ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 30, 2012

Magazeti Kenya yapotosha kuhusu Zanzibar



WAKATI nchi jirani ya Kenya ikikabiliana na tatizo la kiusalama linalotishia biashara ya utalii baada ya kulipuliwa kwa maeneo kadhaa nchini humo, Serikali imesema mji wa Zanzibar na Tanzania ni salama kwa watalii. 

Tamko la Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki lililotolewa na Naibu wake, Lazaro Nyalandu jana lilieleza kuwa hali ya ulinzi na usalama kwa watalii ni shwari Zanzibar na Tanzania kwa jumla. 

Nyalandu katika taarifa hiyo, alifafanua kuwa baadhi ya mitandao ya kimataifa na vyombo vya habari vikiwemo vya Kenya, imeripoti kwa upotofu wa makusudi, kuwa kuna hali ya wasiwasi kwa watalii wanaotaka kutembelea Zanzibar. 


Alisema hadi jana, Mji Mkongwe Zanzibar ulikuwa shwari na hakuna taarifa yoyote ya uharibifu wa maeneo ya vivutio vya utalii wala kuchomwa kwa hoteli au kudhurika kwa raia yeyote wa kigeni. 

“Nasisitiza kuwa Zanzibar na Tanzania ni sehemu salama kwa watalii nakuhakikishia wageni ambao tayari wako nchini na wanaotarajia kuja, kuwa vurugu zilizotokea zimeshadhibitiwa na Serikali… hazikuathiri maeneo ya utalii,” alisema. 

Alisema Serikali inahakikishia wananchi na jumuiya ya kimataifa, kuwa vurugu hizo zilikuwa matukio ya pekee na ya kupita na hatua zimechukuliwa na Polisi kuongeza usalama kwa wakazi na watalii. 

Katika kuhakikisha vurugu na uporaji havitokei katika maeneo ya watalii kama ilivyotokea Masaki jijini Dar es Salaam, ambako watalii wanne waliporwa na waendesha pikipiki, Serikali imeimarisha doria katika maeneo kadhaa hususan katika hoteli za kitalii na fukwe. 

Alisema watalii nchini wanakadiriwa kufikia 800,000 hadi milioni moja, huku zaidi ya 200,000 wakikatisha mipaka ya nchi hivyo matukio manne ya kuporwa si kigezo kuwa nchi kutokuwa salama. 

Mkurugenzi wa Utalii, Ibrahimu Musa alisisitiza kuwa yamekuwapo magazeti mbalimbali na mitandao yakiwamo ya ETN yakionesha masuala mbalimbali ya kupinga utalii nchini. 

Alitolea mfano wa Kenya kwamba licha ya kutokea milipuko ya mabomu na vitisho vya ugaidi, vyombo vya habari nchini humo vimekuwa vikifunika matukio hayo kwa kuripoti zaidi vurugu za Zanzibar kuwa ni hatari kwa watalii ili kulinda soko lao. 

Hali hiyo imekuwa ikitokea mara kwa mara nchini humo kwa vyombo vya habari na hata wanasiasa, kudai kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya na wakati mwingine vilipata kutangaza kuwa Ambilikile Mwaisapile au Babu wa Kikombe yuko karibu na nchi hiyo na si Tanzania. 

Hatua hizo zilikuwa zikilenga kuvutia watalii kufikia nchini humo na kuvuka mipaka kuingia nchini, huku kodi zote wakiwa tayari wamezilipa kwa kampuni za utalii za huko na kuikosesha Tanzania kipato. 

Vyombo hivyo vya habari pia vilipata kupiga kelele vikipinga Tanzania kujenga barabara inayokatiza katika mbuga ya Serengeti kwa madai kuwa itaathiri wanyama ambao watahama.


Habari Leo

No comments: