ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 7, 2012

Msafara wa JK wapata ajali


Rais Jakaya Kikwete akiteremka kwenye gari lake eneo la Kimara Rombo, Dar es Salaam kumjulia hali Askari wa kikosi cha Usalama Barabarani Sajent Steven Laizer, baada ya kupata ajali akiongoza msafara wa Rais kuelekea kwenye msiba wa dereva wa Ikulu, Deokalyus Makwasinga Kimara Kilungule jana. Picha na Fidelis Felix
Kelvin Matandiko na Ibrahim Yamola
MSAFARA wa Rais Jakaya Kikwete jana ulipata ajali baada ya askari aliyekuwa akiuongoza kwa pikipiki kudondoka na kujeruhiwa katika eneo la Kimara, Dar es Salaam.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Kimara Rombo saa 4.30 asubuhi wakati Rais Kikwete alipokuwa akielekea Kimara Kilungule kwenye msiba wa Dereva wa Ikulu, Deokalyus Makwasinga aliyefariki dunia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kupata ajali mbaya ya gari katika eneo la Kimara-Korogwe, Msikitini usiku wa kuamkia Ijumaa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema katika ajali hiyo ya jana, Sanjenti Steven Laizer (D-7380) aliteguka bega na kupata majeraha mbalimbali mwilini na alipelekwa Muhimbili kwa matibabu.

Kenyela alisema chanzo cha ajali hiyo kilitokana na utelezi barabarani kutokana na kunyesha mvua pamoja na tuta la barabarani lililopo karibu na Kituo Mabasi cha Rombo.

“Amepata michubuko kidogo na ameteguka bega lake, ameshapelekwa Muhimbili. Tunawashukuru sana wananchi waliokuwepo maeneo yale, wameonyesha ushirikiano mzuri kwa kweli wameonyesha moyo.”

Mara baada ya askari huyo kudondoka, msafara huo ulisimama na Rais Kikwete aliteremka kutoka kwenye gari lake na kwenda kumjulia hali askari huyo.

Baada ya kumpa pole Sajenti Laizer, aliendelea kubaki pamoja na askari huyo katika eneo la ajali hadi gari la kubebea wagonjwa la Msalaba Mwekundu lilipofika kumchukua kumpeleka hospitali dakika nne baadaye.

Wakati Rais alipokuwa akimjulia hali Sajenti Laizer, walinzi wake walifanya kazi ya ziada ya kuwazuia watu waliokuwa wakisogea eneo hilo kwa lengo la kutaka ama kumsalimia Rais Kikwete au kumuona kwa karibu.

Baada ya majeruhi huyo kupelekwa hospitali, Rais Kikwete aliwapungua mkono wananchi hao alipokuwa akielekea kwenye gari lake kuendelea na safari na wananchi hao waliitikia kwa kumnyooshea mikono mingi hewani.

Awali, akizungumzia hali yake, Sajenti Laizer alisema alikuwa akisikia maumivu makali katika sehemu ya bega lake la kushoto.

Marehemu Makwasinga aliagwa jana na mwili wake kusafirishwa kuelekea Mahenge mkoani Morogoro kwa mazishi.

Januari 2010, msafara wa Rais Kikwete ulipata ajali mkoani Shinyanga wakati gari la polisi lililokuwa likiuongoza kuacha njia na kupinduka na kujeruhi askari.

Walioshuhudia ajali hiyo walisema waliliona gari hilo likiyumba na baadaye kuacha njia na kupinduka kando ya barabara iendayo Meatu.

Katika ajali hiyo iliyotokea katika Kijiji cha Nyikoboko wakati msafara wa Rais ukitokea Kisese alikokuwa amekwenda kuzindua Mto Simiyu unaounganisha Wilaya za Bariadi na Meatu, askari sita walijeruhiwa.

Mei, 2010, magari aliyokuwa amepanda Rais Kikwete akiwa katika ziara yake ya siku mbili Dar es Salaam yalipata hitilafu baada ya magari hayo kuchomoka matairi katika maeneo tofuati yakiwa safarini.

Tukio la kwanza lilitokea maeneo ya Kimara Mwisho wakati Rais alipokuwa akitokea Kimara-Bonyokwa katika alikokwenda kutembelea maeneo yaliyokuwa na matatizo ya maji kwa muda mrefu.

Msafara huo ulilazimika kusimama ghafla kutokana na gari alilokuwa amepanda kuchomoka tairi la mbele.

Katika tukio la pili, msafara wa Rais ulisimama ghafla eneo la bandarini karibu na eneo la Matangini baada ya gari alilokuwemo kuchomoka tari la nyuma wakati akitokea Keko Toroli.


Mwananchi

No comments: