ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 8, 2012

Njaa ya madaraka imeiua Yanga

Joseph Kapinga
WAKATI mashabiki wa Yanga wakiwa bado wanatafakari kipigo cha mabao 5-0 walichokipata kutoka kwa Simba, baadhi ya wachezaji wa zamani wa  Yanga wamedai kichapo hicho kimetokana na njaa ya madaraka ya watu ndani ya klabu hiyo.

Katika mechi yao ya kufunga msimu wa Ligi Kuu mwaka huu, Yanga ilikubali kipigo cha pekee kwa aina yake baada ya kulala mabao 5-0, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 33 kufungwa idadi kubwa ya mabao kama hiyo.

Wakizungumza na Mwananchi mara baada ya kumalizika mchezo huo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam wachezaji wa wa zamani wa Yanga, Abubakari Salum 'Sure Boy' na Dotto Mokili, walisema ameshangazwa na kipigo ambacho amesema anashawishika kuamini kilikuwa na 'maandalizi' nyuma yake.


Salum 'Sure Boy' ameshangazwa na kipigo hicho, lakini amesema kilistahili, na sababu kubwa ni njaa ndani ya klabu ya Yanga. "Yanga kuna kila aina ya njaa. Wanachama, mashabiki, viongozi njaa tupu," alisema.

"...hivi kwa njaa iliyopo Yanga na mgogoro wa uongozi nadhani inaweza kuifunga Simba? Kwanini nisiseme Simba walikuwa na haki ya kutufunga, tena siyo bao tano hata zaidi. Kwanza kwa wachezaji gani wa Yanga kuifunga Simba. Sikiliza nikuambie, hakuna Yanga mbovu kama ya msimu huu," alisema.

Sure boy aliyesajiliwa Yanga mwaka 1986 akitoka Sigala, alisema Yanga inaweza kuepukana na migogoro kama itabadilisha mfumo na kuwatoa watu wa njaa. "Yanga kuna watu wa njaa wengi kuliko wa mpira, hawa ndio kiini cha tatizo, kwanza hata kulipa ada ya mwaka wanashindwa mpaka mfadhili awalipie."

Kuhusu mchezo huo, alisema wachezaji wa Yanga walionekana kama vile wamelazimishwa kucheza. "Sijapata kuona hali hii, mchezaji hathamini jezi ya timu yake, anacheza kama kafumba macho. Haipo sababu ya kumtafuta mchawi, tulichopanda ndicho tunastahili kuvuna," alisema.

Akiongea kwa masikitiko, Mokili  alisema hajawahi kushuhudia Yanga ikicheza mchezo mbovu kama walioonyesha katika mechi yao na Simba Jumapili iliyopita.

"Hii siyo Yanga nayoifahamu...Yanga gani hii?," alihoji na kuongeza: "Tungeweza hata kufungwa hata mabao 10. Nasema hivi, kipigo hiki kimeandaliwa na mgogoro wa uongozi unaoendelea Yanga."

"Kwa jinsi Yanga ilivyocheza kipindi cha kwanza, kila mmoja alifahamu kwamba Simba wasingechomoka kipindi cha pili, lakini tulichokuja kuona toka kwa wachezaji wa Yanga ni kinyume kabisa," alisema.

Mokili aliyejiunga na Yanga mwaka 1985 akitoka Pan African, alisema katika mchezo huo hasa kipindi cha pili, wachezaji wa Yanga walionekana kucheza kwa maagizo ya kupoteza mchezo huo.

"Sisi tumecheza soka, tunafahamu timu inapozidiwa inacheza vipi, au timu iliyoagizwa kucheza kwa sababu fulani pia tunafahamu inacheza vipi. Kwa hali ya mchezo dhidi ya Simba, hakuna ubishi kulikuwa na 'maagizo' hasa kipindi cha pili. Kama wanayanga, wengi wetu tumeumia na kufungwa mabao 5-0, lakini nataka uamini kuna wenzetu ndani ya klabu wamefaidika."

Akiongelea zaidi mchezo huo, Mokili alisema: "Timu ilirudi kipindi cha pili tukiamini imerekebisha kasoro za kipindi cha kwanza, lakini haikuwa hivyo. Kipa (Yaw Berko) hakurudi, hatufahamu ni kwanini, mabeki wakacheza kwa kujifurahisha, wakafanya makosa mengi yasiyo na ulazima," alisema.

Mokili aliyecheza Yanga pamoja na wachezaji wengi mahiri kama, Peter Tino, Makumbi Juma, Abeid Mziba na Juma Mkambi, alisema mgogoro wa uongozi unaoendelea ndani ya klabu hiyo, ndiyo uliobariki kipigo hicho na kuutaka uongozi kuwajibika na aibu hiyo.

"Nachokiona mimi Yanga, kuna mgogoro wa uongozi, na ili upande mmoja ufaidike ni lazima kuhakikisha upande mwingine unabomolewa. Iko wazi, upande mmoja sasa umeshashinda," alisema.


Mwananchi

No comments: