NINAPOANZA mada hii sehemu ya pili, napenda tena nitie mkazo kwamba mapenzi ni magumu. Kama Mzee Nelson Mandela yalimuumiza mpaka akainua mikono kwa mtalaka wake, Winnie, inashindikana vipi kwako?
Ukimpata wa bahati yako, hata uwe maskini unaweza kung’ara na maisha yako yakatawaliwa na faraja, ila ukitumbukia sehemu ambayo si yako, ni mateso ya moyo na sononeko lisilokwisha.
Ukimpata wa bahati yako, hata uwe maskini unaweza kung’ara na maisha yako yakatawaliwa na faraja, ila ukitumbukia sehemu ambayo si yako, ni mateso ya moyo na sononeko lisilokwisha.
Hapa nifafanue kuwa yule ambaye anajiona yupo kwenye uhusiano salama, basi aendelee hapohapo kwa sababu ndipo kwenye bahati yake. Kwa wale wenye maumivu pale walipo, basi wajiangalie mara mbilimbili. Maisha yanaendelea. Maisha bora yanajengwa na mtu mwenye akili iliyotulia.
Huwezi kuwa na matatizo, akili haitulii kwa sababu ya misukosuko ya kimapenzi, ukadhani kwamba utajenga maisha imara. Hapo utakuwa unajidanganya. Tibu kwanza janga lako la mapenzi ili maisha yako yanyooke. Ikiwezekana, jipe muda wa kukaa ‘singo’. Inawezekana.
Beba zingatio kuwa lipo kundi la watu wanaowachezea wenzi wao lakini maisha yao ya kimapenzi bado ni imara. Japo anayetendwa ni maumivu kwake, ila mtendaji ni sawa tu. Haumii, anamnyanyapaa mwenzi wake na anaendelea kupendwa. Ni bahati tu.
Wewe unasaga miguu na kuumiza kichwa. Kila siku unajitahidi kumtafuta mwenzi bora wa maisha yako lakini hujampata. Badala ya furaha, unavuna machungu mtindo mmoja. Usijione una bahati mbaya, badala yake endelea kuitazama mbele kwa matumaini.
Huyo huelewani naye kwa sababu siyo wa bahati yako. Wako yupo na bahati mbaya hujamfikia. Jambo la kufanya si papara, kuwa mtulivu, utampata kwa urahisi. Ukijifanya bingwa wa kuwapanga na kuwapangua, hutafanikiwa, matokeo yake utampita na mwenzi bora wa maisha yako bila kujua.
Penda kutazama mifano kwa walio karibu yako. Je, wanaishi vipi na wenzi wao? Kama nao picha haziendi, tambua kwamba wanalazimishana. Watu wanaopenda, haiwezekani kila siku wakawa wanasumbuliwa na migogoro. Kuna mawili, moja litakuwa sahihi.
Mosi; wote hawapendani ila walijikuta wapo pamoja kwa mvuto wa tamaa za mwili, nao wakajidanganya ni mapenzi, hivyo wakawa pamoja. Pili; kama mosi haikuwa sahihi, basi itakuwa mmoja anapenda, mwingine analeta utani, hivyo kufanya misuguano isiyoisha.
Mapenzi yana nguvu yenye mvutano mithili ya sumaku. Hoja hapa ni kuwa endapo kutakuwa na mapenzi ya kweli, mara nyingi mtajikuta mpo kwenye mstari mmoja, kwani kuna nguvu ya asili ambayo hamuioni, inayowaweka pamoja muda wote. Ni nadra kutofautiana.
Ni lazimka itatokea mara chache kutofautiana kwa maana ninyi si malaika. Mantiki ni kwamba hata kama mnapendana kiasi gani, haiwezekani kila siku wote mkawa mna mawazo ya aina moja, hivyo mtapingana, japo kutokana na mapenzi ya kweli, mtapata suluhu mapema.
Kuna kukosea, kwa hiyo kibinadamu kuna wakati utamkosea mwenzi wako. Ila uwepo wa penzi la kweli, utasababisha muafaka mapema. Utaguswa kuomba msamaha, naye atahamasika kukusamehe. Mvuto wake ndani yake, utamfanya asichelewe kupitisha msamaha. Hayo ndiyo mapenzi.
Ukiona wewe na mwenzi wako mnatofautiana. Suluhu inakuwa ngumu kupatikana. Siku zinapita hamzungumzii tatizo lililowafanya mkawa kwenye sura ya mfarakano. Kila mmoja anajifanya yupo ‘bize’ na mambo yake. Hapo maana yake kuna mambo makuu matatu, na moja lazima ndilo litakuwa sahihi.
Mosi; inawezekana umemkosea kitu kikubwa sana mwenzi wako. Alikuamini mno na hakutaraji kwamba utamfanyia hicho ulichotenda. Kutokana na moyo wake kuingiwa ganzi, inakuwa vigumu kwake kuketi mezani kutafuta suluhu, kwani anakosa imani aliyokuwa nayo awali.
Hapa nikupe angalizo kwamba ni bora uwe huaminiki au imani ya watu kwako iwe ya wastani. Endapo watu watakuwa na imani kubwa kwako, siku wakigundua una nyendo chafu za siri, heshima yako hupotea kabisa. Kama huaminiki, watu wataesema ni kawaida yako. Waliokuamini wastani nao watanena hukuwa ukiaminika asilimia 100, hivyo halitakuwa gumzo.
Unapokuwa unaaminika kwa asilimia 100, maana yake hakuna shaka yoyote kwa watu juu yako. Hivyo basi, unapoboronga, heshima yako itashuka kwa kasi. Mitaani simulizi utakuwa wewe, kwani ni jambo geni na halikuwahi kutabiriwa kwako. Tafadhali, ishi maisha yako, usiishi maisha bandia. Utaumbuka.
Vivyo hivyo kwenye mapenzi. Mpenzi wako anayekupenda na kukuamini kupita kiasi, siku ukimtenda ndivyo sivyo, atakaa na maswali mengi kwa muda mrefu. Utageuka kinyaa mbele yake, kwa hiyo hata kukusamehe atapenda kufanya hivyo lakini atachelewa kwa sababu heshima yako kwake, imeondoka kabisa.
Pili; mapenzi yenu ni kama mnalazimisha. Hampendani kabisa au yeye hakutaki, kwa hiyo anaona hiyo ni fursa ya kukuadhibu. Utashangaa umemkosea jambo dogo lakini anavyolisimamia utadhani umeua mtu. Kama sura ya aina hiyo, inajiri kwenye uhusiano wake, jaribu kutazama mbele kwa matumaini. Hakupendi, atakupotezea muda.
Tatu; mapenzi yake kwako ni ya wastani. Ulivyo kwake, ukiwa naye ni sawa na hata usipokuwa naye, ni sawa vilevile. Huyu atakwambia anakupenda muda mwingine kwa sababu anachulia ni kauli ya mazoea. Ila ukiyatafsiri mapenzi katika kipendelea cha mguso wa moyo. Hakupendi, ila amekusoea.
Kwa mtu wa aina hiyo, mlipaswa kuwa marafiki lakini mkajidanganya mkawa wapenzi. Hizo ni gharama za kulazimisha uhusiano. Elewa kwamba wapo watu ambao ukiwa na urafiki nao wa kawaida, halafu yupo mmoja ambaye ndiye mwenye nafasi yake. Anza kufanya upembuzi leo.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment