ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 12, 2012

MAPENZI NI BAHATI, KAMA ULIPO SI BAHATI YAKO, ENDELEA KUTAFUTA-4

MAPENZI yamekuwa magumu. Ni mzigo mzito kuubeba. Yanaendelea kujeruhi wengi, bado ni mateso kwa wengine. Sasa hivi, asilimia kubwa ya watu, inaamini kwamba kupata mwenzi sahihi wa maisha ni ndoto za alinacha. Ni kamari, ni bahati nasibu.
Maendeleo yamekuja na mambo leo. Kile kinachoonekana ni uzungu, kimeathiri kwa kiasi kikubwa ustaarabu wetu. Mila na desturi zetu, vimepokwa na utandawazi uliotujia. Hii inamaanisha kwamba uhusiano wa kimapenzi wa sasa, hauendani na sura ya utamaduni wetu.

Vijijini kuna unafuu japo na kwenyewe fujo zimeshaingia na mambo yameshabadilika. Mijini ndiyo matatizo yenyewe. Ulimwengu wa digitali na fursa za mitandao zinatutia wazimu. Tunataka kuiga mitindo ya maisha ya wenzetu, matokeo yake tunageuka watumwa wa mapenzi.
Hayakuletwa mapenzi ili yawaumize watu, yapo kwa ajili ya kutoa faraja ndani ya jamii. Yalivyo ni kwamba baada ya misukosuko ya kimaisha, vurugu mechi za kusaka riziki na mihangaiko mingine ya kimaisha, angalau unaweza kusahau yote unaporejea kwa mwenzi wako.
Hata hivyo, mapenzi hugeuka matatizo pale ambapo kazini umeondoka pakiwa moto, unarudi nyumbani nako pia unakuta moto. Unakosa sehemu ya kwenda kujishikiza. Faraja inaota mbawa. Hapa ndipo tafsiri ya mapenzi inapokosa mashiko. Jitazame, muangalie na mwenzako!
Japo ni ukweli usiopingika kuwa mapenzi siku zote hayapo tambarare hata kwa wenza waliostaarabika, ila katika kundi la mabrazameni na masistaduu ni mtihani. Kuna usemi kwamba glasi hugongana kabatini, nakubaliana nao lakini kwa makundi hayo ni pasua kichwa.
Hapa nisisitize kuwa ukiona wewe na mwenzi wako mnatofautiana, suluhu inakuwa ngumu kupatikana. Siku zinapita hamzungumzii tatizo lililowafanya mkawa kwenye sura ya mfarakano. Kila mmoja anajifanya yupo ‘bize’ na mambo yake. Hapo maana yake kuna mambo makuu matatu na moja lazima ndilo litakuwa sahihi.
Mosi; inawezekana umemkosea kitu kikubwa sana mwenzi wako. Alikuamini mno na hakutaraji kwamba utamfanyia hicho ulichotenda. Kutokana na moyo wake kuingiwa ganzi, inakuwa vigumu kwake kuketi mezani kutafuta suluhu, kwani anakosa imani aliyokuwa nayo awali.
Hapa nikupe angalizo kwamba ni bora uwe huaminiki au imani ya watu kwako iwe ya wastani. Endapo watu watakuwa na imani kubwa kwako, siku wakigundua una nyendo chafu za siri, heshima yako hupotea kabisa. Kama huaminiki, watu watasema ni kawaida yako. Waliokuamini kwa wastani, nao watanena hukuwa ukiaminika asilimia 100, hivyo halitakuwa gumzo.
Unapokuwa unaaminika kwa asilimia 100, maana yake hakuna shaka yoyote kwa watu juu yako. Hivyo basi, unapoboronga, heshima yako itashuka kwa kasi. Mitaani simulizi utakuwa wewe, kwani ni jambo geni na halikuwahi kutabiriwa kwako. Tafadhali, ishi maisha yako, usiishi maisha bandia. Utaumbuka.
Vivyo hivyo kwenye mapenzi. Mpenzi wako anayekupenda na kukuamini kupita kiasi, siku ukimtenda ndivyo sivyo, atakaa na maswali mengi kwa muda mrefu. Utageuka kinyaa mbele yake, kwa hiyo hata kukusamehe atapenda kufanya hivyo lakini atachelewa kwa sababu heshima yako kwake, imeondoka kabisa.
Pili; mapenzi yenu ni kama mnalazimisha. Hampendani kabisa au yeye hakutaki, kwa hiyo anaona hiyo ni fursa ya kukuadhibu. Utashangaa umemkosea jambo dogo lakini anavyolisimamia utadhani umeua mtu. Kama sura ya aina hiyo, inajiri kwenye uhusiano wake, jaribu kutazama mbele kwa matumaini. Hakupendi, atakupotezea muda.
Tatu; mapenzi yake kwako ni ya wastani. Ulivyo kwake, ukiwa naye ni sawa na hata usipokuwa naye. Huyu atakwambia anakupenda muda mwingine kwa sababu anachukulia ni kauli ya mazoea. Ila ukiyatafsiri mapenzi katika kipengele cha mguso wa moyo. Hakupendi, ila amekuzoea.
Kwa mtu wa aina hiyo, mlipaswa kuwa marafiki lakini mkajidanganya mkawa wapenzi. Hizo ni gharama za kulazimisha uhusiano. Elewa kwamba wapo watu ambao ukawa na urafiki nao wa kawaida, halafu yupo mmoja ambaye ndiye mwenye nafasi yake. Anza kufanya upembuzi leo.
Mapenzi si kumuona mtu barabarani akakuvutia basi ukajiaminisha kuwa huyo anakufaa. Mwenzi wa maisha yako ni lazima akidhi vigezo vingi.
Wapo ambao utalazimika kuwaacha barabarani wakirandaranda na dunia, halafu yupo mmoja mahsusi anayekufaa kwa hali zote kuwa mwandani wako.
Mada hii ikupe tafsiri kwamba siku za mwanzoni za uhusiano wako, inafaa utulize kichwa, ujadili mwenendo wa mwenzi wako kama anakufaa au la! Uzuri wa umbo na sura yake, visikufanye uwe kipofu ukasahau kilicho na faida kwa maisha yako ya leo na kesho. Tazama faida zaidi.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info.

No comments: