ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 8, 2012

Dawa pekee itakayookoa nchi hii ni katiba mpya; kazi kwenu Jaji Warioba na timu yako


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba.

NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa nguvu ya kuandika haya nitakayoyaandika nikiamini kuwa yatasaidia jamii.
Ndugu zangu, kupitia Televisheni ya Taifa TBC nilisikiliza kwa utulivu mkubwa hotuba ya Rais wangu, Mheshimiwa Jakaya Kikwete aliyoitoa Mei Mosi mjini Tanga.
Hakika, ilikuwa ni hotuba bora ya Rais Jakaya kati ya alizowahi kuwahutubia Watanzania. Ilileta matumaini kwa wananchi wengi na yenye kuwabana wanafiki wachache ambao wamo ndani ya chama chake CCM.
Niliwasikia watu wengi sana wakiisifia hotuba ile hali iliyonifanya nihisi kuwa anaweza kuanza kuibadili mitazamo ya wengi juu yake, kwani sasa mingi ni hasi.

Alisema wazi kuwa mjadala wa bungeni Dodoma haukumsikitisha bali ulimfurahisha. Anaonekana kana kwamba ametua mzigo mzito lakini niseme wazi kuwa furaha yake yaweza kuwa ya muda mfupi kama asipokwenda sawa kwa vitendo katika kusimamia kazi ya kuwakomboa Watanzania.
Raia wanyonge wa nchi hii, hudhalilishwa sana wakati wa kampeni kwa kuhongwa vijisenti na kupewa pilau na watu wenye nia mbaya ya kutamani uongozi ili watafune fedha za umma ‘kama mchwa.
Katika hotuba yake Rais Kikwete alionekana yupo mbali sana na uozo ulioonyeshwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)na kusababisha baadhi ya wabunge wakiwemo wa CCM wachachamae bungeni na hata kufikia hatua ya kuweka saini zao kushinikiza waziri mkuu ajiuluzu.
Kikwete kwa tafsiri rahisi ni kwamba aliwaambia wananchi wa nchi hii kuwa yuko pamoja nao kwenye kilio chao cha ufisadi uliokubuhu na unaofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji waliopewa dhamana ya kulinda rasilimali za taifa letu.
Ameona na kukiri kuwa kule kwenye halmashauri fedha zinatafunwa utadhani hazina mwenyewe! Rais Kikwete ameonekana sasa kuwa kasimama upande wa umma na kushiriki kwa vitendo kuwaandama viongozi na watendaji waliojigeuza miungu watu na huku wakishiriki wizi wa mali ya umma.
Niliwahi kuandika siku za nyuma kuwa ndani ya nchi hii kuna wachache wanajigeuza ni miungu watu, kwamba wana uwezo wa kutafuna mali za wananchi bila kuulizwa na mtu, nikasema viongozi kama hao wanakiharibia chama tawala hasa kwa vijana.
Hii ni kwa sababu wengi wanaotuhumiwa kushiriki ufisadi wamo ndani ya Chama Cha Mpinduzi (CCM). Ni wenye uhusiano mzuri au kama inavyosemwa siku hizi, ni ’ marafiki’ wa chama tawala.
Lakini watu wengi tunaamini Kikwete anaweza kuweka historia kwa kuongoza kazi ya kuondoa ubaguzi wa kisiasa Tanzania bara maana visiwani tayari amefanikisha hilo.
Anaweza kuondoa ule ukiritimba na ubaguzi ulioota mizizi wa ’Hawa ni wenzetu’ na ’ Wale ni maadui zetu’ ambao msingi wake ulikuwa ni kulindana katika maovu. Tayari ameanza kwa kumteua Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia kuingia bungeni.
Ili kuondokana kabisa na wizi wa kutisha wa mali za umma kama tulivyojionea safari hii, ipo haja ya chama tawala kuwa na utayari wa kugawana madaraka ya uongozi wa kisiasa na vyama vingine. 
Kwa kufanya hivyo ni wazi kuwa tutajenga uchumi imara na amani na utulivu itatawala na niseme wazi kwamba hakuna uchumi unaokua katika nchi yoyote bila kuwepo wa utulivu wa kisiasa.
Ni kweli kabisa kwamba bila kuwa na utawala bora ambao viongozi watakuwa wakiangalia masilahi ya taifa badala ya kuchumia matumbo yao, bila kuwa na demokrasia, kwamba uchaguzi uwe huru na kusiwepo ujinga wa takrima na bila kuheshimu haki za binadamu kwa kila mtu kuheshimika kulingana na sheria za nchi, mafanikio ya kiuchumi hayatawezekana.
Ni jambo linalojulikana na wengi hasa kwa baadhi ya viongozi wa CCM kuwa mambo ya kupanua demokrasia ikiwamo uwepo wa vyama vingi kwao ina tafsiri ya kutishia vibarua vyao! Lakini je kuna mtu katika dunia hii aliwahi kuzuia mabadiliko ambayo jamii inataka na akafanikiwa?
Hivi sasa ndani ya serikali kuna panya watu ambao wapo ghalani wanatafuna fedha za umma na dawa yake ni moja tu, kuwaua na kuwaondoa kabisa katika serikali.
Viongozi wanaochumia matumbo yao ni sawa na panya, waondolewe na kufikishwa katika vyombo husika wapate adhabu inayowastahili.
Wengine wanasema dawa ya panya watu hao ndani ya serikali ni kuundwa kwa Katiba mpya ambayo ndiyo mkombozi wa nchi hii. Ndiyo ambayo itapambana na panya wanaotafuna fedha za umma kwa kuweka utaratibu wa kuwabana kisheria wahujumu wote wa mali za umma.
Itawabana wote wanaopenya kwenye uongozi kwa njia ya rushwa.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema kuwa mtu anayenunua kura ni lazima atarejesha fedha zake kwa kula rushwa.
Panya watu hao wakijua kuwa kuna sheria mama ambayo inatamka hukumu kali ya mtu anayeliibia taifa, basi, wataogopa hata kuiba karatasi katika ofisi za umma.
Mimi naamini kazi ya Jaji Joseph Sinde Warioba na jopo lake la kutengeneza rasimu ya katiba mpya ndiyo itakuwa muarubaini wa wezi wa mali za umma.
Naamini baada ya katiba mpya halmashauri za miji na manispaa zitajenga barabara nyingi za lami na maendeleo yatasonga mbele kwa sababu nyufa za wizi zitazibwa.
Jaji Warioba na wajumbe wote wa kamati yake ni mkombozi pekee wa taifa hili ambalo baadhi ya viongozi wanaona kuiba mali za umma ni staili. Komesheni staili hii kupitia katiba mpya.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli

Chanzo:GPL

No comments: