ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 12, 2012

Maximo kutua Yanga leo

Kocha Marcio Maximo
Kocha wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbrazil Marcio Maximo anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuifundisha Yanga ambayo hivi karibuni itakuwa na kibarua cha kutetea ubingwa wake wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame).

Habari zilizopatikana kutoka Yanga zinasema kuwa Maximo atatua nchini leo Jumanne saa 8 mchana na tiketi yake alitumiwa Ijumaa baada ya kufikia makubaliano na uongozi wa klabu hiyo.


Chanzo chetu kinaendelea kusema kuwa msimu ujao Yanga imejipanga kufanya vizuri na hatimaye kumaliza machungu yaliyowakuta msimu uliopita ambao waliumaliza kwa kupoteza ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Bara na kukumbana na kichapo cha aibu cha magoli 5-0 kutoka kwa watani zao Simba.

"Tumejipanga na tunaendelea kujipanga, tunawaambia kuwa Yanga ya msimu ujao itakuwa tishio," kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilitamba kuwa (yeye) kila anachoamua kukifanya ndani ya Yanga huwa kinafanikiwa na kwa kawaida yeye huweka wazi mipango yake baada ya kukamilika na si vinginevyo.

Aliongeza kuwa tayari wameshaandaa malazi na usafiri kwa Maximo na msaidizi wake ili watakapofika waanze mazoezi ifikapo Alhamisi kama walivyopanga.

Maximo aliwasili nchini mwezi Julai mwaka 2006 na kuanza kuifundisha Taifa Stars mpaka mwaka mwaka 2010 ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Jan Poulsen kutoka Denmark.

Poulsen naye mkataba wake wa miaka miwili ulitarajiwa kumalizika mwezi ujao lakini tayari TFF imesitisha ajira yake na sasa timu iko chini ya aliyekuwa kocha wa U-20 (Ngorongoro Heroes), Kim Poulsen, ambaye naye ni raia wa Denmark.

Hata hivyo, Yanga mwakani haitashiriki mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kutokana na kumaliza Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa ya tatu huku Simba ikitwaa ubingwa huo na Azam ikimaliza ya pili.

No comments: