ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 12, 2012

Mawakili wataka washitakiwa wa mauaji ya Fundikira waachiwe huru




Mawakili wa upande wa utetezi Godfrey Ukwong’a na Mluge Karolin katika kesi ya mauaji ya Swetu Fundikira inayowakabiliwa askari watatu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ),  wameiomba mahakama kuwaachia huru washtakiwa hao kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka  kushindwa kuthibitisha kama walifanya mauaji hayo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni, Rhoda Robart (42), Ally Ngumbe (37) na Rashid (30), wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Ombi hilo lilitolewa na mawakili hao  mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wakitoa hoja za majumuisho ya mwisho, mbele ya Jaji Zainabu Muruke, baada ya mashahidi sita wa upande wa mashtaka kutoa ushaidi wao na mahakama hiyo kuona washtakiwa wana kesi ya kujibu.


Upande wa utetezi uliita mashahidi watatu ambao ni washtakiwa wenyewe waliopanda kizimbani kujitetea dhidi ya mashtaka dhidi yao.

Wakili Karoli kwa niaba ya mshtakiwa wa kwanza, Rhoda, alidai kuwa shtaka la mauaji ni kubwa kuliko yote na kwamba ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri hakuna unaomgusa mshtakiwa kwa namna moja au nyingine.

“Mtukufu jaji ushahidi uliotolewa mahakamani hapa hakuna shahidi aliyemtaja mteja wangu kama alimuona akimuua Fundikila hivyo naomba mahakama yako imuachie huru” alisema..

Naye wakili Ukwong’a kwa niaba ya washtakiwa wa pili na wa tatu ambao ni ndugu wa kuzaliwa kwa baba na mama mmoja, alidai kuwa ushahidi wote uliotolewa mahakamani hapo hakuna ulioithibitishia mahakama bila kuacha shaka kama washtakiwa walifanya mauaji hayo.

Hata hivyo, akijibu hoja za majumuisho hayo, Wakili wa Serikali Charles Ishengoma alidai kwamba ushahidi uliotolewa na mashahidi sita unatosha kuiongoza mahakama kuwatia washtakiwa hatiani kwa mauaji hayo.

Alidai kuwa washtakiwa walionekana na mshtakiwa akiwa mzima wa afya na baadaye alikutwa mahututi akiwa mikononi mwao mpaka kufikia hali ya umauti uliotokana na majeraha yaliyopelekea kifo.

Kesi hiyo inaendelea leo ambapo wazee wa baraza katika kesi hiyo watatoa majumuisho yao ya mwisho dhidi ya kesi hiyo.



 
CHANZO: NIPASHE

No comments: