ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 16, 2026

SIMULIZI YA KISHERIA: KESI YA REGINALD MENGI VS YUSUF MANJI (2011) MAPAMBANO YA VIGOGO WAWILI.

 


​​Imeandaliwa na Karim Gabriel Mussa

Mwanasheria & Mchambuzi wa Sheria (KGM Attorneys) 0755 395 572.


​Leo tunatupa jicho kwenye moja ya mivutano ya kisheria iliyovuta hisia za kipekee nchini Tanzania mapema miaka ya 2010. Hili lilikuwa ni pambano la kisheria kati ya miamba miwili ya biashara: Aliyekuwa Mwenyekiti wa IPP Media, Marehemu Dr. Reginald Mengi (pamoja na Independent Television - ITV Tanzania), dhidi ya mfanyabiashara na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu ya Young Africans Sports Club, Marehemu Yusuf Manji.


​Kesi hii haikutikisa tu kwa sababu ya majina ya wahusika, bali iliacha funzo kubwa la kiutaratibu wa kisheria (Procedural Law) katika shauri la madai ya kuchafuliwa jina (Civil Defamation) na matumizi ya rungu la Marejeo (Civil Revision) chini ya Kifungu cha 79 cha Sheria ya Mwenendo wa Madai (CPC, 2002).


↘️ SAKATA LILIVYOANZA: Tuhuma za "Mafisadi Papa" na Dai la Fidia ya Shilingi Moja!


​Sakata hili lilianza mnamo mwaka 2009 baada ya Dr. Reginald Mengi kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwataja baadhi ya wafanyabiashara akizungumzia kile alichokiita "Mafisadi Papa" wanaohujumu uchumi wa nchi. Katika orodha hiyo, jina la Yusuf Manji lilitajwa.


​Yusuf Manji akahisi jina na hadhi yake kama mfanyabiashara mkubwa wa ndani na kimataifa vimechafuliwa vibaya, alifungua kesi ya madai ya kashfa (Civil Case No. 85 of 2009) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu dhidi ya Dr. Mengi na ITV.


​Lakini Manji alitega mtego wa kipekee na wa kisaikolojia wa kisheria: Katika madai yake ya fidia, tofauti na kesi nyingine ambapo watu huomba mabilioni kwa mabilioni, Manji aliomba kulipwa Fidia ya Jumla (General Damages) ya Shilingi Moja tu ya Kitanzania (TZS 1/=)!


​Hoja ya Manji ilikuwa rahisi: "Jina na heshima yangu havina thamani ya kifedha inayoweza kununulika. Sihitaji fedha za Mengi; ninachohitaji ni Mahakama ya Tanzania isafishe jina langu na kutamka kuwa nimesingiziwa."


↘️ MTIFUANO MAHAKAMANI: Mapambano ya Nyaraka na Pingamizi la Awali


​Kesi ilianza kusikilizwa mwaka 2011 mbele ya Hakimu Mkazi Katemana pale Yusuf Manji (PW1) alipoanza kutoa ushahidi wake. Katika kujihami, mawakili wa akina Dr. Mengi waliwasilisha mahakamani orodha ya nyaraka (List of Documents) zilizolenga kutumika kumng'oa Manji kwenye ushahidi wake.


​Hapo ndipo dhoruba ya kiutaratibu ilipolipuka. Mawakili wa Manji waliweka pingamizi wakidai kuwa uwasilishaji wa nyaraka hizo ulifanyika nje ya utaratibu na kanuni za mwenendo wa madai. 


Baada ya malumbano ya siku mbili, Hakimu Katemana alikubaliana na upande wa Manji na akazitupa nje nyaraka zote za akina Mengi, lakini akawapa nafasi ndogo ya kwenda kuomba kibali rasmi cha kuziwasilisha upya.


​Dr. Mengi na ITV, wakaona kuwa kutupwa nje kwa nyaraka zao kungezuwia utetezi wao kusikika kikamilifu, walisikitika na kukimbilia Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia maombi ya marejeo (Civil Revision No. 38 of 2011) chini ya Mheshimiwa Jaji Dr. Fauz Twaib.


↘️ ​MBELE YA MAHAKAMA KUU: Pambano Linalohamia Kwenye "Ufundi wa Sheria"


​Mbele ya Jaji Dr. Fauz Twaib, pambano halikuwa tena kuhusu "Nani fisadi au nani amesingiziwa", bali lilihama kabisa na kuwa pambano la ufundi wa sheria (Technicalities of Procedure). Mawakili wa Yusuf Manji waliweka mapingamizi makali ya awali (Preliminary Objections) wakitaka maombi ya Dr. Mengi yatupiliwe mbali bila hata kusikilizwa.


Maombi hayo yaliwasilishwa Mahakama Kuu yakitaka kufutwa kwa mwenendo mzima wa kesi iliyokuwa ikiendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi na kuamriwa ianze upya (de novo). 


Waombaji Dr. Mengi na mwenzake walidai kuwa kulikuwa na mazingira maalumu yaliyohitaji Mahakama Kuu kutumia mamlaka yake ya marejeo ili kurekebisha makosa yaliyokuwa yametokea katika mwenendo wa shauri hilo.


Miongoni mwa malalamiko yao kulikuwa na namna masuala ya kesi yalivyopangwa (framing of issues), kuondolewa kwa baadhi ya nyaraka zao katika kumbukumbu za mahakama, kujiondoa kwa hakimu aliyekuwa akisikiliza shauri bila kutoa sababu, pamoja na amri iliyozuia vyombo vya habari kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.


Hata hivyo, kabla ya kuingia katika kiini cha hoja hizo, Mahakama ilikabiliwa na pingamizi la awali kutoka kwa mawakili wa Yusuf Manji. 

Pingamizi hilo lilihusu mambo mawili makubwa: 

1️⃣ kwanza, kwamba baadhi ya maamuzi yaliyolalamikiwa yalikuwa yamepitwa na muda wa kuombewa marejeo; na 

2️⃣ Pili, kwamba maamuzi hayo hayakuwa ya aina inayoweza kurejelewa kwa njia ya revision.


Mahakama ilikubaliana na hoja kwamba baadhi ya maamuzi yaliyokuwa yanalalamikiwa yalikuwa yamepitwa na muda kwa mujibu wa Sheria ya Ukomo wa Madai. Ilisisitiza kuwa pale ambapo upande binafsi ndiye anayeliomba Mahakama itumie mamlaka yake ya marejeo, maombi hayo lazima yawasilishwe ndani ya muda unaotakiwa na sheria. 


Lakini somo kubwa zaidi lilitokana na hoja ya pili. Mahakama ilieleza kuwa si kila uamuzi wa kati unaotolewa wakati kesi inaendelea unaweza kuwa msingi wa marejeo. Kimsingi, sheria imeweka kanuni kwamba maamuzi ya awali au ya muda (interlocutory decisions) hayawezi kukatiwa rufaa wala kuombewa marejeo isipokuwa kama yana athari ya kuamua kwa mwisho haki za wahusika katika shauri husika. 


Mahakama ilikumbusha kuwa mamlaka ya marejeo ni mamlaka ya kipekee yanayotumiwa kwa tahadhari kubwa. Ili Mahakama iingilie kati, lazima kuwe na kosa la msingi linaloweza kusababisha dhuluma au kuathiri haki za mhusika kwa kiwango kikubwa. Si kila kutokuridhishwa na uamuzi wa hakimu kunatosha kuhalalisha matumizi ya mamlaka hayo. 


Katika kuchambua malalamiko yaliyowasilishwa, Mahakama iliona kuwa baadhi ya maamuzi yaliyolalamikiwa yalikuwa ndani ya mamlaka ya mahakama ya chini na hayakuonyesha uwepo wa dhuluma au kosa kubwa kiasi cha kuhitaji kuingiliwa na Mahakama Kuu. Kwa mfano, kuhusu suala la kuanza kesi upya baada ya hakimu mwingine kuchukua usikilizaji wa shauri, Mahakama ilieleza kuwa uamuzi huo ni wa hiari ya hakimu anayesikiliza shauri kwa mujibu wa sheria, hivyo haukuwa msingi wa marejeo. 


Baada ya kusikiliza maombi hayo Mahakama kuu, maombi hayo ya marejeo ya Dr. Mengi yalitupiliwa mbali.


Uamuzi huu unafundisha jambo muhimu sana katika mfumo wa haki. Mahakama za juu hazipo kwa ajili ya kurekebisha kila hatua au kila uamuzi mdogo unaotolewa wakati wa usikilizaji wa kesi. Badala yake, huingilia pale tu ambapo kuna kosa la msingi la kisheria, ukiukwaji mkubwa wa haki, au mazingira maalumu yanayoonyesha kuwa kuendelea kwa mwenendo wa shauri kunaweza kusababisha dhuluma. 


Kwa hiyo, kabla ya kukimbilia kuomba revision dhidi ya uamuzi wa kati uliotolewa na mahakama ya chini, ni muhimu kujiuliza swali moja muhimu: 


Je, uamuzi huo umeamua mwisho haki zangu au umesababisha dhuluma kubwa inayohitaji Mahakama ya Juu iingilie kati? Kama jibu ni hapana, basi mara nyingi sheria itahitaji usubiri shauri likamilike ndipo hatua nyingine za kisheria zichukuliwe.


Uamuzi katika kesi ya Reginald Abraham Mengi & IPP Limited v. Yusuf Manji (Miscellaneous Civil Cause No. 45 of 2011, High Court of Tanzania, Dar es Salaam Registry, 20 December 2011) umeendelea kuwa rejea muhimu katika kuelewa mipaka ya mamlaka ya marejeo na umuhimu wa kutofautisha kati ya uamuzi wa kawaida wa mwenendo wa kesi na kosa la kisheria linalostahili kuingiliwa na Mahakama ya Juu. Na ​​Sakata hili la Mengi na Manji linabaki kuwa shule tosha kwa wanafunzi na watendaji wa sheria nchini;


1️⃣ ​Fidia Si Utajiri, Ni Heshima: 

Manji alionyesha mfano wa kipekee kuwa kwenye kesi ya kashfa, lengo kuu la mdai linapaswa kuwa kusafisha jina (vindication of reputation) na sio fursa ya kujipatia ukwasi wa haraka; ndio maana dai la "Shilingi Moja" lilikuwa na uzito wa kimaadili kuliko madai ya mabilioni.


2️⃣ ​Utaratibu Usiue Haki (Substantive Justice): Mahakama Kuu ilikumbusha kuwa ufundi wa kisheria na mapingamizi (technicalities) yasitumike kama mtego wa kuwaziba mdomo wadau wasiweze kupata haki yao ya kusikilizwa.


​Je, unaoni gani kuhusu mkakati wa Yusuf Manji kudai fidia ya Shilingi Moja tu ili kulinda heshima yake?  Tukutane kwenye maoni!


​⚠️ DISCLAIMER: Makala hii ni kwa ajili ya kutoa elimu ya kisheria, kihistoria na kijamii pekee kulingana na kumbukumbu rasmi za uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania (2011).

#kgmupdates #sheria #tanzania #LegalEducation

No comments: