ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 13, 2012

Wananchi wamuua mtoto aliyemuua mama yake-Habari Leo

MKAZI wa Kijiji cha Mchinga wilayani Lindi, Sikujua Selemani (68), ameuawa kinyama na mwanawe aliyemcharanga kwa mapanga hadi kufa baada ya kukosa chakula. 

Hata hivyo, baada ya mama huyo kuuawa, wananchi wenye hasira walimtafuta mtoto huyo aliyejulikana kama Ahmadi Musa (30) na kumshambulia kwa silaha mbalimbali hadi naye alipokutwa na mauti. 

Habari kutoka kijijini humo zilizothibitishwa pia na vyombo vya Dola, zinasema watu hao mama na mtoto walipoteza maisha yao juzi saa tatu asubuhi na saa sita mchana. 

Baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo, wameliambia gazeti hili kuwa hatua hiyo, imetokana na kijana huyo anayedaiwa ni mtumiaji wa dawa za kulevya aina ya bangi, kumlazimisha mama yake ampatie chakula majira ya asubuhi. 

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mchinga, Said Makinda juzi saa tatu asubuhi, Musa alimuomba ampatie chakula kwa kuwa alikuwa na njaa, lakini aliambiwa hakuna, jambo lililomfanya kijana huyo achukie. 

Alisema baada ya kijana huyo kupatiwa jibu hilo, alianza kumkaba koo mama yake na baadaye kumpiga sehemu mbalimbali za mwili hadi watoto wake wengine wawili akiwemo mmoja mwanamke walipoingilia. 

Makinda alisema kitendo cha wadogo zake kumgombelezea, kilitoa mwanya kwa Musa kuingia ndani ya nyumba yao na kutoka na panga ambapo alianza kumcharanga nalo mama yake sehemu mbalimbali ya mwili wake, ikiwemo kichwani. 

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Lindi, George Mwakajinga alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu tukio hilo, alikiri kutokea na kueleza tayari amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya kufuatilia mauaji hayo.

No comments: