huu inatakiwa ijibu maswali makuu manne; nani ni nani; yuko wapi; anamiliki nini na anafanya 
nini,” alieleza Maimu alipozungumza na wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari nchini Desemba mwaka jana. 

Aliongeza kuwa vitambulisho hivyo katika eneo la usalama, vitasaidia kuimarisha usalama wa raia na mali zao na kupunguza vitendo vya uhalifu na hasa unaofanywa na raia kutoka nchi jirani na wafungwa waliomaliza adhabu zao.


Habari Leo

No comments: