Mhe. Balozi Mawanaidi Maajar na Mhe. Asha Rose Migiro
Na Mwandishi Maalum
Naibu Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro amewaasa watanzania kwa kusema, hakuna jambo njema katika utumishi wowote ule
uwe wa kuajiriwa serikalini, katika sekta binafsi au hata kujiajiri mwenyewe
kama kuwa na utumishi wenye nidhamu.
Anasema ni nidhamu tu
ndiyo itakayomuwezesha mfanyakazi
kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu, Uadilifu na uwajibikaji.
Ametoa wasia huo
wakati alipokuwa akisalimiana na
watanzania waishio jijini, New York, Washigton DC na vitongoji vingine. Wakati wa
hafla ya kusherehekea mafanikio yake ya kushika wadhifa wa Unaibu Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa kwa Miaka mitano na nusu. Hafla hiyo iliandaliwa kwa
ushirikiano wa jumuia za watanzania NY na DMV
na Balozi za Tanzania nchini Marekani na Umoja wa Mataifa.
Katika hafla hiyo
iliyofanyika katika makazi ya Balozi wa Tanzania New York, Migiro anasema hata
yeye asingefika hapo alipo au hata asingemaliza miaka hiyo mitano na nusu kama
asinge onyesha nidhamu ya hali ya juu katika kazi.
“ Tumekusanyika
hapa kusherehekea mafanikia haya, haya si mafanikio yangu binafsi ni mafanikio
yetu
sote, ni mafanikio ya nchi yetu ni mafanikio ya Bara la Afrika. Lakini
nimefika hapa nilipo pamoja na mambo mengine ni suala ninadhamu ,nidhamu ile tuliyofundishwa zamani
mashuleni. Kwa sababu hiyo ninawaomba na
nyie muweke mbele nidhani katika kazi na shughuli zenu” akasisitiza Dkt. Asha- Rose Migiro.
Aidha Migiro anasema
kwamba utumishi wenye kuweke mbele
nidhani si jambo geni kwa sababu ni nidhamu hiyo hiyo iliyoonyeshwa na viongozi
waasisi wa taifa la Tanzania , waliopita na waliopo ndiyo imeifanya Tanzania
kuwa kama ilivyo na kutambulika
kimataifa.
“Tumefika hapa, kwa
sababu viongozi wetu walifanya kazi kwa
nidhamu sana, wakafyeka misitu na mapori, wakaua majoka,
kazi ambayo imetuwezesha sisi kupita na kufika hapa tulipo” akasititiza.
Katika mazungumzo
hayo ambayo mara kwa mara yalikuwa yakibwagizwa kwa “Tanzania
Oyeee”. Naibu Katibu Mkuu, pia amewataka watanzania kudumisha amani, upendo,
mshikamano na umoja.
Anasema kwamba katika
nafasi yake ya unaibu katibu mkuu, ameyaona mengi, ameyasikia mengi kiasi cha
kumfanya aienzi amani na mshikamano
walionao watanzania.
“ Jamani hakuna jambo
jema kama kuwa na amani, kama kuwa na upendo, kama kuwa na mshikamano. Nikiwa
katika jengo lile nimeona na kushuhudia mengi. Ndugu zanguni, ninawaombeni
sana, tuendelee kuienzi , kuilinda na kuidumisha amani yetu, amani na utulivu
wetu ni sababu nyingine inayotufanya
tuwe tofauti na nchi nyingine” akasisitiza Migiro.
Awali akimkaribisha
Naibu Katibu Mkuu kuwasalimia watanzania, Balozi wa Tanzania Nchi Marekani, Mwanaidi Maajar yeye
alimuelezea Migiro kama kiongozi mwanamke
na mama ambaye amekuwa kivutio
kikubwa kwa wanawake wengi kwamba hata wao wanaweza kuja kuwa kama Migiro.
Akamtaja Asha- Rise Migiro, kuwa
kiongozi anayethamini kazi, na pia
ni mtu wa kujituma na mwenye nidhamu sana hapana shaka amefika hapo alipo.
Akasema kuwa utumishi
wa kutukuka, nidhamu kazini na moyo wake wa kujituma na kusaidia watu wanyonge ameanza nao zamani
sana tangu akiwa shuleni na hatimaye aliposhika
nyadhifa mbalimbali serikalini na katika Umoja wa Mataifa.
“ Ninamfahamu vizuri
sana, tumepita pamoja katika sehemu mbalimbali,
kuanzia shuleni , chuo kikuu na hasa wakati tunafanya kazi ya kuwasaidia wanawake waliokuwa wanataka
msaada wa kisheria, ni mtu wa nidhamu kweli kweli, anayejali muda na wakati”
akasisitiza Balozi Maajar
Balozi Maajari akasema miaka mtano na nusu ya unaibu katibu mkuu wake katika umoja wa mataifa, ni miaka ambayo imeiweka Tanzania katika ramani ya uso
wa dunia, lakini ni miaka ambayo kila mtanzania amejivunia nayo na kwa
wanawake imewapa changamoto ya kujituma
zaidi na kufanya kazi kwa bidiii zaidi.
No comments:
Post a Comment