KATIKA somo lililopita kama nilivyogusia ushauri wa Brandon King na makala yake ya “Be aware with ones heart” nilieleza kuwa ni kosa kubwa kumuona mwenzi wako ana thamani ndogo na wakati huo huo ukawa unatoa kipaumbele kwa watu wa pembeni.
Tafsiri inayotawala katika uhusiano ni kuwa kundi linalosumbua mno na kuonekana ni sugu kwa tabia ya namna hii ni lile ambalo linawahusisha memba wanaoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi pasipo imani kamili. Wanajaribu na hawana ufahamu kwamba moyo haufanyiwi majaribio.
Hii ndiyo sababu ya kusisitiza kuwa ikiwa hujaamua kupenda basi kaa mbali. Kuna mengi unayoweza kumsababishia mwenzako, ukampotezea muda huku ukimjengea imani upo naye lakini mwisho wa siku anakuja anakuja kujikuta anauguza donda la moyo. Sikitiko la mahaba linashinda msiba!
Hujaumia subiri usimuliwe. Moyo unapouma kwa sababu ya mapenzi hakuna kitu cha kupoza. Unaweza kunywa pombe na usilewe, ukabugia dawa za usingizi na usilale. Kifua kinajaa na kwa sababu inaathiri mfumo wa upumuaji na mapafu nayo huingia katika maumivu.
Sikitiko la mahaba ni hatari, likikufika utapungua uzito kwa kasi bila maelezo ya ziada. Chakula hakiwezi kupita na macho yanaweza kujaa machozi ilhali unatamani kujizuia. Binadamu tumetofautiana, wapo wanaotamani kupendwa lakini wengine wanawacheza shere wanaowapenda.
Dawa kuu ni kujihadhari na watu wasio na mapenzi ya dhati. Kuwaepuka kadiri inavyowezekana. Ni mzuri na anakuvutia lakini heri umuone kwa mbali kwa sababu ukimjaza moyoni atakusumbua. Atakutoa machozi katika eneo ambalo ulihitaji kufurahi.
Maumivu yako hatoyajali kwa sababu hana hisia na wewe. Atakusaliti bila woga kwa maana hana hofu yoyote juu yako. Itakuwa ngumu kumuacha, vilevile utaona uamuzi wowote wa kutengana naye ni mateso makubwa kwamba heri uumie ukiwa naye kuliko kuachana.
Usijidanganye ndugu yangu, wewe ni binadamu uliyekamilika, kwahiyo usitarajie mtu wa pili au wa tatu anaweza kusikia kile kinachokuuma moyoni. Mateso yaliyopo ndani yako unayajua mwenyewe, kwahiyo unatakiwa kuwa wa kwanza kujihurumia na kuchukua uamuzi wa kujiokoa na mateso.
Kuna kitu kimoja ambacho unatakiwa kukifahamu; Binadamu ni wa ajabu sana, watayajua yako ya siri na kile ambacho mwenzi wako anakifanya pembeni, lakini hawakwambii badala yake wataketi pembeni kuzungumza. “Aah yule wa ajabu, anadhani kapata mpenzi kumbe kapatikana!”
Wengine utakaa nao meza moja kushauriana mambo mbalimbali, lakini anayekwambia umvumilie mwenzi wako lisa ya vitimbi anavyokufanyia, ndiyo huyo huyo akikaa pembeni na watu anawaambia kwa mtindo wa kukucheka kwamba unamng’ang’ania mpenzi bomu.
Lingine ni kuwa unapokuwa na mpenzi ambaye hakuheshimu, thamani yako katika jamii inashuka. Kukuheshimu si mpaka akutukane, bali vitendo vyake. Kutoka na wapenzi wengine, kujenga mazoea na watu wa jinsia nyingine kiasi kwamba mpaka anahusishwa kwamba ni wapenzi wake.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment