ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 12, 2012

Wivu una dawa, soma hapa upone-4

Na Luqman Maloto
Leo tunahitimisha mada yetu ya wivu wa kimapenzi na namna ya kuutatua. Tuendelee kuanzia pale tulipoishia wiki iliyopita.
2. USIISHI KWA DHANA
Hutokea mtu ameketi, ghafla anaanza kusumbuliwa na mawazo kuwa mwenzi wake yupo sehemu ya hatari akifanya mambo yasiyokubalika. Hili ni tatizo la wivu ambalo huwatesa wengi, hivyo kuelekea kukamilisha mada hii, nakutaka uachane na maishi ya dhana. Tafsiri matukio. Dhana ikitawala maisha yako, utakuwa unapenda kutuhumu bila hoja. Mbele ya safari ya maisha yako ya kutuhumu, utajikuta ni mwingi wa mawazo na kujiumiza moyo pasipo maelezo yoyote. Hujawahi kumfumania mwenzi wako lakini humuamini tu. Hii inamaanisha wewe mwenyewe hujikubali.

Tambua kuwa kama unafikiria mabaya kwa mwenzi wako bila sababu, hiyo ni dalili ya kukosa uaminifu. Mantiki hapa ipo kwenye hoja kuwa kuwaza kwamba mwenzi wako anafanya madudu, inamvunjia heshima, vilevile nawe unakuwa kwenye kapu baya, kwani si muaminifu. Jihadhari na tatizo hilo.
Unaweza kupona kwenye kipengele kuwa si muaminifu kama kuna jambo aliwahi kukufanyia, hivyo ukamtoa imani. Hata hivyo, muongozo kwako uwe kwenye ukweli kuwa kama mlishaketi, mkazungumza na kukubaliana kusameheana, hutakiwi kutomuamini, kufanya hivyo ni kujiumiza. Usiishi kwa wasiwasi.
Kuna msemo: Aliwazalo mjinga ndilo linalomtokea. Maana yake ni kuwa matukio ambayo unaweza kuyaunga kwenye ubongo wako, ni rahisi kukutokea. Hutakiwi kuwaza mabaya, hebu tafakari mambo katika sura chanya. Mheshimu mwenzi wako naye akupe heshima yako unayostahili.
Ikiwa utawaza mambo mabaya, inawezekana ukamgombeza. Ukamnyima raha. Maswali yakawa mengi, huku ukimjaza tuhuma lukuki. Mwisho wa kero zake, naye atakasirika, hivyo ikiwa ana akili chafu, anaweza kufanya kweli ili unayowaza yatimie.
Unaweza kumpigia simu mwenzi wako lakini akashindwa kupokea. Usikimbilie kufikiria yupo hotelini anafanya uchafu, fikiria kazi zake kuwa ni nyingi. Baadaye akikupigia, usipande jazba kuwa hakupokea simu yako, zungumza naye kwa upole, kama ni maswali muulize kwa lugha laini.
Anza leo kufanyia kazi hili: Umempigia simu mwenzi wako, hajapokea. Baadaye ukimpata hewani au akikupigia, kabla ya kuzungumza lolote, unaanza kumpa pole kwa kutingwa na mambo mengi mpaka akashindwa kupokea simu ulipompigia. Hiyo ina maana kubwa, inaepusha migogoro.
Ipo wazi kuwa ubongo wa mtu mwenye wivu, hufikiria kwamba anasalitiwa kila anapopiga simu ya mwenzi wake na kutopokelewa au kuchelewa kupokelewa. Hawezi kufikiria kama mpenzi wake anaweza akawa amepata ajali. Kama simu haipatikani, hatafikiria kuwa betri imekufa. Atawaza mambo mabaya tu.
1. TAFAKARI KWA NINI UNA WIVU
Je, kuna kitu kilitokea nyuma kwenye uhusiano wenu ndiyo maana umeondoa imani juu yake? Unaogopa kwamba kuna jambo litatokea? Kwamba mpenzi wako ataanzisha uhusiano na mtu mwingine au atakuacha jumla? Wivu hautakiwi lakini ni ukweli usio na shaka kuwa matukio ya nyuma hukaribisha wivu.
Inawezekana mtindo wa maisha ya mwenzi wako ukawa kichocheo cha wewe kumuonea wivu. Ikiwa umetafakari na kugundua hivyo, muweke chini mzungumze. Muweke bayana kwamba anatakiwa kubadilika ili nafsi yako iwe na amani kamili.
Pengine kwenye uhusiano uliopita ulitendwa. Ukafanyiwa mambo mabaya mpaka ukajihisi huna thamani. Sasa unahisi hata huyo uliyenaye anaweza kufanya yaleyale yaliyokuumiza. Katika hilo, una haki ya kuona wivu kwa maana wanasema mtu akigongwa na nyoka, siku akiguswa na jani hushtuka.
Hata hivyo, katika hali kama hiyo wivu wako utakuwa unaongozwa na wasiwasi, hivyo unaweza kutulia kwa njia ya mazungumzo. Usikae na sononeko la moyo, zungumza na mpenzi wako kwenye kila jambo ambalo unahisi linakukwaza. Inawezekana kwako ni kubwa lakini mbele ya mwenzi wako ni dogo na ufumbuzi wake ni rahisi.
HITIMISHO
Kujua jinsi ya kuikabili hali yako ya wivu itakusaidia kwenye maisha yako. Na unapaswa kulitilia mkazo kabla wivu haujaharibu uhusiano wako. Ni watu wachache mno wanaoweza kuwa hawajijui kama wana wivu au la, kwa hiyo ni rahisi kuukabili kwa sababu ni rahisi mhusika kujijua.

www.globalpublishers.info

No comments: