CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimeipa Serikali mwezi mmoja kulipa madeni ya walimu yanayofikia Sh bilioni 13 za mishahara na zingine, vinginevyo kimesema kitachukua hatua zaidi.
Aidha kimeitaka Serikali kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 100 katika bajeti ijayo na ianze kulipwa Julai.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akitoa tamko la Kamati ya Utendaji ya Taifa ya chama hicho kuhusu madai ya walimu nchini.
Mukoba alisema pia Kamati hiyo iliitaka Serikali iingize kwenye bajeti posho ya kufundishia ya asilimia 55 kwa walimu wa Sayansi na asilimia 50 kwa wale wa Sanaa.
Kuhusu madai ya walimu, Mukoba alisema endapo madai hayo hayatalipwa katika muda uliopangwa, CWT itakutana na kuchukua hatua nyingine zaidi ambazo hakuzitaja.
Akizungumzia madeni hayo, Desemba mwaka jana Wizara ya Fedha ilitoa Sh bilioni 22.5 kwa ajili ya kulipa madeni ya walimu yasiyohusu mishahara.
“Kati ya fedha hizo Sh bilioni 19.2 zilikuwa za walimu walio chini ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Sh bilioni 3.2 zilipelekwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,” alisema Mukoba.
Alisema hadi Machi kati ya fedha zilizotengwa kulipa walimu, Tamisemi ilikuwa ililipa Sh bilioni 16.6 na kubakiza Sh bilioni 2.6.
Mukoba aliongeza kuwa hadi Aprili 18, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilikuwa imelipa Sh milioni 800 kati ya Sh bilioni 3.2 zilizotengwa kwa kazi hiyo.
“Kamati ilipokea taarifa ya ulipwaji wa madeni yaliyotokana na mishahara na walimu waliopandishwa vyeo bila kulipwa na kubaini kuwa Serikali inadaiwa zaidi ya Sh bilioni 10 hadi kikao cha Machi 8 na kwamba uamuzi wa Serikali kulipa deni hilo kwa Sh bilioni mbili kila mwezi hautamaliza tatizo kwa kuwa linazidi kuongezeka,” alisema.
Alisema pia kwamba walimu 45,000 waliopandishwa madaraja hawajarekebishiwa mishahara yao na waliorekebishiwa hawajalipwa mapunjo ya nyuma.
No comments:
Post a Comment