POLISI mkoani Shinyanga inamshikilia Mchungaji wa Kanisa la Pentecostal Miracle, Willison Kacheba (65) na mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mwasele wakituhumiwa kumtumbukiza mtoto mchanga katika ndoo kwa lengo la kumuua.
Mchungaji na mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 17 wanadaiwa kumtumbukiza mtoto mwenye saa tatu tangu kuzaliwa, katika ndoo ya plastiki yenye ujazo wa lita 10 akiwa hai.
Mwanafunzi huyo alijifungua mtoto wa kiume juzi saa 9 alasiri nyumbani kwao maeneo ya kata ya Ndala, mjini Shinyanga akiwa na mama yake mzazi aliyemsaidia wakati anajifungua mtoto huyo.
Katika tukio hilo mama mzazi wa mwanafunzi huyo, inadaiwa baada ya kujifungua alihisi kuwa mtoto huyo amefariki kutokana na kumueleza mwanawe kuwa hapumui. Hata hivyo alisema walisubiri waone hali itakavyoendelea.
Baada ya maelezo hayo aliwasiliana na Mchungaji Kacheba, muda mfupi aliwasili nyumbani hapo na zawadi. Mama alitoka nje na kwenda kumuita Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa kuhusu tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo kutoka eneo la tukio, mama wa mwanafunzi alirejea akiwa na Mwenyekiti na walipoingia ndani alimkuta mtoto akiwa amewekwa ndani ya ndoo huku mwanafunzi huyo akiwa amekaa kitandani peke yake na mchungaji akiwa hayupo.
Walimtoa mtoto huyo kwenye ndoo ya plastiki akiwa hai na kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi.
Kaimu Kamanda wa Polisi, Onesmo Lyanga alithibitisha kuwepo tukio hilo na kuongeza kuwa mtoto alipelekwa hospitali kwa uchunguzi wa afya yake.
No comments:
Post a Comment