ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 13, 2012

Babake Kanumba atoa siri nzito Dar

  Yawekwa hadharani nyumbani kwake Dar
  Mapya yaibuliwa kisa cha kutomzika mwanae
Marehemu Steven Kanumba (kushoto) wakati wa uhai wake akiwa na baba yake mzazi Charles Kanumba nyumbani kwao mjini Shinyanga.
Baba mzazi wa aliyekuwa muigizaji maarufu wa filamu nchini, Marehemu Steven Kanumba, amevunja ukimya kwa kuibuka na kueleza sababu iliyomzuia kuhudhuria mazishi ya mwanaye.

Marehemu Kanumba aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka huu jijini Dar es Salaam, alizikwa Jumanne wiki hii bila baba yake mzazi, Charles Kanumba, kuwepo. Hali hiyo iliibua mjadala miongoni mwa watu mbalimbali.

Mzazi huyo jana alieleza sababu iliyomfanya ashindwe kutoka mkoani Shinyanga kwenda Dar es Salaam ambako mazishi ya mwanaye yalifanyika na kuhudhuriwa na halaiki ya watu wakiwemo mashabiki wake, wasanii wenzake, viongozi wa serikali, makundi mbalimbali na wananchi kwa ujumla.



Nyumbani kwa Marehemu Kanumba jana eneo la Sinza Vatican, kulivuta waandishi wa habari na wapiga picha ambao walialikwa kusikiliza barua iliyokuwa imeandikwa na Mzee Charles Kanumba.

Akisoma barua hiyo iliyowasilishwa na wawakilishi wake watatu, mmoja wa wawakilishi hao, Chrisant Msipi, alisema kuwa baba mzazi wa marehemu hakufika kwenye mazishi hayo kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu na malaria.

Katika barua hiyo, baba wa marehemu amenukuliwa akieleza kuwa, alikuwa anajisikia vibaya na alipokwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kupima afya yake alikutwa ana malaria 15 na kuandikiwa sindano za saa.

Kupitia barua hiyo, aliongeza kuwa, ilipofika saa 12:00 jioni alizidiwa na alipopimwa kwa mara ya pili kuangaliwa shinikizo la damu (BP) alikutwa ana 180 kwa 140, kitu ambacho alisema alitakiwa kupumzika zaidi hospitalini chini ya uangalizi wa madaktari.

Barua hiyo iliendelea kueleza kuwa, hadi anawatuma wajumbe hao kwenda Dar es Salaam kupeleka ujumbe huo alikuwa anajisikia vibaya na hali ya afya yake haikuwa nzuri.

Alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, Watanzania wasimfikirie vibaya kwa kutofika katika msiba na mazishi ya mtoto wake.

Aliongeza kuwa, taarifa zilizozagaa zikidai kuwa hakuhudhuria mazishi ya mtoto wake kutokana na kutokuelewana si za kweli, ila alitamani sana kuwepo lakini afya yake haikumruhusu.

Mbali na Msipi aliyekuwa kiongozi wa msafara huo, ujumbe huo pia uliwashirikisha Michael Kanumba na Mjanaeli Kanumba.

Naye Katibu wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF), Wilson Makubi, alisema kuwa kwa sasa hakuna kazi yoyote ya marehemu Kanumba itakayotolewa bila idhini ya familia yake na TAFF. (Habari zaidi soma ukurasa wa 24)

Kwa upande wake, Mama wa Marehemu, Frolence Anjelo, alisema anawashangaa watu kujipatia kipato pasipo kupata ruhusa kutoka kwa familia ya marehemu Kanumba.

Aidha, Anjelo alitoa salamu za shukrani kwa Watanzania wote walioshiriki katika mazishi ya mtoto wake tangu kifo hadi siku ya mazishi.

Marehemu Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi Aprili 7, mwaka huu, baada ya kudaiwa kutokea ugomvi kati yake na msanii mwezake anayedaiwa kuwa mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’ (18).

Lulu juzi alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya mauaji.

Hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiza kesi za mauaji na kesi hiyo itatajwa Aprili 23, mwaka huu.

Ingawa Lulu hakutakiwa kujibu hadi upelelezi wa kesi hiyo utakapokamilika na kuhamishwiwa mahakama kuu, alidai kuwa hana miaka 18 kama ilivyodiwa kwenye hati ya mashitaka ila umri wake ni miaka 17.

CHANZO: NIPASHE

4 comments:

Anonymous said...

Na alipofanya Bday party ya kutimiza miaka 18 mwaka jana alikuwa anamdanganya nani?na wazazi wake waliona ni sawa tu wakakaa kimya bila kupinga au kukanusha.Huyo mtoto ameshindikana kwa wazazi so aangalie maana uongo wake unamponza sasa.

Anonymous said...

jamani vichwa vya habari vingine vinaniboaga sana, siri nzito ko wapi hapo sasa, na kwanza hiyo barua iko ktk mablog tangu juzi, yenyewe kabisa original, waandishi bwana , muandishi shabiki sana.

Anonymous said...

Asante anon wa kwanza. Nawashangaa watu wanaomtetea Lulu nakumlaumu marehemu. Kama Lulu aliweza kudanganya mbele ya media umri wake basi tunajuaje hakumdanganya Kanumba umri wake? Hii kitu ni ngumu sana kulaumu either of the two lakini ni wazi wazazi wa Lulu walijua anadanganya umri publicly lakini wao wahajawahi kukanusha kwenye public umri wa Lulu. What were they getting kwakuficha huu ujinga?

Anonymous said...

kichwa cha habari kimeniboa sana,
Jamani waandishi andikeni habari zenu kisomi mnakuwa kama watu hambao hawana taaluma.
lol!