ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 7, 2012

Mkapa anguruma mahakamani Dar es Salaam

RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa (73) amepanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kumtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi. 

Katika kesi hiyo, Profesa Mahalu anadaiwa kuiibia Serikali Sh. bilioni 2 katika ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini humo.
 

Huku Mahakama hiyo ikiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, Mkapa aliwasili saa 4.45 na kutoa ushahidi kuanzia saa 5.32 asubuhi na kumaliza saa 7.08 mchana. 

Katika ushahidi wake, Mkapa alimmwagia sifa Profesa Mahalu kuwa ni mchapa kazi, mwenye heshima na mwaminifu mkubwa. 

Alidai kuwa hajui aliyemshitaki mahakamani ni nani kwa sababu mpaka anaondoka madarakani, mchakato wa ununuzi wa jengo hilo anajua ulikwenda sawa. 

“Namfahamu Balozi Mahalu kama msomi mzuri, mtumishi mwadilifu …na balozi wetu Bon, Ujerumani,” alidai mahakamani Mkapa alipoulizwa anamfahamu vipi Profesa Mahalu. 

Huku akiongozwa na Wakili wa Upande wa Utetezi, Alex Mgongolwa mbele ya Hakimu 

Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mgeta; mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo: 
Wakili: Mwaka 1995 hadi 2005 ulikuwa wapi? 

Mkapa: Nilikuwa Dar es Salaam nikishika wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania. 

Alipoulizwa uzoefu wake katika mambo ya kimataifa, alifafanua kuwa alipata kuwa Ofisa wa Mambo ya nNje na Balozi wa Tanzania katika nchi za Nigeria, Canada na Marekani. 

Wakili: Ukiwa Rais unafahamu nini kuhusu ununuzi wa jengo la ubalozi nchini Italia? 

Mkapa: Nilifahamu Balozi wetu alifanya ununuzi wa jengo kwa euro 3,098,741.40 kwa maagizo ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa wakati huo alikuwa Profesa Mahalu. 

Wakili: Katika ununuzi mlipewa masharti yoyote? 

Mkapa: Ndio, mimi nilielezwa kuwa mmiliki wa jengo alitaka alipwe mara mbili, kiasi kimoja akaunti moja na kiasi kingine akaunti nyingine na akaunti zote ni za mtu mmoja ambaye ndiye mmiliki wa jengo. 

Maelezo mengine ya Mkapa 

Mkapa aliendelea kudai kuwa Serikali ilitoa baraka na yeye alitaarifiwa na hakuzuia, kwa sababu nia yake ilikuwa ni kupata jengo kwa ajili ya ofisi za ubalozi, hivyo masharti hayo hayakuwa kizuizi kwake. 

Kuhusu mikataba miwili iliyosainiwa katika ununuzi wa jengo hilo, Mkapa alidai kuwa yeye hakumbuki kama alijulishwa, anachojua ni kwamba fedha zingelipwa katika akaunti mbili. 
Amshangaa Lumbanga 

Rais huyo mstaafu alidai kumshangaa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka katika kesi hiyo, Matern Lumbanga, kwa madai yake mahakamani hapo kuwa Serikali haitambui ununuzi wa jengo hilo. 

“Namshangaa sana, kwa nini alisema hivyo wakati mimi Rais nilikuwa na taarifa!” Alisema huku akionesha mshangao. 

Mkapa katika ushahidi wake alidai kuwa angeweza kuzuia ununuzi wa jengo hilo, lakini aliona umuhimu wa kulinunua akatoa amri linunuliwe, ingawa nchi ilikuwa kwenye matatizo ya fedha na fedha za ununuzi huo zingeweza kwenda katika mambo mengine. 

JK atajwa 

Mkapa alipewa taarifa ya kumbukumbu za Bunge ambamo Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo (Rais Jakaya Kikwete), akitoa taarifa bungeni kuwa mwaka 2001/02 wizara hiyo ilinunua jengo hilo la ofisi ya ubalozi Italia kwa Sh bilioni 2.9. 

Kikwete katika taarifa hiyo ya Bunge, alieleza kuwa lengo ni kuondokana na adha ya kupanga kwenye majengo ya watu na kwamba ununuzi wake ulifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na ushauri wa watathimini wa Wizara ya Ardhi na Wizara ya Ujenzi. 

Baada ya kusomewa taarifa hiyo, Mkapa aliulizwa na Wakili Mgongolwa kama kuna usahihi katika taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo, akajibu kuwa taarifa hiyo ilikuwa sahihi na ndicho anachotambua yeye akiwa Rais wakati huo. 

Mkapa alipoulizwa kama kuna malalamiko yoyote kuhusu mchakato wa ununuzi wa jengo hilo yaliyotolewa na Serikali ya Italia au mmiliki wa jengo kuwahi kuyapata baada ya ununuzi, alijibu kwa kifupi. “Hapana.” 

Kuhusu mawasiliano kati ya Serikali na Balozi Mahalu, Mkapa alidai kuwa balozi anaweza kuandika barua kwa waziri wake ambaye ni wa Mambo ya Nje, au Katibu Mkuu Kiongozi au kwa Rais moja kwa moja na kuongeza kuwa mawasiliano mengine yanaweza kufanyika kwa mdomo tu. 

Aliongeza:“Inategemeana na unyeti wa jambo mnalowasiliana.” 

Mawakili wa Serikali 

Katika maswali na majibu na mawakili wa Serikali, Wakili Vincent Haule alitaka kujua tofauti kati ya kiwango alichodai kufahamu cha ununuzi wa jengo hilo cha euro milioni 3.09 na kiwango kilichotajwa bungeni kuwa ni gharama ya jengo hilo Sh bilioni 2.9. 

Mkapa alijibu kuwa yeye mambo ya viwango vya kubadilisha fedha hakuyajua kwa wakati huo, ndiyo maana akataja bei aliyokuwa akiijua na kwamba hiyo haikuwa kazi yake kujua. 

Ashtuka Mahalu kushitakiwa 

Mkapa alidai kuwa hajui aliyeagiza upelelezi dhidi ya ununuzi wa jengo hilo na pia hajui kama upelelezi ulifanywa akiwa madarakani au la, ila alipata taarifa za kushitakiwa Mahalu siku aliyoletwa mahakamani kusomewa mashitaka na pia aliona kwenye magazeti kesho yake. 

Alipohojiwa na Wakili Haule kuhusu ruhusa aliyoitoa kwa mdomo kwa Mahalu kama ilikuwa ya kuridhia mikataba miwili au kuingiza malipo ya jengo katika akaunti mbili alijibu: “Mimi niliagiza ununuzi huo mambo mengine sijui, si kazi yangu mambo ya makaratasi. 

“Nilitoa maelekezo … utekelezaji ni kazi ya wizara, lakini mwisho tulipata ubalozi nilioutaka,” alisisitiza Mkapa. 

Alipohojiwa na Wakili Ponziano Lukosi kuhusu uhusiano wake na Lumbanga, Mkapa alidai alimwamini Katibu Mkuu Kiongozi huyo wa zamani na kumshirikisha katika mambo yote na pia alijua ununuzi wa ubalozi si Italia tu, ila ni pamoja na Marekani, Uingereza na India na akashangaa kudai kwake mahakamani hapo kuwa hajui. 

Alipoulizwa kama anakumbuka jengo lingine walilowahi kununua kwa mfumo huo wa kuingiza fedha katika akaunti mbili, alijibu kwa ukali kidogo; “nakumbuka lakini siwezi kusema…kwa sababu mambo mengine yanaweza kuharibu uhusiano wa nchi na nchi.” 

Baada ya kuonesha ukali kidogo, Hakimu Mgeta aliuliza kama mazingira hayo yapo na Mkapa akajibu kwa kifupi: “Yapo”.

Akijibu swali la Lukosi, aliyetaka kujua kama kulipwa katika akaunti mbili muuzaji wa jengo hilo, haoni kuwa alikuwa akikwepa kodi katika nchi yake, alijibu: “Nitasema kuwa hilo ni tatizo la nchi yake, mimi nimepata jengo nililolitaka nasema alhamdulilah!” 

Kuna wizi? 

Akijibu swali la mwisho la Lukosi kuwa kwa ulipaji huo wa akaunti mbili haoni kuwa ulikuwa ni wizi wa mshitakiwa Mahalu, alijibu; “nitashangaa sana na nitakushangaa wewe, Mahalu ni ni mwaminifu sana.” 

Baada ya jibu hilo, Mkapa alitaka kuongeza neno, lakini akasita akidai: “Unanichokoza utanifanya niongee mengine mengi (anacheka).” 

Kesi hiyo inaendelea leo mahakamani hapo ambapo mshitakiwa wa pili, Grace Martin ambaye alikuwa ofisa wa ubalozi Italia atatoa ushahidi wake.

Habari Leo

No comments: