ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 19, 2012

Mwigulu achafua Bunge




  Kauli yake yazua zogo
  Zitto ataka iondolewe
Hali ya hewa ndani ya Bunge jana jioni ilikuwa ni kama msemo wa wahenga wa ‘hala hala mti na jicho’, baada ya Mbunge wa Iramba Mashariki (CCM), Mwigulu Mchemba, kutumia lugha ya kuudhi bungeni akichambua bajeti mbadala iliyowasilishwa na kambi ya upinzani, hali iliyoibua kelele za wabunge wakitaka muongozo wa Mwenyekiti wa kikao cha jana jioni.

Mwigulu ambaye pia ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wa Uchumi, alianza mchango wake kwa kusema kuwa Bunge limejaa waigizaji na kuwataka Watanzania kuwa macho na watu hao, hasa akirejea mbunge aliyekuwa amechangia mjadala wa bajeti ya mwaka 2012/13 bila kumtaja jina.


Ingawa Mwigulu hakumtaja kwa jina, aliyekuwa ameichambua bajeti ya serikali kwa kauli kali alikuwa ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ambaye alisema kuwa ni aibu kuwa serikali ya sasa ya CCM, wabunge wa CCM na amekosa imani na serikali hiyo na kuwataka wananchi kufanya maamuzi ya kuwaondoa madarakani kama wanataka umasikini uondoke.

Lissu akichanganya Kiingereza na Kiswahili alisema ni aibu kuwa serikali inayosema uongo, wabunge wake wanaosema uongo na kwamba ni aibua ya taifa hili ni ya CCM na wabunge wake kwa kushindwa kuleta mabadiliko yoyote ya kuondoa umasikini nchini.

Kauli ya Mwigulu ilimfanya Mwenyekiti wa kikao hicho amtake kufuta baadhi ya kauli zake ikiwemo ya ‘kuwapo waigizaji bungeni’ na ‘watu wenye mapepo’.

Mwendelezo wa makombora pia uliendelea wakati Mbunge wa Mbinga Magharibi (CCM), John Komba, ambaye alitaka kuwe na utaratibu wa kuwapima kwanza wabunge kama wana uendawazimu hospitali ya vichaa ya Mirembe kabla ya kuingia bungeni kwani wengi wameonyesha kuwa na wendawazimu.
Komba pia alionya kuwa kama matusi hayataachwa ndani ya Bunge kuna siku ngumi zitalipuka na watakaoumia ni kambi ya upinzani kwani CCM ina wabunge wengi na ngumi zao zitakuwa nyingi. Alionya wabunge wa kambi ya upinzani kuwa watakufa.

Awali akiwasilisha bajeti mbadala, Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, aliitaka serikali kuiondoa bungeni bajeti hiyo ili ikatayarishwe upya kwa nia ya kuifanya ikidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo kama ulivyoidhinishwa na Bunge na kusainiwa na Rais wa nchi.

Zitto alisema uamuzi huo umechukuliwa na kambi yake kwa kuwa bajeti iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa, Alhamisi iliyopita, haikukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo kama ambavyo ulipitishwa na Bunge.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 63 (13) (C) madaraka ya Bunge ni pamoja na kujadili na kuidhinisha mpango wo wote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo,” alisema.

Alisema Bunge liliidhinisha mpango kwa mujibu wa ibara tajwa ya katiba, lakini serikali imeshindwa kuonyesha utekelezaji wake.

Alitaja maeneo ambayo kambi ya upinzani imeona kuwa  hayakutekelezwa katika bajeti iliyopita kuwa kupunguza makali ya maisha kama ambavyo serikali ilitangaza nia yake ya kupunguza.

Alisema licha ya hatua mbalimbali kuchukuliwa na serikali ili kukabiliana na hali hiyo, mfumuko wa bei uliongezeka maradufu kutoka wastani wa asilimia 6.3 mwaka 2010/11 mpaka wastani wa asilimia 17.8 mwaka 2011/12.

“Serikali inapendekeza hatua zile zile ilizofanya mwaka wa fedha unaokwisha kwa kutoa vibali kwa wafanyabiashara vya kuagiza mchele na sukari,” alisema.

Kuhusu sera ya mapato, alisema kambi yake imependekeza kutunga kwa sheria kwa kuimarisha zaidi sheria za Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 kwamba mikopo ya kampuni kwenye uwekezaji, kwa sababu za kikodi, isizidi asilimia 70 ya mtaji wote uliowekezwa na hii ianze mara moja bila kujali mikataba iliyopo.

Kuhusu kodi ya kuendeleza stadi, Zitto, alisema wamependekeza kiwango kishuke kutoka asilimia sita ya sasa mpaka asilimia nne na kwamba waajiri wote walipe kodi hiyo ikiwemo serikali na mashirika ya umma.

Kambi ya Upinzani Bungeni pia imepinga kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi kwenye simu za mkononi kwa maelezo kuwa makampuni ya simu za mkononi hayalipi kodi ya kutosha na hasa kodi ya kampuni.

Zitto alisema pendekezo la kuendelea na kutoza ushuru wa bidhaa kwenye masuala ya huduma ya mawasiliano ya simu litamgusa mtumiaji wa huduma hiyo ambaye ni mwananchi wa kawaida na hivyo kuongeza gharama za simu, huku kampuni husika zikitoa kodi  kiduchu.

“Wakati wananchi wanataka kodi zaidi kutoka kampuni za simu, serikali inapendekeza kuongeza kodi kwa mwananchi anayetumia simu...kampuni zilipe kodi ya mapato na siyo kukandamiza wateja kwa ushuru wa bidhaa ilihali huduma zenyewe za simu hazina ubora,” alisema.

Pamoja na kulipa kodi kiduchu, alisema wananchi pia wanalalamika kwamba kampuni hizo haziweki wazi mapato yake yote hali iliyopelekea Kamati ya Bunge ya POAC kuiagiza TCRA kufunga mtambo utakaoweza kuijulisha TCRA mapato yote ambayo kampuni za simu zinapata.

Alisema kwa mfano, Serikali ya Ghana ilifanya hivyo na kupandisha mara dufu mapato yanayotokana na sekta ndogo ya simu na hivi sasa nchi hiyo yenye watumiaji wa simu milioni 17 ikilinganishwa na Tanzania yenye watumiaji 23 milioni, inakusanya asilimia 10 ya mapato ya serikali kutoka kwenye kampuni za simu peke yake.

Alisema iwapo Tanzania ikifikia kiwango cha Ghana cha asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Serikali kutoka kwenye kampuni za simu, itakusanya zaidi ya Sh. bilioni 860 kutoka kwenye sekta ndogo ya simu peke yake.

Alisema uamuzi wa kufuatilia mapato ya kampuni za simu na marekebisho wanayopendekeza utaiingizia Serikali mapato ya takribani Sh. bilioni 660.

Mapendekezo mengine waliyopinga ni hatua ya serikali kupandisha kiwango cha chini cha kipato ili kutoza Kodi ya Mapato (PAYE) kutoka Sh. 135,000 mpaka Sh. 170,000 bila kushusha kodi yenyewe.

Alisema hatua hii haitamsaidia mwananchi hata kidogo kwani bado kiwango cha kodi  cha asilimia 14 kipo juu sana na kwamba kiwango cha chini cha pato litakalotozwa kodi kitawaathiri wafanyakazi wa Serikali maana ndio ambao Serikali ina mamlaka ya kutangaza kima cha chini cha mshahara wao na kuwaacha wafanyakazi wa sekta binafsi ambao wengi hulipwa kiwango kidogo sana cha mishahara.

Alisema kupanda kwa gharama za maisha kumepunguza uwezo wa matumizi ya wananchi walioajiriwa na kulipwa mishahara ambayo inakatwa kodi (PAYE).

“Tunapendekeza PAYE ianzie asilimia tisa kutoka asilimia 14 na kiwango cha chini cha kutoza kiwe Sh. 150,000…tunatambua kuwa kodi hii ni chanzo kikubwa cha mapato kwa Serikali ambapo kwa mwaka huu wa Fedha kinatarajiwa kuingiza takribani Sh. bilioni 1,437,” alisema.

Alifafanua kuwa, asilimia 18 ya mapato yote ya kodi yanayokusanywa na TRA kutoka Idara ya Kodi za Ndani (Wafanyakazi wa Serikali Sh. bilioni 115, wafanyakazi wa mashirika ya umma Sh. bilioni  47 na wafanyakazi wa sekta binafsi Sh. bilioni  312.

Alisema Idara ya walipa kodi wakubwa (wafanyakazi wa Serikali Sh. bilioni 450, wafanyakazi wa mashirika ya umma Sh. bilioni 108 na wafanyakazi wa sekta binafsi Sh. bilioni 406.

 Hata hivyo, alisema wananchi wanapobakia na pesa za matumizi kodi nyingine kama VAT na ushuru wa bidhaa huongezeka na hivyo kupunguza kiwango cha mapato ya Serikali ambayo yangepotea kutokana na uamuzi huu.

Alitaka Serikali kuangalia upya madaraja ya kodi (tax brackets) na kuzirahisisha kwa kuzipunguza na kuongeza kiwango cha kodi ya mapato kwa watu wenye kipato kikubwa zaidi.

Kuhusu kuongeza mapato kutoka kwa watu wenye kipato kikubwa, Zitto, alisema wanapendekeza mabadiliko katika viwango vya juu vya kodi ya mapato kwa kupandisha kiwango cha juu kabisa cha kukokotoa kodi ya mapato (PAYE) kiwe Sh. milioni 10 na kodi iwe asilimia 42 kutoka asilimia 30 ya sasa.

Kambi hiyo pia imependekeza kwamba mtu yeyote anayepata mapato ya zaidi ya Sh. milioni 10 alipe kodi ya mapato ya Sh.  500,000 kujumlisha na asilimia 42 ya tofauti ya Sh. milioni 10 na Sh. 3,200,000.

Alisema lengo la mapendekezo hayo ni kuwafanya watu wenye kipato kikubwa walipe kodi zaidi kulingana na kipato wanachopata maana hivi sasa masikini wanalipa kodi nyingi zaidi kuliko wenye nacho.

Kambi hiyo imependekeza mchakato kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na zaidi awe anajaza fomu za kodi kila mwaka na tangazo litangazwe mwaka huu, ili kuwa na mwaka mzima wa kujitayarisha ili zoezi hilo lianza Julai 2013.

Kwa upande wa ajira, alisema jukumu la serikali ni kujenga mazingira ya wananchi kupata ajira ama kwa kujiajiri au kwa kuajiriwa na shughuli za uchumi, lakini ukweli ni kwamba serikali imeshindwa kushughulikia tatizo la ajira na hasa ajira kwa vijana.
Alisema tatizo la ajira kwa vijana ni bomu litakalokuja kulipuka vibaya sana kama serikali haitakuwa makini nalo kwa kuwa hii ni nchi ya vijana.

Akizungumzia mfumuko wa bei, Zitto, alisema, Kambi ya Upinzani inaamini kuwa, hakuna mbadala wa kudhibiti mfumuko wa bei zaidi ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwekeza kwa wananchi.

WABUNGE WAICHAMBUA BAJETI

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Pauline Gekul, aliifananisha bajeti hiyo sawa na pulizo na kusema itakuwa ni aibu kwa Watanzania kuipitisha akisema kwamba, fedha zilizopendekezwa na serikali kwa ajili ya bajeti hiyo ni za kula.

“Ni aibu kupitisha hii bajeti. Haifai hata kidogo kupitishwa,” alisema na kuongeza: “inawezekana imeandaliwa kwa zimamoto.”

MACHALI: CHANGA LA MACHO

 Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali,  aliishangaa serikali kwa kuja na bajeti ya Sh. trilioni 15 na kuliomba Bunge liipitishe, wakati bajeti ya mwaka ya jana ilikuwa ni ‘changa la macho.’

Kauli hiyo ilimfanya Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba, kumtaka Machali kufuta kauli hiyo.

Hata hivyo, Machali alishikilia kauli hiyo baada ya kuitolea ufafanuzi kwa kusema kwamba, alichokuwa amemaanisha ni kwamba, kilichofanywa na serikali katika kuleta bajeti hiyo ni “kudanganyana”.

Aliwataka wabunge kuikataa bajeti hiyo na kuonya kuwa iwapo wataipitisha watakuwa wanajitafutia laana kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kusisitiza kuwa chama chake cha NCCR kamwe hakiwezi kuiunga mkono wakati imesheheni mambo ya siku zote.

Alisema kwa upande wake hawezi kuunga mkono bajeti kwa kuwa amepoteza imani na baadhi ya viongozi wa serikali ya CCM na kutolea mfano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, kwamba, ni mmoja wa viongozi ambao wanakera.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Amina Makilagi, aliishauri serikali kuongeza kwa kasi ukusanyaji kodi kwa sababu baadhi ya Watanzania wanakwepa kodi.

CHEYO: HAKUNA UWAZI

Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, alisema tatizo la bajeti ni kukosekana uwazi.

Alisema Waziri Fedha, Dk. William Mgimwa, hajaeleza madeni yaliyomo kwenye maendeleo kuwa ni kiasi gani ili wabunge watakapoipitisha waone kama wanakwenda mbele.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Leticia Nyerere, alionyesha masikitiko yake kwa kuona kila mwaka pato la taifa linashuka, huku serikali ikitoa visingizio mbalimbali, ikiwamo kupanda kwa uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme na ukame.

“Mimi kwangu siona kama ni bajeti. Kuwa kwenye kamati ya fedha na uchumi, haimaanishi kuwa ninaunga mkono, inagandamiza taifa. Ni bajeti gandamizi na ni hatari sana kwa taifa,” alisema.

KIGOLA: MISAMAHA NI MINGI

Mendrad Kigola (Mufindi Kusini-CCM), alisema maeneo nyeti kama madini yamekuwa yakisamehewa kodi na kwamba uamuzi wa serikali wa kuongeza mshahara wa wafanyakazi haujawasaidia kwa kuwa kodi imeongezwa.

Alisema watu wengi wanatumia simu, ukiongeza kodi maana yake unataka kudidimiza maisha ya watu, kwani Afrika Mashariki watu wengi wanatumia simu, hivyo kodi yake isiongeze.

BULAYA: HAKUNA JIPYA

Mbunge wa Viti Maalum, Ester Bulaya (CCM), aliipongeza serikali kuondoa ushuru kwa bodaboda.

“Kwenye bajeti sijaona jipya kwa sababu, mwaka jana wakati tunachangia bajeti, wabunge tulizungumzia fedha nyingi kwenda kwenye matumizi ya kawaida, kutegemea fedha za wafadhili katika mwaka huu hayo mambo yapo,” alisema.

“Trilioni 10 zimwekwa kwenye matumizi ya kawaida. Mwaka jana zilikuwa Shilingi  trilioni 8. tulitarajia ingeanza kufanyiwa kazi kwenye bajeti hii. Mmepunguza kama mlivyoahidi au mmeongeza?”alihoji.

Awali Lissu alisema hiki ni kipindi kingine cha muda wa mambo ya kipuuzi.

“Kila mwaka tunakutana katika Bunge hili kuzungumza na kupitisha mambo ambayo hayatekelezeki. Serikali inakuja na bajeti inakuja na ahadi yenyewe inajua haitekelezeki,” alisema. Na kuongeza: “Wabunge wanaunga kile wanajua hakitekelezeki.”

Mwaka jana, tuliambiwa na serikali tukaletewa mpango wa maendeleo wa miaka mitano. Huku ikijua wataetenga sh trlioni 8.6 kwa mapato ya ndani ajili ya bajeti ya maendeleo.

CHENGE AMRUKA MPINA

Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, imeridhia bajeti iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, kuwa imezingatia na kukubali ushauri  wa kamati wa kuboresha bajeti ya serikali.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Andrew Chenge, alitoa msimamo huo jana  wakati akiwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi  ya mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2012/13 pamoja na tathmini ya  utekelezaji wa bajeti ya 2011/12 na  mapendekezo ya bajeti ya 2012/13.

Akisoma ripoti  hiyo alisema iliridhia bajeti hiyo kuwa ndiyo iliyokubaliwa na kamati kwa kusema: “ Kamati inaipongeza Wizara kwa kuwa sikivu na kukubaliana na ushauri uliotolewa na kamati ya Fedha na Uchumi katika kuboresha bajeti hii, taarifa hii ni ushauri wa ziada  katika maeneo kadhaa ambayo serikali itayazingatia.”

 Ripoti ya Mwenyekiti wa Kamati imepinga madai ya Mbunge wa Kisesa (CCM) ambaye pia mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi, Luhaga Mpina , aliyedai kuwa bajeti hiyo haikuwa ile iliyokubaliwa na wajumbe wa kamati hiyo, hata hivyo Chenge hakuzungumzia suala hilo.

Mpina alipoulizwa na NIPASHE kama aliomba mwongozo na kama bado ana msimamo wa kuipinga bajeti hiyo, alisema kuwa hakuomba mwongozo kwa kuwa hakuwepo mjini Dodoma. Alisema jana alikuwa safarini kurejea Dodoma kutoka jimboni kwake katika msiba wa bibi yake na kuahidi kutoa msimamo wake wakati wa kuchangia.

Hata hivyo, kamati hiyo iliionya serikali kuacha mchezo wa kuibua  matumizi mapya yasiyokuwa ya dharura na yasiyoidhinishwa na Bunge wakati ikitekeleza bajeti, ili kudhibiti  matumizi makubwa ya serikali.

Kamati ilisema mtindo huo unavuruga bajeti na kupunguza uwezo wa kutoa fedha za matumizi mengineyo  na na ya maendeleo kama ilivyokusudiwa.

Akichambua bajeti ya Sh. trilioni 15 ya 2012/13 ambayo imetenga Sh. trilioni 10.5 kuendesha serikali na  Sh trilioni 4.5 fedha za maendeleo na kuonya kuwa inaashiria kuwa uchumi wa Tanzania utabakia kuwa wa utumiaji mkubwa ikilinganishwa na uzalishaji.

“Hii ni hatari kubwa kwa maendeleo ya taifa,” alisema Chenge. Pia amati iliitaka serikali kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo ndani ya  mwaka huu wa fedha kwani imekuwa ni wimbo wa muda mrefu usiotekelezeka.

Aidha kamati iliitaka serikali itoe ufafanuzi wa fedha zilizotengwa  kwa ajili ya Benki ya Rasilimali na ya Kilimo  kwa mwaka huu wa fedha  wa 2012/13  kama ilivyoelezwa na Waziri  wa Fedha wakati wa kuwasilisha bajeti.

Akizungumzia mfumuko wa bei,  alisema umedumu kwa muda mrefu  na sasa umekuwa mfumuko sugu wa bei.

“Sera za kifedha  na zile za kodi zimeshindwa kutatua tatizo hili na kuufanya mfumuko uwe sugu. Kamati inaishauri serikali  uchukue changamoto hii na kuifanyia kazi ipasavyo, ikiwemo kusimamia  ugavi  wa chakula na kuimarisha  mipango ya hifadhi  ya chukala na kuhakikisha  kupatikanaji  wa umeme wa kutosha,” alisema Chenge.

Kadhalika, Kamati ya Fedha iliitaka serikali kufuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT)  kwenye sembe, sukari, maharage ili kudhibiti mfumuko wa bei unaochangiwa na bei za vyakula ambao umefikia zaidi ya asilimia 18.
CHANZO: NIPASHE

No comments: