ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 21, 2012

BALOZI WA SAN MARINO AMSHUKURU MIGIRO KWA USHIRIKIANO

 Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro akiwa na mwenyeji wake. Balozi Daniele Bodini wa San Marino. Balozi Bodini aliandaa chakula cha mchana kwa  heshima ya Naibu Katibu Mkuu kwa kutambua mchango wake na ushirikiano mkubwa wakati wa  uongozi wake.
Naibu Katibu Mkuu akiwa pamoja na mwenyeji wake na waalikwa wengine walioshiriki chakula cha mchana kilichoandaliwa na Balozi  Daniel Bodini wa San Marino. kutoka kushoto ni Bw. Parfait Onanga Anyanga, Mkurugenzi katika Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu, Balozi wa Mongolia, Bi. Enkhtsetseg Ochir, Balozi wa Nigeria, Bibi. Joy Ogwu,  Balozi Bodini, Dkt. Asha- Rose Migiro na Bw. Vijay Nambier aliyekuwa Msimamizi Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu  na  ambaye sasa ameteuliwa  kuwa Mwakilishi Maalum  wa Ban Ki Moon huko  Myanmar .

 ------------
Balozi wa  Jamhuri ya San Marino katika Umoja wa Mataifa, Bw. Daniele Bodini amemuelezea Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro kama kiongozi ambaye katika  uongozi wake daima aliweka mbele maslahi ya nchi zote bila ya kujali ukubwa au udogo wa nchi . Balozi Bodini ametao kauli hiyo siku ya jumatano wakati alipomuandalia chakula cha  mchana Dkt. Asha-Rose Migiro kumshukuru kwa mchango wake na ushirikiano aliouonyesha wakati wa uongozi wake. Chakula hicho cha mchana kiliandaliwa katika makazi ya  Balozi Bodini na kuwashirikisha pia Balozi wa Nigeria katika Umoja wa Mataifa Bibi Joy Ogwu,  na Balozi wa Mongolia Bi. Enkhtsetseg Ochir. Aidha  Balozi huyo wa San Marino   Akasema yeye binafsi anashukuru kwa kupata nafasi ya kufanyakazi kwa karibu na Naibu Katibu Mkuu katika maeneo mbalimbali  yakiwamo  utekelezaji  wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia, uanzishwaji wa UN -Women,  masuala ya Ulinzi na Usalama na  System wide Coherence.
 Vile vile  akasema  Migiro amekuwa mfano wa kuigwa  na wanawake, wasichana na watoto wa kike ambao wanamchukulia yeye kama kielelezo cha mafanikio ya wanawake  na kwamba ameatia moyo wengi. Akabainisha kwamba yako mambo mengi ambayo Migiro ameyafanya wakati wa uongozi wake na kwamba hapana shaka yataendelea kukumbukwa katika Umoja wa Mataifa. Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu akamshukuru kwa heshima hiyo na  kwa ushirikiano aliompatia  katika, pamoja na mambo mengine  kutekeleza majukumu aliyokuwa amekabidhiwa ya kumsaidia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Akasema daima ataienzi heshima hiyo na kuwashukuru wale wote ambao wameshirikiana  naye kwa karibu katika  utekelezaji wa masuala mengi na muhimu kwa maendeleo ya mwanadamu.


No comments: