ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 19, 2012

Mbunge amlipua mfanyabiashara kwa jasusi


Mbunge wa Wawi (CUF),Hamad Rashid Mohamed
Neville Meena, Dodoma
MBUNGE wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed jana aliilipua Kampuni ya Madini ya Minerals Extractions Technologies Ltd kutokana na mmiliki wake kufanya biashara za madini kwa njia za utapeli na ujasusi.

Minerals Extractions Technologies Ltd ni kampuni ambayo inafanya kazi ya kusafisha mchanga wa dhahabu katika baadhi ya migodi iliyopo Kanda ya ziwa na iliwahi kulalamikiwa kwa kukataa kushirikiana na mpango wa kufuatilia mapato yanayolipwa kwa Serikali na kampuni za madini, gesi na mafuta (TEIT) unaoongozwa na Jaji Msitaafu, Mark Bomani.

Kutokana na hali hiyo, Mohamed alitoa mapendekezo ya kuundwa kwa kamati ya wabunge sita kutoka Kamati tatu za Bunge ili kuchunguza kampuni hiyo na mmiliki wake ambaye (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye alisema kuwa anatamba kwamba Tanzania hakuna mtu anayeweza kumgusa.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Serikali ya 2012/2013, Mohamed alisema mwekezaji huyo anamiliki hati tano za kusafiria, tatu kutoka nchini kwake Belgium na mbili za Burundi na kwamba bado anaishi nchini licha ya kufukuzwa nchini na Serikali.

Mbunge huyo alisema katika hali ya kushangaza, taarifa za mwekezaji huyo ziliripotiwa polisi ili akamatwe katika hoteli ya Holiday Inn ya jijini Dar es Salaam, lakini kwa kuthibitisha kwamba amekuwa akiishi nchini kijasusi, taarifa hizo zilimfikia kabla ya kutekelezwa kwa mpango huo, hivyo aliwakwepa polisi kwa kukodi vyumba viwili katika hoteli hiyo na baadaye kuwatoroka.
 
“Huyu mtu aliwahi kumtukana Kamishna wa Nishati na Madini ambaye ni mbunge mwenzetu (Dk Dalaly Kafumu). Tumeshirikiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani (Pereira Ame Silima) na polisi walikwenda kumkamata lakini…ndo maana nasema ni jasusi, alikuwa amekodi vyumba viwili katika hoteli ya Holiday Inn kwa hiyo hakukamatwa,” alisema mbunge huyo.

Alisema mwekezaji huyo amekuwa akiliibia taifa mamilioni ya fedha kutokana na kufanya udanganyifu katika kiasi cha dhahabu ambacho amekuwa akikisafirisha kwenda nje ya nchi kila wiki na kwamba baadhi ya vyombo vya dola vinafahamu suala hilo lakini vimeshindwa kuchukua hatua.
 
“Huyu bwana amekuwa akisafirisha kila wiki kilo 15 za dhahabu kwenda nje ya nchi, lakini anafanya udanganyifu mkubwa hivyo kuliibia taifa mamilioni ya pesa, lazima Bunge hili lichukue hatua kwa kulifanyia kazi suala hili,” alisema Mohamed.
 
Alipendekeza timu ya wabunge itakayoundwa ijumuishe wajumbe wawili kutoka kamati za Bunge za Mambo ya Nje na Ulinzi na Usalama, Nishati na Madini na Kamati ya Fedha na Uchumi.
 
Mbunge huyo aliahidi kuwasilisha kwa Spika nyaraka kadhaa kuhusu kampuni hiyo na madudu inayofanya nchini, huku mmiliki wake akitamba kwamba anawamiliki Watanzania wote.
 
Habari ambazo gazeti hili lilizipata zimeeleza kuwa mbunge huyo alikuwa amewasilisha nyaraka mbalimbali katika ofisi ya Spika ambazo zilikuwa zikionyesha taarifa mbalimbali za mwekezaji huyo.
 
Miongoni mwa taarifa hizo ambazo Mwananchi imeziona ni namba za hati za kusafiria za raia huyo wa Ubelgiji ambazo ni EG 125092, EH 096587 na EI 590081 za Ubelgiji wakati hati zake za kusafiria kutoka nchini Burundi ni EE 132212 na EF 558746.
 
Nyaraka hizo pia zinaonyesha kuwa mwekezaji huyo anaishi nchini kwa hati ya daraja la kwanza (Class A) ambayo aliipata Novemba 2011 lakini ukweli ni kwamba yupo nchini tangu 2005, japokuwa hakuna taarifa zozote kwamba tangu wakati huo alikuwa akiishi nchini kama nani na kwa shughuli ipi.
 
Baadaye Mohamed aliliambia Mwananchi kuwa kuna udanganyifu mkubwa katika taarifa za uhamiaji kuhusu mwekezaji huyo na kwamba ujeuri alionao hata kwa viongozi wa Serikali, unatia shaka kwamba huenda analindwa na mfumo ambao unahitaji nguvu za Bunge kuuvunja.


Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Wabunge kama hawa ndio tunaowataka na tuwape ulinzi wa kutosha na pia sisi wananchi tumlinde kwa namna nyingine asije kumalizwa taratibu.Huyo mwekezaji kama anavunja sheria basi mkataba wake ufutwe na yeye aondolewe nchini haraka sana