ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, May 9, 2012

Wachezaji Yanga wadai Sh mil. 127

WAZEE wa klabu ya Yanga wameibua madai mapya dhidi ya uongozi wa klabu hiyo kwamba unadaiwa na wachezaji kiasi cha Sh milioni 127. 

Kutokana na hali hiyo wazee hao wamesema hali ndani ya klabu hiyo si nzuri, hivyo uongozi unapaswa kujiuzulu haraka iwezekanavyo kabla mambo hayajawa mabaya zaidi. 

Akizungumza Dar es Salaam jana katika mkutano na waandishi wa habari, Katibu wa Baraza la 
Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali alisema ni wakati wa Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga na wenzake kuachia ngazi haraka iwezekanavyo kuinusuru Yanga.
 

Akilimali alisema wachezaji wa Yanga wanadai kiasi hicho cha fedha, ambazo ni malimbikizo 
mbalimbali ikiwemo fedha za usajili na kwamba ni chanzo cha wachezaji hao kufanya vibaya hadi Yanga ikafungwa mabao 5-0 na Simba katika mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya timu hizo Jumapili. 

Alisema ili kuimarisha hali ya usalama na amani katika klabu hiyo, inatakiwa Nchunga achukue 
hatua ya kujiuzulu mapema, ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine achukue timu na kwamba 
si vizuri akaondoka kwa aibu zaidi ya ile ya kufungwa mabao 5-0 Jumapili. 

“ Sisi kama waasisi wa klabu hii, ambayo tuna uchungu nayo, tunamtaka Nchunga kuhakikisha 
anafuata ushauri huu kwa hiyari ili kunusuru mtafaruku kwa klabu hii, ” alisema Akilimali. 

Kwa upande wake Nchunga alipoulizwa jana kuhusiana na kauli ya wazee kumtaka ajiuzulu alisema alikuwa akiingia kwenye kikao, hivyo asingekuwa na muda kuzungumzia jambo hilo lakini alikiri kuna wachezaji wanadai kiasi kidogo cha fedha na si hizo Sh milioni 127 zilizotajwa na wazee. 

Alisema wachezaji wanaodai ni watatu ambao ni Jerry Tegete anayedai fedha za usajili za miaka ya nyuma ambazo ni chache, Nurdin Bakari na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambao pia wanadai fedha kiasi walizoongeza mkataba lakini pia si za kiwango kikubwa. 

Alishangaa kusikia madai hayo na kwamba hata posho kuhusiana na mechi mbalimbali wamelipwa na kiasi kilichobaki ni kidogo na kwamba katika malipo hayo walimhusisha Nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, hivyo hakuna malalamiko. 

Aliwaomba wanachama na mashabiki wa Yanga kutosikiliza maneno ambayo yana nia ya kuwachonganisha wachezaji na viongozi hivi sasa na kwamba uongozi wa Yanga unawatimizia mahitaji yao wachezaji wake.

Habari Leo

No comments: