Mwanza, Tanzania
Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa miongoni mwa taasisi zilizoshiriki kikamilifu katika Tamasha la Utamaduni la Bulabo 2026 lililofanyika kuanzia tarehe 7 hadi 14 Juni 2026 katika Viwanja vya Ngomeni, Kisesa, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Tamasha hilo lililobeba kaulimbiu ya “Maridhiano kwa Njia ya Amani Ndiyo Jadi Yetu, Linda Maadili ya Mtanzania” lilikusanya pamoja viongozi wa Serikali, viongozi wa kimila, taasisi mbalimbali na wananchi kutoka maeneo tofauti ya nchi kwa lengo la kuenzi urithi wa utamaduni wa Tanzania, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kukuza maadili yanayochangia maendeleo ya Taifa.
Miongoni mwa washiriki wa tamasha hili alikuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na maafisa wa Tume ya Taifa ya UNESCO, walioshiriki katika shughuli mbalimbali zilizofanyika katika kipindi chote cha tamasha. Ushiriki huo ulitoa fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kushuhudia namna utamaduni unavyoendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha umoja, amani na utambulisho wa Taifa.
Kilele cha tamasha hilo kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Said Mtanda, aliyemwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Mtanda aliwapongeza machifu wa jadi kwa juhudi zao za kuendelea kuhifadhi na kurithisha mila, desturi na maadili mema ambayo yameendelea kuwa msingi wa mshikamano na amani nchini.
Alieleza kuwa utamaduni wa Kitanzania una mchango mkubwa katika kujenga jamii inayoheshimiana, inayosikilizana na inayoweza kutatua changamoto zake kwa njia ya mazungumzo. Alisisitiza kuwa maadili na tamaduni zetu ni hazina muhimu inayopaswa kulindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Tamasha la Bulabo limeendelea kujidhihirisha kuwa jukwaa muhimu la kuenzi na kutangaza urithi wa utamaduni wa Tanzania. Kupitia maonesho ya mila na desturi, ngoma za asili, sanaa za jadi na mijadala mbalimbali kuhusu nafasi ya utamaduni katika maendeleo ya jamii, washiriki walipata fursa ya kutambua mchango wa urithi wa kitamaduni katika kujenga Taifa lenye umoja na mshikamano.
Ushiriki wa Tume ya Taifa ya UNESCO katika Tamasha la Bulabo 2026 unaendana na dhamira ya UNESCO ya kulinda na kuendeleza urithi wa utamaduni duniani, pamoja na kutambua nafasi ya utamaduni katika kujenga amani na maendeleo endelevu. Kwa kutekeleza majukumu yake nchini, Tume ya Taifa ya UNESCO inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhifadhi na kuhamasisha matumizi ya urithi wa utamaduni kama nyenzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Tamasha hilo pia limetoa ujumbe muhimu kuhusu umuhimu wa maridhiano, uvumilivu na kuheshimu tofauti zilizopo katika jamii. Kaulimbiu ya mwaka huu imewakumbusha Watanzania kuwa amani na umoja ni tunu za Taifa zinazopaswa kuendelezwa na kulindwa wakati wote.
Kadiri dunia inavyobadilika, umuhimu wa kuhifadhi utamaduni na maadili ya jamii unaendelea kuwa mkubwa zaidi. Matukio kama Tamasha la Bulabo yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuimarisha utambulisho wa Taifa, kukuza mshikamano wa wananchi na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika maendeleo endelevu.
Tume ya Taifa ya UNESCO itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhifadhi, kuendeleza na kutangaza urithi wa utamaduni wa Tanzania kama nguzo muhimu ya amani, umoja na maendeleo ya Taifa.


No comments:
Post a Comment