ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 19, 2012

Wizi fedha za safari za JK kuchunguzwa

Nora Damian
SERIKALI imeanza uchunguzi wenye lengo la kubaini kama maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa walifuata taratibu kutoa  Hazina Sh3.5 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya safari za Rais Jakaya Kikwete ndani na nje ya nchi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatifa, Bernard Membe alisema jana kuwa fedha zinazochunguzwa ni zile zilitolewa kati ya Machi Mosi na Machi 8, mwaka huu kwa ajili ya safari za Rais Kikwete kwenda Geneva, Brazil, Adis Ababa na Arusha.

Wiki iliyopita gazeti moja la kila wiki liliripoti kuwa maofisa watano wa wizara hiyo wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kuiba fedha zilizotengwa kwa ajili ya safari za rais kutoka benki moja nchini.

Fedha zilizotolewa kutoka Hazina ni Sh 3.5 bilioni wakati zilizokuwa zimepangwa kwa safari hizo ni Sh2 bilioni.Fedha hizo zinadaiwa kutolewa Hazina na maofisa waliokuwa wakikaimu nafasi mbalimbali, katika wizara hiyo.

Waziri Membe alisema wakati tukio hilo likitokea, yeye, naibu wake, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Mhasibu Mkuu walikuwa safarini na kwamba nafasi zao zilikuwa zinakaimiwa.“Waliokuwa wanakaimu wali-process (andaa) fedha za safari pamoja na hazina, na fedha zikapatikana tarehe 8,” alisema Membe na kuongeza kuwa;

“Ofisa Masuhuri hakushirikishwa na uchunguzi wa kamati unaendelea ili kujiridhisha kama taratibu zote za kiutawala zilifuatwa,” alisema.

Alifafanua kwamba tayari walifanya uchunguzi uliohusisha Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Usalama wa Taifa na wakaguzi wawili kutoka wizarani hapo.“Hakuna tuliyemshuku ama kumuita mwizi kwa sababu hakuna hata fedha iliyoibwa, zote ziliingia kwenye akaunti ya wizara na nyingine zililetwa wizarani,” alisema.

Waziri huyo alisema uchunguzi wa kamati unaoendelea, sasa unalenga kuangalia kama taratibu zilifuatwa na wale waliokuwa wanakaimu.“Uchunguzi wa kamati utakapokamilika na kubainika makosa yalikuwa wapi utawekwa hadharani,” aliahidi.
Utabiri wake Chadema

Akizungumzia taarifa za kuitabiria Chadema ushindi mwaka 2015, Membe aliwatuhumu watu aliowaita maadui wake kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema wameshiriki kumlisha maneno ya kukitabaria ushindi chama hicho kikuu cha upinzani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

"Kuna taarifa za mimi kutabiria ushindi Chadema 2015. Naomba niseme kitu kimoja, kama kuna mtu anajua mimi niliwahi kufanya utabiri ajitokeze. Mimi siyo TB Joshua wa Nigeria, mtoto wa marehemu Shehe Yahaya au (jina la kampuni moja ya kimataifa)...ambao wao kila mara ndiyo hufanya utabiri," alisema Membe huku akionekana kuchukizwa na taarifa hizo.

Membe alifafanua kwamba, ni kweli alikutana na ujumbe wa Chadema nyumbani kwake jimbo la Mtama, mkoani Lindi na kufanya nao mazungumzo, lakini hakuwahi kutabiri kwamba chama hicho kikuu cha upinzani kingeweza kushinda mwaka 2015.

"Nikweli nilifanya mazungumzo na Chadema walipokuja jimboni kwangu Mtama. Tena walikuja bahati nzuri walikuta chakula cha mchana tayari, nikawakaribisha vizuri. Wapinzani si maadui, yaani watu walitaka niwafukuze chakula. Najua kuna watu hawakufurahia kuwaalika Chadema kuja kwangu," alisema Membe na kuongeza;

"Ni kweli niliongea nao. Niliongea nao mambo matatu, kwanza niliwapongeza kwa kujipenyeza hadi vijijini. Niliwaambia, ni vema mmetambua umuhimu wa kufika hadi vijijini maana mwaka 2010 mlilalamika kuibiwa kura wakati vijijini mlikuwa hamjafika. Lakini pia, nikawambia ni vema wametambua umuhimu wa kuanza kufanya siasa kwa kujenga hoja na tatu, nikawambia nyie fikeni vijijini sisi kina Membe hatujaanza kutimua vumbi."

Alifafanua kwamba, anaamini watu wa Chadema waliokuwapo katika mkutano huo ambao ni pamoja na Dk Slaa na Lema hawawezi kuzusha taarifa hizo zilizotolewa na kuongeza, "Nimesoma vizuri Political Science, adui wa kisiasa katika chama siku zote yumo ndani ya chama hicho. Kwa hiyo hata hili naamini limetoka kwa baadhi ya maadui ndani ya CCM na kwa Chadema ni maadui wa Chadema."  

Kuhusu APRM

Katika hatua nyingine, Membe alisema taarifa ya Tanzania kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Kujitathmini wa Umoja wa Afrika (APRM), itajadiliwa mwakani nchini Addis Ababa.

Licha ya waziri huyo kukiri kwamba Tanzania inadaiwa dola za Marekani 800,000 za ada, alisema hiyo si sababu ya taarifa ya Tanzania kutojadiliwa mwaka huu kama ilivyotarajiwa.

Rais Kikwete alitarajiwa kuwasilisha ripoti ya Tanzania kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU), utakaofanyika Lilongwe, Malawi Julai 10 mwaka huu, lakini haitafanyika hivyo.
Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti kuwa Rais Kikwete amezuiwa kuwasilisha taarifa ya Tanzania kutokana na deni hilo.

“Walitakiwa wajadili taarifa ile halafu walete maswali tujibu ndipo wataandaa taarifa ikajadiliwe,” alisema Membe na kuongeza;

“Watu wa APRM hawajaja, hivyo itajadiliwa katika mkutano wa Addis Ababa mwaka 2013,” alisema.
Tanzania inadaiwa dola za Marekani 800,000  deni ambalo ni malimbikizo ya ada ya dola 100,000 kila mwaka, kwa miaka minane mfululilizo tangu mwaka 2005.

“Mara kwa mara tumekuwa tukiwakumbusha Hazina kuhusu deni hili na si kwamba ndilo limezuia,” alisema. 

Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

haya haya tena mafisadi oyee oyeee, ndo mambo hayoo eti pesa hazikuibiwa hamuachi nyinyi kuwadanganya WADANGANYIKA KILA LEO KAMA WATOTO MAYATIMA.

UFISADI OYEE KWENDA MBELE UKIPATA TUMIA ZA MALI YA UMMA NA UKIKOSA SHUKURU