ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 9, 2012

Uko kwenye uhusiano wa aina gani? - 3

INAWEZEKANA upo kwenye penzi la mateso lakini hufahamu. Si ajabu mpenzi wako hana time na wewe na hafikirii chochote baada ya leo, lakini hutambui hilo. Ndugu zangu, haya ndiyo ninayoyazungumzia hasa katika mada yetu inayofikia ukingoni leo.
Nilianza kufafanua kwa undani tangu wiki mbili zilizopita, ni imani yangu kwamba, somo linaeleweka. Katika kuhitimisha, leo tunakwenda moja kwa moja kuona namna penzi la kilaghai linavyokuwa. Hebu twende tukaone.

UTAMJUAJE MPENZI MLAGHAI?
Katika toleo lililopita nilijaribu kuchambua baadhi ya tabia za matapeli wa mapenzi, ambapo tuliona kuwa ni pamoja na kukataa kukutambulisha kwa rafiki zake, kufanya mambo yake kwa kificho na kuweka mipango ya kuwafanya ndugu zenu wasifahamiane.
Hizo ni baadhi tu ya sifa zake, leo tunamalizia kuangalia sifa zilizosalia kabla ya kuangalia kipengele kingine kipya. Karibu rafiki yangu.
Anakuchenga...
Hili ni tatizo lingine kwa mpenzi tapeli, anakuwa mtu wa mambo mengi, kumpata kwake siyo rahisi. Anajifanya mtu wa kazi nyingi ambazo mwanzoni wakati mkikutana hakuwa nazo! Kipindi hiki anakuwa na visingizio vingi visivyokuwa na maana lakini lililokuwa akilini mwake ni kukwepa kuonana na wewe.
Tamaa ya mwili wake imeshaisha kwa maana hiyo haoni kama kuna umuhimu wa kukutana na wewe tena. Ukimwomba mkutane hutoa sababu nyingi ili mshindwe kuonana.
Anapunguza mawasiliano...
Hii ni hatua nyingine ya mpenzi aliyekuchoka, haoni umuhimu wa kuwasiliana na wewe kama zamani na kama akifanya hivyo, ujue ana shida yake muhimu. Inawezekana alishakuzoesha kukupigia simu kila wakati au kukutumia sms za kukujulia hali, lakini kwa wakati huu hawezi kufanya hivyo tena.
Ukiona alama hii ujue mwisho wa penzi lenu unakaribia. Mwanaume wa aina hii anaweza kukupigia simu anapohitaji uende kwake kwa ajili ya kumfulia nguo zake, kumfanyia usafi nyumba/chumba chake, kumpikia na mambo mengine ambayo yatakuwa na manufaa kwake.
Haishangazi sana kuacha kukupigia simu kwa wiki nzima, lakini siku atakayokupigia atasema wazi kwamba anakuhitaji kimapenzi. Kwa maneno mengine ni kwamba, amekufanya wewe chombo cha starehe. Zinduka, toka katika usingizi. Hakuna mpenzi hapo. Anaongozwa na tamaa tu huyo.
Majibu ya mkato
Wakati huu huwa hapimi ajibu nini na lipi aache! Thamani yako kama mpenzi imeshaisha na sasa anakuona kama dada yake tu! Sana sana atakujibu vizuri pale anapokuhitaji.
Wewe kama mpenzi wake una haki ya kumwuliza sababu za kuzima simu kwa saa tatu bila kukutaarifu na inawezekana huo ndiyo utaratibu wenu wa siku zote lakini kwa sasa ukimwuliza, atakupa majibu ya hovyo. Hiyo ni alama nyingine unayopaswa kuifahamu.
Hafurahii ukaribu wenu
Hana furaha kabisa anapokutana na wewe, wakati mwingine anaweza kujisahau na kuonesha wazi kuwa hafurahii kabisa uwepo wako nyumbani kwake. Anaweza kukuuliza muda utakaokaa ili ajue mapema.
Wakati mwingine anaweza kuondoka au kukuambia ana mtoko muda mfupi baada ya wewe kufika kwake. Jiulize, anakwenda wapi penye umuhimu zaidi kuliko wewe? Jambo hili linahitaji akili ndogo sana kujua kwamba jamaa hana time na wewe tena. Sasa unasubiri nini? Kuumizwa na mapenzi?
Hajali...
Hakusikilizi sana kama zamani, ni mtu wa kupuuza kila unachomwambia, lakini kama wewe ni mjanja wa mambo, anaweza kukusikiliza mara chache lakini kwa mambo yanayomhusu yeye. Kwa kifupi thamani na utu wako vinashuka na unakuwa mtu wa kawaida kwake kama walivyo rafiki zake wengine.
Ukiona alama hii, anza kuona taa nyekundu mbele yako, maana jamaa anakutafutia sababu ya kuachana na wewe. Usisubiri hiyo sababu, ondoka mapema na umuache na umapepe wake aone faida yake.
HAYA YATOSHE KUKUFARIJI
Ingiza hili ubongoni mwako; Kila kitu kinafanyika kwa mipango! Hata Mungu mwenyewe wakati wa uumbaji alipanga kuumba kila unachokiona, yeye ndiye anayejua mwanzo na mwisho wa kila kitu. Kama ndivyo, una haja gani ya kuwa na wasiwasi?
Una sababu gani ya kuhisi lazima uolewe na huyo anayekutesa na kuunyong’onyesha moyo wako? Hakika huna haja ya kuumia kiasi hicho! Mungu amekuumba kwa makusudi, amekujalia ukakua, ukasoma hadi ukafikia hapo ulipo hivi sasa.
Hapana shaka kwamba anajua mume wako atakuwa nani, atakuja lini na mtaishi vipi? Anajua pia mwisho wa maisha yako utakuwa ni lini! Kwa misingi hiyo, una sababu gani ya kuendelea kuutesa moyo wako wakati aliyekuumba yupo?
Unafikiri haoni jinsi unavyoteseka, unavyolia na kuumia kwa sababu ya huyo anayekupotezea muda? Anajua.. nenda kwake, msihi akuonyeshe aliyemwandaa kwa ajili yako na siku moja utaishi maisha ya furaha na amani. Sina shaka hakuna nilichoacha. Hadi wiki ijayo kwa mada nyingine.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.

No comments: