HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO (MB), WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI, KUHUSU MAPENDEKEZO YA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
_______________
I. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, ninatoa maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Bajeti ya Nchi ya mwaka wa fedha 2012/2013 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99(7) toleo la Mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, Natoa pongezi za dhati kabisa kwa Ndugu William Augustao Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa kwa kuteuliwa na Rais kuwa Waziri wa Fedha na Uchumi. Vile vile nawapongeza Ndugu Saada Mkuya na Ndugu Janeth Mbene kwa kuteuliwa kwao kuwa Wabunge na baadaye kuwa Manaibu Mawaziri katika Wizara hii nyeti sana. Ninawapa pole pia maana Wizara ya Fedha sio Wizara lelemama. Kambi ya Upinzani itaendelea kuisimamia Wizara hii kwa ukaribu sana kama ilivyofanya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Mtakapofanya vizuri tutawapongeza ili muongeze juhudi, mtakapoharibu tutawawajibisha.
Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba Mwaka wa Fedha uliopita ulikuwa mwaka mgumu sana kwa Watanzania. Ni mwaka ambao gharama za maisha zilipanda kwa kasi kubwa sana na juhudi za Serikali kuwakwamua wananchi na hasa wananchi wanyonge kutoka kwenye lindi la ufukara ziligonga mwamba. Kambi ya Upinzani inawapa pole Watanzania kwani hili ndilo walilochagua. Muhimu ni kuvumilia mpaka uchaguzi ujao na kufanya mabadiliko ya Serikali ili kuweka Serikali itakayoongozwa na CHADEMA na itakayoweza kukabili changamoto za sasa na za baadaye.
Mheshimiwa Spika, naomba tufanye mapitio kidogo ya Bajeti inayomaliza muda wake.
- UTEKELEZAJI WA BAJETI ILIYOPITA
Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani ni vema kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali iliyopita ili kuona ni kwa namna gani Serikali inathamini fedha za walipa kodi, na dhamira yake ya kuleta maendeleo ya kiuchumi katika Taifa. Katika kufanya hivyo, tutapitia baadhi ya maeneo ambayo Kambi ya Upinzani tunaona kuwa hayakutekelezwa katika bajeti iliyopita.
Kupunguza Makali ya Maisha
Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali ilitangaza nia yake ya kupunguza makali ya maisha. Hatua mbali mbali zilichukuliwa ikiwamo kupunguza kodi na tozo kwenye mafuta ya Dizeli na Petroli, kuanza kutekeleza mpango wa dharura wa umeme na kutoa fedha za kununua chakula kwa Wakala wa Chakula. Serikali ilitumia shilingi bilioni 296 na dola za Marekani milioni 183 kwenye Umeme. Vilevile Serikali ilitumia shilingi bilioni 27 kununua Mahindi na kusambaza kwenye masoko.
Mheshimiwa Spika, licha ya hatua hizo zilizochukuliwa Mfumuko wa Bei uliongezeka maradufu kutoka wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2011/12. Serikali imefeli katika lengo lake la kupunguza makali ya maisha kwa wananchi. Sio tu kwamba Serikali imeshindwa kudhibiti upandaji holela wa gharama za maisha bali pia hatua za Serikali zimeongeza kasi ya kupanda kwa makali ya maisha.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni katika Hotuba yake mbadala ya mwaka 2011/12 iliitaka Serikali kushughulikia msingi wa mfumuko wa Bei hapa nchini ambao ni uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula. Tumeelezwa na Waziri Kivuli wa Mipango na Uchumi kwamba Chakula peke yake ni asilimia 48 ya kapu la bidhaa na huduma ambazo mwanachi anatumia. Mfumuko wa Bei ya Chakula kinacholiwa nyumbani na kwenye migahawa ilikuwa asilimia 25 mwezi Aprili 2012 (BoT monthly Economic Review, May 2012). Vile vile mfumuko wa bei wa nishati inayotumika nyumbani na mafuta ya Dizeli na Petroli ulifikia asilimia 25 pia mwezi Mei mwaka 2012. Ni dhahiri kwamba iwapo tutadhibiti mfumuko wa bei ya chakula tutaweza kushusha mfumuko wa bei kurudi kwenye tarakimu moja.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapendekeza hatua zilezile ilizofanya mwaka wa fedha unaokwisha kwa kutoa vibali kwa Wafanyabiashara vya kuagiza Mchele na Sukari. Katika hotuba yake Waziri wa Fedha anasema ‘….Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari bila kutoza ushuru wa forodha kiasi cha tani 200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa bei ya Sukari…’(uk 9 ibara ya 15). Baada ya hatua hii bei ya Sukari ilipanda kutoka tshs 1700 mpaka tshs 2800 kwenye maeneo mengi nchini. Waziri wa Fedha katika hotuba yake anatoa suluhisho. Ninanukuu. ‘…hatua za haraka ambazo Serikali itachukua ni pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa Sukari na mchele kutoka nje….’! Serikali inachukua hatua zilezile kwa tatizo lile lile ikitegemea matokeo tofauti.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inarejea pendekezo lake la mwaka jana kwa Serikali kutoa vivutio kwa wakulima wadogo kuzalisha chakula kwa wingi. Miongoni mwa vivutio hivyo ni:
i. Kuwekeza kwenye barabara za vijijini ili mazao yao yafike kwenye masoko na kupata bei nzuri,
ii. Kuwekeza kwenye Usambazaji wa Maji vijijini ili kina mama wasitembee mwendo mrefu kutafuta maji na hivyo kutumia muda mwingi kwenye uzalishaji,
iii. Kuwekeza kwenye Umeme vijijini ili wafanyabiashara wa vijijini waongeze thamani ya mazao. Kwa mfano, kuuza Unga badala ya Mahindi.
iv. Kuwekeza kwenye miundombinu ya Umwagiliaji vijijini ili wakulima wazalishe muda wote wa mwaka.
v. Kuwekeza kwenye Elimu vijijini na pia Afya vijijini ili wananchi wetu wawe na Afya bora na waelimike katika mbinu za uzalishaji bora.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa, hakuna mbadala wa kudhibiti mfumuko wa bei zaidi ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwekeza kwa wananchi wetu. Serikali inafikiria uzalishaji utaongezeka kwa kusaidia wakulima wakubwa ambao watageuza wananchi wetu kuwa Manamba na vibarua ndani ya nchi yao. Tuwekeze kwa watu wetu vijijini ili waongeze uzalishaji na kwa kufanya hivyo mfumuko wa Bei ya chakula utakuwa historia. Hakuna mwarobaini wa kupanda kwa bei za vyakula isipokuwa Kilimo.
Mhesimiwa Spika, Tunatambua kuwa hatua tunazotaka Serikali ifanye ni za muda wa kati. Kwa muda mfupi tunataka Bodi ya Mazao mchanganyiko, Wakala wa Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Sukari zipewe fedha kuagiza Mchele na Sukari na pia kununua kutoka kwa wakulima na kusagisha Mahindi. Wafanyabiashara waagizaji wa Chakula washindane na Taasisi hizi za Umma badala ya kuwapa vibali ambavyo hutolewa kwa rushwa na hivyo kuongeza bei za bidhaa hizo.
Kuwezesha Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira.
Mheshimiwa Spika, Serikali imesema kwamba ilichukua hatua mbalimbali kukabiliana na tatizo la Ajira kwa kuongeza fursa za ajira. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza mitaji katika Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki ya Posta na Twiga Bancorp. Pia Serikali imetangaza kwamba imeajiri walimu, maafisa ugani na watumishi wa Afya. Hatua kama hizi pia zimetangazwa kwa mwaka wa Fedha wa 2012/13 ambapo pia Serikali imetangaza kuajiri watumishi 71,756.
Mheshimiwa Spika, Duniani kote Serikali haizalishi ajira bali ajira huzalishwa na Uchumi mzima ambapo Serikali ni sehemu tu ya Uchumi (Jobs are created by the economy). Takwimu zinaonyesha kwamba kila mwaka Tanzania inaingiza kwenye soko la Ajira watu takribani laki saba. Shughuli za Uchumi zikiongezeka ndio Ajira zinatengenezwa. Serikali inafikiria nini kuhusu vijana takribani milioni nane walio shule za Msingi hivi sasa, Vijana milioni 1.7 walio katika Shule za Sekondari hivi sasa, Vijana 200,000 waliopo vyuo vya Ufundi na Wanachuo 180,000 walio katika Vyuo vya Elimu ya Juu (takwimu kutoka kitabu cha hali ya uchumi, 2012 sura ya 19). Serikali ambayo bado inategemea takwimu za Ajira za Mwaka 2006 inajitamba kwa kuajiri watu 70,000.
Mheshimiwa Spika, Jukumu la Serikali ni kujenga mazingira ya wananchi kupata ajira ama kwa kujiajiri au kwa kuajiriwa na shughuli za uchumi. Lakini ukweli ni kwamba Serikali imeshindwa kushughulikia tatizo la Ajira na hasa ajira kwa vijana. Tatizo la Ajira kwa Vijana ni Bomu litakalokuja kutulipukia vibaya sana kama hatutakuwa makini nalo. Hii ni nchi ya Vijana. Kutoshughulikia masuala yao ni kutoshughulikia masuala ya nchi.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya ajira kwa vijana Bajeti mbadala imeiwekea mikakati mipana ya kiuchumi kwa kuanzisha miradi mikubwa ya Umma itakayomeza vijana waliopo mtaani na kuanzisha kwa makusudi na kwa kasi Vyuo vya Ufundi stadi na Vyuo vya Ufundi na Mafunzo vingi. Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza Uwekezaji wa Miundombinu Vijijini kama njia ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana. Vilevile tunapendekeza Miradi mikubwa ya kuongeza mazao ya Kilimo hasa Pamba, Korosho na Katani ili kupanua Ajira. Kambi ya Upinzani pia inapendekeza kujenga VETA katika kila Halmashauri ya Wilaya na Chuo cha Ufundi katika kila Mkoa ili kutoa ujuzi kwa vijana ili waweze kukabili maisha yao. Badala ya Serikali kukopa kwa ajili ya Matumizi ya kawaida, Serikali ikope kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi na vyuo vya Ufundi na Mafunzo. Ni Lazima viongozi sio tu tuwe makini bali tuonekane kuwa makini tunaposhughulikia suala la Ajira kwa Vijana.
Sera ya Mapato
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni ilitangaza vipaumbele katika sera ya Mapato ambavyo ni pamoja na kukusanya Mapato ya Serikali mpaka zaidi ya asilimia 20 ya Pato la Taifa ili kuwezesha kujitegemea kupata fedha za miradi ya maendeleo. Pia Kambi ya Upinzani inakusudia kufanya marekebisho mbalimbali ya sheria za kodi ili kulinda viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi za kilimo na mifugo za hapa nchini, kupanua wigo wa Mapato kwa kutunga sheria ya kulazimu kila Mtanzania kujaza fomu za marejesho ya kodi na kurekebisha viwango vya kodi ya Mapato (PAYE). Vile vile tunapendekeza kufanya marekebisho ya sheria za kodi kwenye sekta za madini na mawasiliano ili kuongeza mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha 2011/12 Serikali ilichukua hatua mbalimbali katika masuala ya Kodi. Katika Bajeti mbadala pia tulipendekeza hatua mbali mbali ambazo tuliona zitaongeza mapato ya Serikali na hivyo kutuwezesha kuendeleza nchi yetu. Baadhi ya hatua mbalimbali tulizopendekeza Serikali imetangaza kuzitekeleza.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani katika Bajeti Mbadala ya mwaka 2011/12 ilipendekeza masuala yafutayo ili kuongeza mapato ya Serikali.
- Hatua zifuatazo zilipendekezwa ili kuweza kukabiliana na ukwepaji wa kodi unaofanywa na makampuni makubwa ya kimataifa (Multinational Corporations) na hatimaye kulipunguzia taifa mapato:
(i) Kutunga sheria kwa kuimarisha zaidi sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 kwamba, mikopo ya makampuni kwenye uwekezaji, kwa sababu za kikodi, isizidi asilimia 70 ya mtaji wote uliowekezwa na hii ianze mara moja bila kujali mikataba iliyopo.
(ii) Kutunga sheria kuhakikisha kwamba riba kwenye mikopo kutoka Makampuni yanayohusiana (sister companies) haitaondolewa kwenye kutoza kodi (not tax deductible).
(iii) Kuhakikisha kwamba mauziano ya Kampuni yoyote ambayo mali zake zipo Tanzania yanatozwa kodi ya asilimia 30% kama ‘ongezeko la mtaji’ (‘capital gains’).
Mheshimiwa Spika, katika mapendezo haya ni pendekezo moja tu ndilo limechukuliwa na Serikali katika Bajeti ya mwaka 2012/13 nalo ni pendekezo la ‘capital gains tax’. Hata hivyo Pendekezo la Serikali lina makosa makubwa sana ya kifundi. Waziri wa Fedha Mhe. Mgimwa amesema, ninanukuu ‘Kuanzisha kodi itokanayo na uuzaji wa rasilimali ya uwekezaji (capital gains tax) kwenye uuzaji wa HISA za kampuni mama ya nje ya nchi’
Mheshimiwa Spika, Ukisoma pendekezo letu kwa haraka utaona kama Serikali imelichukua lilivyo, lakini kwa jicho la kiuchumi pendekezo la Serikali na lile la Kambi ya Upinzani ni mambo tofauti sana. Pendekezo la Serikali linazungumzia HISA. Mamlaka ya Mapato Tanzania haitakuwa na mamlaka (jurisdiction to tax) kutoza kodi kwa Kampuni mama (as a source or even residence). Mamlaka ya Mapato Tanzania ina mamlaka na Mali (assets) zilizopo Tanzania za Kampuni mama. Kwa mfano, wakati kampuni ya Barrick inanunua mgodi wa Bulyanhulu haikuinunua Kampuni ya Kahama mining ltd bali ilinunua hisa zote za Kampuni ya Sutton Resources. Vile vile, wakati Zain inanunua Celtel, haikununua Celtel Tanzania ltd bali Celtel Africa BV ambayo ilikuwa inamiliki Celtel Tanzania BV ambayo ilimiliki Celtel Tanzania ltd. Hivyo hivyo ilikuwa kwa AirTel ilipoinunua Zain. Kukwepa mitego hii ya Mashirika ya Kimataifa (MNCs) sheria itaje kwamba Kodi hii itozwe kwa Mali zilizopo Tanzania na sio kwa HISA kama alivyopendekeza Waziri wa Fedha. Hata hivyo Kambi ya Upinzani inatambua hatua hiyo ya Serikali kuchukua wazo hili ili kuongeza Mapato ya nchi.
Misamaha ya Kodi
Mheshimiwa Spika, Katika Bajeti ya mwaka 2011/12 Serikali iliahidi kupunguza misamaha ya Kodi mpaka kufikia asilimia 1 ya Pato la Taifa. Ahadi hii haikutekelezwa na Serikali na badala yake imerejea kuahidi tena. Waziri wa Fedha ameliambia Bunge katika hotuba yake, nanukuu ‘kuendelea kufanya mapitio ya sharia mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo’ (uk.39). Badala ya Serikali kutuambia hivi sasa misamaha ya kodi imefikia asilimia ngapi, imeendelea kutoa ahadi isizoweza kutekeleza.
Mheshimiwa Spika, Katika Taarifa ya Utafiti uliofanywa na Jopo la Taasisi za dini hapa nchini waliyoiita ‘The One Billion Dollar Question’ imeonekana kwamba Tanzania inapoteza takribani shilingi trilioni 1.7 kutokana na misamaha ya kodi, ukwepaji wa kodi, utoroshaji wa mitaji nje na udanganyifu katika biashara ya kimataifa. Fedha hizi ni zaidi ya jumla ya Bajeti za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Nishati na Madini. Fedha hizi ni zaidi ya Mkopo ambao Serikali itadhamini kwa TPDC ili kujenga Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam. Fedha hizi zinazopotea kutokana na misamaha ya kodi ni zaidi ya gharama za Ujenzi wa Gati mpya katika Bandari ya Dar es Salaam. Kambi ya Upinzani inawapongeza Viongozi wa Dini kwa kufanya kazi hii nyeti sana lakini tunampongeza zaidi Mtafiti Mtanzania Dokta Prosper Ngowi kwa kushiriki katika utafiti huu. Tunaishauri Serikali kusoma Taarifa hii na kutekeleza mapendekezo yake ili kuongeza mapato ya Serikali. Lugha za kufanya mapitio kila mwaka hazisaidii, wananchi wanataka kuona misamaha ya kodi imepungua mpaka kiwango kinachostahili cha asilimia 1 ya Pato la Taifa.
Kurekebisha mfumo wa Kodi ya Mapato
Mheshimiwa Spika, Bajeti mbadala ya mwaka 2011/12 ilipendekeza kuifanyia marekebisho sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004. Tunarejea pendekezo letu na kuongeza pia kwamba sehemu ya kodi ya Mapato inayotoa fursa (grandfathering) kwa Kampuni za Madini kutumia sheria ya kodi ya Mapato iliyofutwa ya mwaka 1973, ifutwe. Pendekezo letu lina lengo la kutaka kuweka mfumo wa ‘straightline method of depreciation’ ya asilimia 20 badala ya sasa ambapo Kampuni za Madini hufanya ‘100% depreciation’ kwenye Mitambo yao mwaka wa kwanza na hivyo kuchelewesha kulipa ‘Corporate Tax’.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kupandisha kiwango cha chini cha kipato ili kutoza kodi ya Mapato (PAYE) kutoka tshs 135,000 mpaka tshs 170,000 bila kushusha kodi yenyewe. Hii haitamsaidia mwananchi hata kidogo kwani bado kiwango cha kodi cha asilimia 14 kipo juu sana. Vile vile kiwango cha chini cha pato litakalotozwa kodi kitawaathiri wafanyakazi wa Serikali maana ndio ambao Serikali ina mamlaka ya kutangaza kima cha chini cha Mshahara wao na kuwaacha wafanyakazi wa Sekta Binafsi ambao wengi hulipwa kiwango kidogo sana cha mishahara. Kimsingi kutokana na tangazo lake, Waziri wa Fedha ametangaza kima kipya cha chini cha mshahara kuwa kitakua tshs 170,000.
Mheshimiwa Spika, tunarejea kauli yetu kwamba kupanda kwa gharama za maisha kumepunguza uwezo wa matumizi ya wananchi walioajiriwa na kulipwa mishahara ambayo inakatwa kodi (PAYE). Tunapendekeza kwamba PAYE ianzie asilimia 9 kutoka asilimia 14 na kiwango cha chini cha kutoza kiwe tshs 150,000. Tunatambua kuwa kodi hii ni chanzo kikubwa cha Mapato kwa Serikali ambapo kwa mwaka huu wa Fedha kinatarajiwa kuingiza takribani shilingi bilioni 1,437 (asilimia 18 ya Mapato yote ya kodi yanayokusanywa na TRA) kutoka Idara ya Kodi za Ndani (Wafanyakazi wa Serikali tshs 115bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma tshs 47bn na Wafanyakazi wa Sekta binafsi tshs 312bn) na Idara ya Walipa kodi wakubwa (Wafanyakazi wa Serikali tshs 450bn, Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma Tshs108bn na Wafanyakazi wa Sekta Binafsi tshs 406bn). Hata hivyo wananchi wanapobakia na pesa za matumizi kodi nyingine kama VAT na Ushuru wa Bidhaa huongezeka na hivyo kupunguza kiwango cha Mapato ya Serikali ambayo yangepotea kutokana na uamuzi huu.
Mheshimiwa Spika, Hata hivyo bado kuna haja ya kuangalia upya ‘tax brackets’ na kuzirahisisha kwa kuzipunguza na kuongeza kiwango cha kodi ya Mapato kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza mapato kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa kambi ya Upinzani inapendekeza mabadiliko katika viwango vya juu vya kodi ya Mapato ambapo tunapendekeza kupandisha kiwango cha juu kabisa cha kukokotoa kodi ya mapato (PAYE) kiwe shilingi milioni kumi na kodi iwe asilimia 42 kutoka asilimia 30 ya sasa.
Mheshimiwa Spika, Tunapendekeza kwamba mtu yeyote anayepata mapato ya zaidi ya shilingi 10,000,000 alipe kodi ya Mapato ya shilingi 500,000 kujumlisha na asilimia 42 ya tofauti ya shilingi 10,000,000 na shilingi 3,200,000 kama inavyoonekana kwenye jedwali hapa chini. Lengo la mapendekezo haya ni kuwafanya watu wenye kipato kikubwa walipe kodi zaidi kulingana na kipato wanachopata maana hivi sasa masikini wanalipa kodi nyingi zaidi kuliko wenye nacho.
Mapato ya kutozwa kodi kwa mwezi
|
Kodi (PAYE)
|
Mapendekezo ya mapato ya kutozwa kodi kwa mwezi
|
Kiwango kipya cha Kodi (PAYE)
|
Mapato yanayozidi shilingi 720,000
|
Sh. 112,500 ongeza 30% ya kiasi kinachozidi sh. 720,000
|
Mapato yanayozidi 720,000 lakini hayazidi sh. 3,199,199
|
Sh.112,500 ongeza 30% ya ziada ya sh. 720,000
|
Mapato yanayozidi sh. 3,200,000 lakini hayazidi sh.9,999,999
|
Sh.190,000 ongeza 38% ya ziada ya 3,200,000.
| ||
Mapato kuanzia sh. 10,000,000 na kuendelea
|
Sh. 500,000 ongeza 42% ya mapato yake.
|
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo haya hayatapunguza Mapato ya Serikali kwani wigo wa kodi utakuwa umeongezeka kwa kuwagusa wafanyakazi katika sekta binafsi na pia kupata kodi zaidi kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.
Mheshimiwa Spika, vile vile Kambi ya Upinzani inaendelea kupendekeza kuwa mchakato uanze ili kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na zaidi awe anajaza fomu za kodi (tax returns) kila mwaka. Suala hili ni muhimu sana na litangazwe mwaka huu ili tuwe na mwaka mzima wa kujitayarisha ili lianze Mwezi Julai mwaka 2013. Mtanzania yeyote, awe na kipato au asiwe na kipato ajaze Tax Returns. Mfumo huu utatoa takwimu muhimu sana kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania na utasaidia sana hapo baadaye kupanua wigo wa Mapato. Tunapendekeza marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Mapato ili mfumo huu uwepo kisheria ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa.
Mheshimiwa Spika, Vile vile, Kambi ya Upinzani inapendekeza kuanzishwa kwa Real Estate Regulatory Authority kama tulivyofanya kwa mwaka uliopita na kwamba kila mwenye nyumba ya kupangisha lazima atambuliwe na kulipa kodi inavyostahili. Lengo ni kuhakikisha Sekta ya Nyumba inatoa mapato ya kutosha kwa Serikali na kuzuia mianya ya ukwepaji kodi inayofanywa na wenye nyumba.
Presumptive Tax
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza mwaka 2011/12 kwamba ushauri wa Mradi wa kuboresha mfumo wa kodi (Tax Modernisation Project) ambao ulishauri kwamba ipo haja ya kuainisha Kodi ya VAT na Presumptive Tax, utekelezwe. Tunashauri kuwa kodi anayotozwa mfanyabiashara ndogondogo kabla hajaanza kufanya biashara ifutwe kabisa. Uamuzi huu utapunguza mapato ya Serikali (Shilingi bilioni 21.6 kwa mujibu wa Kitabu cha Bajeti Vol. I) katika kipindi cha muda mfupi lakini itakuwa ni chanzo kikubwa sana cha mapato katika kipindi cha muda mrefu.
Vyanzo vipya vya Mapato
Mheshimiwa Spika, Pamoja na kupitia vyanzo vya mwaka jana na kulinganisha na mapendekezo ya Serikali, Kambi ya Upinzani bado inapendekeza vyanzo vya ziada mwaka huu ili kuboresha Mapato ya Serikali.
Kupanua wigo wa Skills Development levy
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunapenda kushukuru kuwa wazo letu la kutoza kodi ya skills development levy tuliyopendekeza katika hotuba yetu ya mwaka uliopita lilifanyiwa kazi na serikali lakini kwa mwaka ujao wa fedha tunaitaka serikali kuipitia upya kodi kwa kuongeza wigo wa wachangiaji ili kuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, tunapendekeza kiwango cha tozo ya kuendeleza stadi (skills development levy – SDL) kishuke kutoka asilimia 6 ya sasa mpaka asilimia 4. Tunapendekeza kuwa Waajiri wote walipe kodi hii ikiwemo Serikali na Mashirika ya Umma. Lengo ni kupunguza mzigo kwa Waajiri na kuondoa ubaguzi kwani wanaofaidika na tozo hii (wanafunzi wa elimu ya Juu) pia huajiriwa na Serikali na Mashirika ya Umma. Serikali ilipanga kukusanya tshs 161bn kutoka katika tozo hii kwa mfumo wa sasa.
Mheshimiwa Spika, Marekebisho ambayo Kambi ya Upinzani inayapendekeza yataongeza mapato ya Serikali mpaka tshs 320bn.
Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha katika tozo hii amesema Serikali ‘itapitia upya maudhui ya viwango vya tozo’ hii. Kambi ya Upinzani imetamka maudhui na viwango na tunaiomba Serikali itekeleze pendekezo hili.
Mheshimiwa Spika, Tunapendekeza mgawanyo wa tozo hii urekebishwe kwa kuongeza mapato yatakayokwenda kwenye Vyuo vya Ufundi mchundo.
Mheshimiwa Spika, kama wanafunzi wetu watasomeshwa na kodi hii basi tuangalie upya mfumo wa Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Fedha inayopatikana kwenye Kodi hii itumike kusomesha kwa ‘grant’ wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi darasani na kuwapunguzia mzigo wa mikopo. Vile vile tuangalie kama tunaweza kukopesha wanafunzi malazi na chakula tu na kutoa bure ada na mafunzo kwa vitendo pamoja na vitabu.
Kulinda kazi za Wasanii
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani mara kwa mara tumekuwa tukieleza jinsi wasanii wanavyoshindwa kunufaika na kazi zao kutokana na kukosekana mfumo rasmi wa kiserikali unaozuia wizi wa kazi za wasanii. Pamoja na serikali kukubali kuahidi kuwa na mfumo rasmi wa kuzuia wizi wa kazi hizo, serikali haijaweka wazi mfumo rasmi utakaokuwa unatumika kuzuia wizi huo na hatimaye wasanii kunufaika na kazi zao.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani katika hotuba ya Wizara ya Habari Vijana na Michezo kwa mwaka uliopita tulingumzia suala hili na tulishauri kwamba kuwe na utaratibu wa kuweka sticker maalumu zinazotolewa na mamlaka za serikali kuonyesha uhalali wa muuzaji wa kazi za wasanii. Serikali imetekeleza pendekezo letu. Hata hivyo tuna maoni tofauti kuhusu namna ya kutekeleza pendekezo hili.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, serikali mwaka 2006 kupitia gazeti la Serikali Na. 18 la tarehe 10 Mwezi wa Februari, ilianzisha utaratibu wa HAKIGRAM kama stiker maalumu za kazi halali za wasanii zinazotolewa na COSOTA. Kambi ya Upinzani tunapendekeza utaratibu huo uendelee na Mamlaka ya Mapato TRA ihusike kukusanya mapato kwa ajili ya kazi hiyo na COSOTA wataratibu utoaji wa HAKIGRAM. Hii itaenda sambasamba na kuzuia uchakachuaji wa HAKIGRAM hizo ili kutopoteza lengo la kuweka mfumo huo. Stiker zisitolewe na TRA bali zitolewe na COSOTA na TRA isimamie eneo la Mapato tu. Hii itasaidia kwani stiker hizi hazitatumika kupata mapato peke yake bali pia kuweka kumbukumbu muhimu za kazi za wasanii.
Mapato kutoka Sekta ndogo ya Mawasiliano ya Simu
Mheshimiwa Spika, serikali imekuja na pendekezo la kuendelea na kutoza ushuru wa bidhaa kwenye masuala ya huduma ya mawasiliano ya simu, jambo ambalo litamgusa mtumiaji wa huduma hiyo ambaye ni mwananchi wa kawaida na hivyo kuongeza gharama za simu. Kambi ya Upinzani inapinga kabisa kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye muda wa Maongezi (airtime) kwenye simu za mkononi.
Mheshimiwa Spika, Hoja ya wananchi hapa ni kwamba Kampuni za Simu za mkononi hazilipi kodi ya kutosha na hasa kodi ya Makampuni (corporate tax). Waziri Mkuu alipokuwa anafunga Bunge la Bajeti mwaka 2011 alitangaza Kampuni ambazo ni walipa kodi wakubwa katika kipindi cha miaka 5 iliyopita. Katika orodha hiyo kulikuwa na Kampuni moja tu ya Simu za Mkononi (Kampuni ya AirTel).
Mheshimiwa Spika, wakati wananchi wanataka kodi zaidi kutoka Kampuni za simu, Serikali inapendekeza kuongeza kodi kwa mwananchi anayetumia simu. Kampuni zilipe kodi ya Mapato na sio kukandamiza wateja kwa ushuru wa bidhaa ilihali huduma zenyewe za simu hazina ubora.
Mheshimiwa Spika, vilevile wananchi wanalalamika kwamba Kampuni za simu za Mkononi hajiweki wazi mapato yake yote hali iliyopelekea Kamati ya Bunge ya POAC kuiagiza TCRA kufunga mtambo utakaoweza kuijulisha TCRA mapato yote ambayo kampuni za Simu zinapata. Serikali ya Ghana ilifanya hivi na kupandisha maradufu mapato yanayotokana na sekta ndogo ya simu. Hivi sasa Ghana, nchi yenye watumiaji wa simu milioni 17 ukilinganisha na Tanzania yenye watumiaji 23 milioni, inakusanya asilimia 10 ya Mapato ya Serikali kutoka kwenye kampuni za Simu peke yake. Iwapo Tanzania ikifikia kiwango cha Ghana cha asilimia 10 ya Mapato ya ndani ya Serikali kutoka kwenye kampuni za simu, Tanzania itaweza kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 860 kutoka kwenye sekta ndogo ya simu peke yake. Hata hivyo mazingira ya Ghana na Tanzania ni tofauti na hivyo tunapendekeza kiwango kutokana na hali yetu.
Mheshimiwa Spika, Shirika la TCRA kupitia zabuni nambari AE-020/2010-11/C/04 imetangaza ‘request for expression of interest for design, development, installation and Management of Telecommunication monitoring system under build, operate and transfer’ ili kupata chombo cha kufuatilia Mapato ya Kampuni za Simu. Kwa mujibu wa ratiba zilizotangazwa na TCRA chombo kitakuwa kimeanza kazi mwishoni mwaka huu wa 2012. Kwa dhati kabisa napenda kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA na watumishi wote kwa kutekeleza maelekezo ya Kamati ya Bunge kwa haraka ili kuhakikisha mapato kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kilichotushangaza ni kwamba Waziri wa Fedha na Uchumi hakugusia kabisa suala hili muhimu sana kwa mapato ya Serikali badala yake Serikali imekimbilia kukandamiza wanyonge watumiaji wa Simu na kuyaacha Makampuni ya Simu yakilipa kiduchu kutoka kwenye mapato yao.
Mheshimiwa Spika, uamuzi huu wa kufuatilia mapato ya Kampuni za Simu na Marekebisho tunayopendekeza ya kujenga uwezo zaidi wa TCRA kwa kuwa na Idara ya ‘Revenue Assurance’ na kurekebisha sheria ya TCRA kwa kuweka wazi makujumu ya TRA ndani ya TCRA, utaiingizia Serikali mapato ya takribani tshs 660bn.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili la Sekta ya Mawasiliano ninaomba kurejea kuitaka Wizara ya Fedha itoe maelezo hapa Bungeni namna ambavyo Hisa za serikali katika Kampuni ya MIC Tanzania ltd inayomiliki Kampuni ya Tigo zilivyouzwa. Mheshimiwa Spika Serikali ilikuwa inamiliki hisa asilimia 26 katika Kampuni hii. Kwa mujibu wa kumbukumbu nilizoziona Hisa hizi zote ziliuzwa kwa thamani ya dola laki saba kwa mwana hisa mwenza mnamo mwezi Februari mwaka 2004. Kampuni hii leo inapata mapato ya Tshs bilioni 20 kwa mwezi, tuliuza hisa zetu asilimia 26 kwa dola laki saba! Laki Saba dola! Kambi ya Upinzani inataka uchunguzi maalumu katika mauzo haya na Taifa liambiwe nini kilitokea na hatua gani za kuchukua dhidi ya waliouza mali hii ya Umma bila zabuni wala kuzingatia thamani ya fedha.
Kuzuia mauzo ya ngozi ghafi nje ya nchi
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imeshangazwa na hatua ya serikali kuja na pendekezo la kuongeza ushuru kwenye bidhaa ya ngozi ghafi inayosafirishwa nje kutoka asilimia 40 hadi 90 lengo likiwa ni kuhamasisha usindikaji wa ngozi hiyo na kuiongezea thamani.
Mheshimiwa Spika, kwa nchi iliyo na mianya mingi ya rushwa kama Tanzania hatua hii haitakuwa na tija kwa kuwa wafanyabiashara wengi wa ngozi ghafi wamekuwa na tabia ya kupunguza takwimu za kusafirisha ngozi ghafi na hivyo kupelekea serikali kukosa mapato mengi sana. Serikali inafahamu kwamba hata ushuru wa mauzo nje wa asilimia 40 haukuweza kutatua tatizo la viwanda vya ndani kukosa malighafi. Kambi ya Upinzani haikubaliani na Pendekezo la Serikali kwani halitatatua tatizo la kukuza sekta ndogo ya Ngozi nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani tunaitaka serikali kuzuia kabisa kusafirisha ngozi ghafi kwenda nje na badala yake kuwe na mpango wa kutumia ngozi ghafi hapa nchini na kuleta tija katika uchumi wa taifa kwa kutengeneza ajira na kuongeza thamani ya mauzo nje.
Mheshimiwa Spika, hatua ya kuzuia ngozi ghafi kusafirishwa kwenda nje kwa Tanzania itakuwa sio suala jipya kwa sababu Ethiopia imezuia na kuwekeza katika kiwanda cha viatu, mikanda na bidhaa za ngozi. Kutokana na Mpango wa Mendeleo ya Ethiopia (GTP – Growth and Transformation Plan) sekta ya Ngozi itaingiza fedha za kigeni za thamani ya dola za Kimarekani bilioni 4 kwa mwaka. Hii ni sawa na fedha za kigeni ambazo Tanzania inapata kutoka kwenye Dhahabu na Utalii kwa pamoja. Ethiopia nchi iliyokuwa inatembea na bakuli na kulia njaa leo inakuwa nchi ya kupigiwa mfano na sisi Watanzania! Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda pia amepiga marufuku kuuza ngozi ghafi nje. Hata nchi ya Pakistani ambayo ndio ngozi zetu zinakwenda nayo imepiga marufuku mauzo ya ngozi ghafi nje. Serikali ipige marufuku Mauzo ya ngozi ghafi nje ya Nchi ili kulinda viwanda vya ngozi nchini, kuoongeza Ajira na kuongeza mapato ya Fedha za kigeni.
Kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa za Maziwa
Mheshimiwa Spika, sekta ndogo ya Maziwa hapa nchini inahitaji kuwekewa maazingira ya kukua ili izalishe ajira na mapato ya kodi kwa Serikali. Wakati Tanzania ndio nchi ya Afrika Mashariki inayoongoza kwa kuwa na Ng’ombe wengi lakini inaongoza kwa kuagiza maziwa kutoka nje yenye thamani ya dola za kimarekani 3.6m. Wakati Kenya imelinda soko la Maziwa na Bidhaa za Maziwa kwa kuondoa (zero rating) kodi ya VAT kwenye bidhaa za Maziwa, Waziri wa Fedha hajaonyesha kabisa juhudi zozote za kujengea uwezo sekta ndogo ya Maziwa hapa nchini na hivyo kuweza kuondolewa kabisa katika ushindani na kujikuta wafugaji wanakosa kabisa soko la kuuza maziwa yao hapa nchini. Nchi za Rwanda na Uganda pia zimelinda Maziwa na Bidhaa za maziwa kwa njia hii. Ni muhimu Serikali kuwianisha kodi hii na Nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kufanya marekebisho kwenye sharia ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kufanya ‘zero rating’ kwenye Maziwa na Bidhaa za Maziwa zinazozalishwa hapa nchini kwa kipindi cha miaka 5 ili kufikisha uzalishaji wa angalau lita 500,000 za maziwa kwa siku kutoka lita 123,000 za sasa na kuweza kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya elfu tatu.
Mheshimiwa Spika, hatua zote za kuongeza mapato tulizopendekeza pamoja na hatua za Bajeti Mbadala iliyopita ambazo tunarudia kuzipendekeza zitaongeza Mapato ya Serikali kwa takribani shilingi bilioni 2,885 kama inavyoonyeshwa katika jedwali hapa chini.
NYONGEZA YA VYANZO VYA MAPATO MBADALA 2012/2013
Chanzo cha Mapato
|
Makisio - Bilioni
|
Marekebisho ya kodi za misitu ikiwemo Mkaa
|
130.8
|
Kupunguza misamaha ya kodi, kuzuia ukwepaji kodi na udanganyifu wa Biashara ya Nje
|
742.74
|
Mauzo ya hisa za serikali
|
415.55
|
Marekebisho ya kodi Sekta ya madini (kodi ya Mapato, Kodi ya CGT na ushuru mbalimbali) (25% ya Mauzo ya Madini Nje)
|
578.36
|
Marekebisho ya Kodi na Usimamizi bora wa Mapato Kampuni za Simu
|
502.26
|
Marekebisho ya Kodi ya SDL
|
243.52
|
Mapato ya wanyamapori
|
61.64
|
Kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta- kampuni za madini
|
44.9
|
Usimamizi wa mapato ya utalii
|
51.75
|
Kuimarisha biashara katika EAC kwa kuongeza mauzo
|
114.15
|
JUMLA
|
2,885.67
|
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hapo juu, vyanzo hivi vya mapato ni mjumuisho wa vyanzo ambavyo katika hotuba zetu mbadala za nyuma tumekuwa tukipendekeza, ambapo tumevifanyia marekebisho kulingana na hali halisi ya uchumi ulivyo kwa sasa, pamoja na kupendekeza baadhi ya marekebisho ya sheria za kodi ili kuongeza mapato zaidi kwa Serikali.
No comments:
Post a Comment