ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 30, 2012

UNAPENDWA, UNAACHWA TATIZO NI NINI?

KUACHWA au kuachana kwa wapenzi si jambo la ajabu sana katika jamii, lakini inapotokea wewe unakuwa wa kuachwa kila siku, hapo ndipo kwenye tatizo. Ndiyo zao la mada hii. Kwa nini uingie kwenye uhusiano na kuachwa kila mara?
Msingi wa mada hii ni wanawake, ingawa hata wanaume kuna wakati wanaachwa na wenzi wao. Rafiki zangu, pamoja na ugumu wa jambo hili, lakini inakupasa ukubali kwamba wewe ni tatizo. 

Kuufanya ubongo wako kukubali kuwa wewe ni tatizo, utakuwa mwanzo mzuri wa kutafuta dawa. Ni jambo gumu kidogo kupata hekima ya kugundua jambo hili, lakini waliobahatika wanafanya maamuzi ambayo hayawaumizi mioyo yao.
Haya mambo yanawezekana rafiki zangu. Kwanza ni kukubali kujifunza, kuangalia wapi ulikosea, ni kipindi gani wenzi unaochana nao wanapatwa zaidi na hisia za kukuacha n.k. Baada ya hapo ni rahisi kusogea mbele zaidi katika kujua jinsi ya kutatua tatizo ulilonalo.
Wapo wanawake wengi sana ambao wanahangaika kwa sababu ya kuachwa kila siku. Kila mwanaume anayekuwa naye, baada ya muda mfupi tu, anamuacha! Hajui tatizo, badala yake anaishia kulia tu. Kulia kwako hakutakusaidia lolote kama hutakaa chini na kujiuliza ni wapi kwenye matatizo, ni sehemu gani huwa unakosea.
Una miaka ishirini na nne tu, lakini umeshakuwa na wanaume tisa! Hili ni tatizo, tena kubwa ambalo linahitaji dawa ya kuponya na siyo ya kutuliza maumivu. Twende darasani...
KUJIRAHISISHA...
Kwanza jaribu kujichunguza kama una tabia ya kujirahisisha. Ni kweli umekuwa na tabia ya kujishusha thamani na kuona kama wewe ni kuonewa? Kuchezewa? Mwanaume mwenye ndoto na mwanamke wa baadaye wa maisha yake hahitaji mwanamke wa aina hii.
Anapenda zaidi awe na mwanamke mwenye msimamo anayetambua thamani yake yeye mwenyewe na maisha yake kwa ujumla. Hapendi mwanamke mwepesi kuingilika. Kama utakuwa wa aina hii, hata kama atakuwa amekupenda, ataishia kukutumia na kukuacha, kwani wewe mwenyewe umejionesha wa namna hiyo.
Mwanaume anapenda mwanamke wa kumsumbua kidogo, angalau baadaye apate stori za kusema; “Lakini mama nanilii ulinisumbua!”
Huu ni ukweli ambao baadhi ya watu wanaukwepa. Acha kujirahisisha. Kujirahisisha huku ni pamoja na suala zima la kufanya mapenzi. Usiwe na haraka na tendo hilo, usiulizie juu ya kufanya mapenzi, lakini kama ikitokea jamaa akataka, usikubali haraka. Onyesha msimamo wako, ukiainisha usivyotaka kuchezewa.
JICHUNGUZE MWENYEWE
Wakati mwingine mambo yako yasiyotamanika yanaweza kuwa chanzo cha wewe kuachwa na wenzi wako kila wakati. Angalia tabia zako, tizama mienendo yako, marafiki, kauli na kila kitu ambacho unadhani kinaweza kuwa tatizo.
Mwanaume hapendi kuwa na mwanamke ambaye ana kampani mbaya, kwani anaamini na wewe pia inawezekana ukawa na tabia chafu kama rafiki zako, lakini kauli nzuri kwa mwenzi pia ni kati ya mambo ambayo mwanaume mwenye nia ya kuoa atavutiwa navyo. Jichunguze!
VIPI, UNAJALI?
Kujiona wewe ni bora kuliko wanawake wote hakukusaidii, sana sana kunazidi kukurudisha kwenye matatizo yale yale kila siku. Mwanamke ambaye hajali na haoneshi umakini wakati akizungumza na mpenzi wake, hana sifa ya kuwa mke.
Kama ni kweli unataka kuwa mke, lazima uwe makini, uoneshe kujali kwako na kumuona mwenzi wako kila kitu. Mheshimu, mpe nafasi ya kwanza, hiyo inaweza kuwa safari nzuri ya kuelekea kwenye mafakio.
Jifunze unyenyekevu, ukikosea kuwa wa kwanza kuomba msamaha, kubali kusamehe na hakikisha kwamba unakubali kufundishwa unapokosea. Usiwe mtu usiyejali, ambaye upo tayari kwa lolote, hata kama ni kuachana na mwenzi wako. Hii ni kati ya sumu hatari zitakazokufanya uishie kuachika kila siku.
Bado kuna mengi ya kujifunza marafiki zangu. Wiki ijayo tutaendelea. USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi, anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.

No comments: