ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 19, 2012

MAPENZI NI BAHATI, KAMA ULIPO SI BAHATI YAKO, ENDELEA KUTAFUTA-5

NIKIMALIZIA sehemu ya mwisho ya makala haya, nianze kusisitiza kuwa unapoangalia tafsiri ya mwenzi wa maisha yako katika kipengele cha bahati, ni vizuri ukaweka kando hisia za kuridhishwa kitandani. Ufundi wake wa kukufanya usahau matatizo yako yote pindi mnapokutana faragha, si lolote endapo hatakuwa na sifa za kutimiza matarajio yako ya kimaisha.
Mwenzi wa maisha yako haendani na harufu yake. Kwamba ukiwa naye unajisikia mtulivu kiasi gani, la hasha! Kinachobeba uzito ni kiasi gani huyo uliyenaye anavyokupunguzia mzigo wa maisha yako. Je, mtindo wa maisha yake, haukupi mzigo wa moyo? Kama jibu ni ndiyo, basi iwe heri.

Wengine hutafsiri kwamba mwenzi wa maisha yako utamtambua kwa namna ambavyo anakufanya ujisikie hamu ya tendo mara kwa mara hata baada ya kutoka naye faragha muda mfupi uliopita. Mtazamo huu nao ni potofu, badala yake jiulize tena, je, mwenzi wako anakufanya ujihisi mtulivu?
Je, anakufanya ujione ni mwenye furaha? Nazungumzia furaha ambayo inakuja yenyewe, siyo ile ya kulazimisha. Mwenzi sahihi kwako kwa zaidi ya asilimia 99, anapaswa kuongeza kitu chanya kwenye maisha yako. Endapo ukijitazama unajikuta unazidi kupotea badala ya kusafiri kwenye mstari ulionyooka, hapo unazidi kupotea.
Yatazame maisha yako kabla hujakutana naye, halafu jiulize mabadiliko yako. Je, ni hasi au chanya? Inawezekana kweli ameyafanya maisha yako kuwa na furaha lakini hiyo furaha anaidumisha vipi? Isije ikawa anakufurahisha pale tu anapokuwa na shida zake, pindi unapomtatulia huyo anakwenda zake, akirudi tena ujue ana shida.
Mathalan, mwenzi wako anatimiza kila kitu unachohitaji. Anageuka mtu wa ndiyo na kutekeleza kila ombi lako. Wewe unajiona unatisha kwa kuona kwamba mwenzi wako anakunyenyekea unavyotaka. Kumbe mwenzako ana malengo yake, mkishaingia faragha na kukidhi haja zake, ule unyenyekevu wake wote unaondoka, anarudi kuwa yuleyule.
Mwenzi wako ana asili ya kiburi, mara nyingi ombi lako la kukutana naye faragha hulitolea nje kwa maelezo kwamba eti huwa hajisikii. Lakini anapokuwa na shida ya pesa, anakuwa mpole, kiburi chake chote kinapotea. Hakawii kukwambia ana hamu na wewe. Akili ikae kichwani kwako.
Mfano: Msomaji wangu ambaye naomba nimtaje kwa jina moja la Bryson, aliwahi kunilalamikia kwa njia ya simu, kuhusu tabia ya mke wake. Akadai kuwa wakati mwingine hafikirii kama aliyemuoa ni mke wake, ila changudoa anayetaka kuvuna kwake. Akaenda mbali zaidi kwa kusema anahisi mkewe ana kidumu nje ya ndoa yake.
Akaeleza kwamba yeye na mkewe tofauti yao kubwa huwa ni usiku wakati wa kulala. Kila anapomhitaji mkewe hukutana na vizingiti visivyokwisha. Visingizio ni vingi, mara ooh, leo nilifanya kazi nyingi, nimechoka sana, siku nyingine ooh, leo nimezunguka sana, hapa mapaja yote yamechubuka.
Kwa mujibu wa Bryson, visingizio vya mkewe huwa haviishi. Pale ambapo husisitiza, hutokea ugomvi mkubwa kiasi kwamba hata majirani hutambua kwamba kuna kimbembe chumbani kwao. Hii ndiyo inamfanya Brayson ahisi kwamba mkewe ana kidumu pembeni ambacho hutimiza haja zake.
Bryson akaendelea kueleza kuwa inapotokea mkewe ana shida ya fedha, siku hiyo ataanza kumtumia SMS za mapenzi siku nzima. Atamsisitiza awahi kurudi nyumbani kwamba ana hamu naye, wakati mwingine hudanganya analia kwa madai eti, ‘amemmisi’ kupitiliza.
Anaweza kuandika SMS yenye sura hii: “Mume wangu leo uje na shilingi 100,000, kuna nguo nataka ninunue, ukija nayo usiku nitakupa.” Wakati Bryson anatafakari jinsi ya kujibu, mkewe wanatuma SMS nyingine: “Yaani tuache utani, ukweli nimekumisi. Leo jiandae kabisa, lazima tukeshe.”
Bryson akichelewa kujibu, mkewe ataandika SMS nyingine: “Nakupenda sana mume wangu. Usichelewe kurudi, leo nina mzuka wa ajabu na wewe, si unajua ni wewe ndiye unayenipatia?” Punde tena, SMS nyingine: “Mbona unijibu, najisikia vibaya mpaka nalia peke yangu, hiyo tabia gani ya kunichunia?”
Msomaji wangu huyo akaeleza kwamba kimbembe hujiri pale anapofika nyumbani. Hukuta kila kitu kimebadilika. Mandhari huwa ni nzuri, mkewe huwa mchangafu kupita siku zote. Hata huduma za nyumbani, huwa zipo juu kupita maelezo. Akifika atafunguliwa vifungo vya shati na kuvuliwa shati kwa unyenyekevu.
Atafunguliwa kamba za viatu na kuvuliwa viatu kwa madaha. Atapelekwa mezani kula, baadaye bafuni kuoga, huko ataogeshwa naye atabaki amesimama tu kama mlingoti. Atatolewa huko na kupandishwa kitandani, wakati wa kulala atafanyiwa ‘masaji’ na kubembelezwa kwa sauti tamu, iliyonakshiwa na tundu za pua.
Ikifika wakati wa tendo, katikati ‘romansi’, mke huulizia ile shilingi 100,000 aliyoomba. Bryson akijibu ipo, mke hutaka aoneshwe kabisa, akishawekewa mezani, basi hujituma kweli. Bryson hupewa ladha na mitindo ambayo hajawahi kupata. Endapo atasema fedha hana, mchezo huishia hapo, tena wakati mwingine mke huwa mkali kweli.
“Kipindi kingine mke wangu hulazimisha usiku huohuo twende kwenye ATM nikamtolee hiyo fedha. Nikisema benki sina akiba, mipango yote ya mapenzi inaishia hapo. Atanisimanga, mwisho tunalala mzungu wa nne. Nikifikiria hapa ndiyo maana huwa nasema mke wangu ni kama changudoa, hafanyi nami tendo la ndoa mpaka fedha,” Bryson.
Inawezekana picha iliyopo kwako siyo sawa na ile ya Bryson lakini hebu fikiria upande wako, kama mwenzi wako anakuwa nawe kwa masharti, hebu jichenge. Upendo unaotakiwa hapa ni ule usiozingatia hali wala masharti. Ukipuuza hili, kaa ukijua kuwa ukiyumba katika kile ambacho anakupendea lazima atakuacha.
Anakupenda? Penzi lenu halina migogoro? Anakidhi matarajio yako? Je, maisha yamekuwa rahisi baada ya kuwa naye? Hakupi maumivu ya moyo? Mna mtazamo wa aina moja? Kama jibu la maswali haya ni “ndiyo”, basi huyo ni wa bahati yako, kama jawabu lipo kinyume, endelea kutafuta. Itazame bahati yako mbele kwa matumaini.

www.globalpublishers.info

No comments: