Mbunge wa
Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel, akiwa chini ya ulinzi wakati
alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es
Salaam leo kwa ajili ya kusikiliza kesi inayomkabili. Mbunge huyo
alikamatwa jana kwa kile kilichodaiwa kudai na kutaka kupokea Rushwa
baada ya kukamilika kwa mitego ya Wana TAKUKURU katika Hoteli ya Peacock
iliyopo maeneo ya Mnazi Mmoja jana.
Mbunge wa Bahi (CCM), Omary
Ahmed Badwel, akiwa chini ya ulinzi wa Polisi wakati akitoka Mahakamani
huku baada ya kusomewa mashitaka mawili ya rushwa ya sh. milioni 1,
aliyokuwa akiitaka kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mkuranga, Jonathan Liana.
Wakili wa Mbunge wa Bahi, Omary Ahmed Badwel, Mpare
Mpoki (kushoto) akitoka Mahakamani.
Na Mwandishi Wetu, Jijini
MBUNGE wa Jimbo la Bahi (CCM),
Omary Ahmed Badwel (43) leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu Dar es Salaam, na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), kwa kosa la rushwa ya shilingi Milioni moja toka kwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan Liana.
Wakili
wa Takukuru, Janeth Machullia na Ben Lincoln, walidai mbele ya Hakimu
Mkazi Faisal Kahamba, kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili
ya rushwa.
Wakili Machullia, alidai kuwa kosa la kwanza
ni la rushwa kinyume na kifungu cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007, kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2
mwaka huu katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam , Badwel, akiwa ni
Mbunge wa Bahi na Mjumbe Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na
wakati huo akiwa ni ofisa wa serikali kwa maana ya sheria ya Takukuru,
alitenda kosa la kushawishi ili apewe rushwa ya jumla ya Shilingi
milioni nane kutoka kwa, Sipora Liana, ili kiasi hicho cha fedha aweze
kuwapelekea wajumbe wenzake wa Kamati hiyo ya Bunge ili waweze
kuipitisha ripoti ya fedha ya mwaka 2011/2012 ya Halmashauri hiyo.
Wakili Machullia, alidai shitaka
la pili ni kwamba kati ya Juni 2 mwaka huu, katika Hoteli ya Peacock,
mshitakiwa akiwa na nyadhifa zake zote hizo alipokea rushwa ya Milioni
moja kutoka kwa Liana ili aweze kwenda kuwashawishi wajumbe wa Kamati
hiyo ili waweze kuipitisha ripoti ya fedha ya Halmashauri ya Mkuranga
huku akijua kufanya hivyo ni kosa.
Hata
hivyo mshitakiwa huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea Mpare Mpoki,
alikanusha mashitaka yote na wakili wa Machullia, alidai kuwa upelelezi
wa shauri hilo umekamilika.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Kahamba, alisema ili
mshitakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika
ambao kila mmoja atasaini bondi ya shilingi milioni nne na kusalimisha
hati zao za kusafiria mahakamani, sharti ambalo lilitimizwa na
mshitakiwa huyo na akapata dhamana.
Hakimu
Kahamba, ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 18 mwaka huu, kesi hiyo
itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuja kumsomea
maelezo ya awali mshitakiwa huyo.
No comments:
Post a Comment