ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, June 27, 2012
Mwakyembe akagua mabasi
Hamida Shariff, Morogoro
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harison Mwakyembe amefanya ziara ya kushtukiza katika Kituo cha Mabasi cha Msamvu Manispaa ya Morogoro na kufanya ukaguzi wa mabasi ya abiria ambapo mabasi matatu aliyaamrisha yalipe faini ya Sh250,000 kila moja kutokana na makosa mbalimbali likiwamo la kutokuwa na dereva wa akiba.
Ziara hiyo aliifanya mapema wiki hii asubuhi kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ambapo lengo la waziri huyolilikuwa kukagua mabasi yanayofanya safari za mikoani na nje ya nchi na kuona kama yanakidhi vigezo vya Sumatra katika shughuli ya kusafirisha abiria.
Katika ziara hiyo, Dk Mwakyembe alifika katika kituo hicho cha mabasi na kuegesha gari mbali kidogo kisha kuelekea kwenye mabasi huku akijifanya abiria na kuingia ndani ya mabasi hayo kisha kuanza kukagua leseni za madereva na vitambulisho vya kampuni za mabasi wanavyotumia madereva.
Ukaguzi mwingine alioufanya ni ratiba za safari pamoja na usalama wa mabasi na baadaye Dk Mwakyembe aliamrisha madereva walioonekana kuwa na makosa kulipa faini Sumatra.
Mabasi yaliyolipishwa faini ni pamoja na Royal Coach linalofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kuelekea Bukoba ambalo dereva wake hakuwa na kitambulisho cha kampuni, basi la Super Najimunisa na Muro Investiment yanayofanya safari zake Dar es Salaam kuelekea Mwanza ambapo mabasi hayo yalikuwa na kosa la kutokuwa na dereva wa akiba.
Baada ya kubaini makosa hayo Waziri Mwakyembe aliwataka madereva ambao walionekana kuwa na makosa kulipa faini ya papo hapo kwa Sumatra, vinginevyo aliwataka Sumatra kuwafikisha mahakamani hata hivyo madereva hao walikubali kulipa faini hiyo waliwasiliana na wamiliki wa mabasi wanayofanyia kazi.
Akizungumza na maofisa wa Sumatra pamoja na madereva, Dk Mwakyemba alisema makosa kama hayo yanaweza kusababisha ajali za barabara na hivyo kupoteza maisha ya watu, kusababisha ulemavu wa kudumu kwa abiria.
Alisema pia ajali zinasababisha uharibifu wa mali na kwamba ataendelea kufanya ziara za namna hiyo mara kwa mara ili kubaini makosa mengine.
Aidha aliwataka Sumatra pamoja na kikosi cha usalama barabarani kusimamia sheria za usalama barabarani na kutowaonea aibu madereva watakaonekana kuwa na makosa kwani kwa kufanya hivyo kutapunguza ajali za barabarani ambazo zimekuwa ni tishio hapa nchini.
Kwa upande wake, mkuu wa usalama barabarani mkoani hapa, Leonard Gyindo alisema kuwa kikosi cha usalama barabarani kimejipanga katika kudhibiti ajali za barabarani kwa kufanya ukaguzi kabla ya gari halijaondoka katika kituo hicho.
Gyindo alimpongeza Waziri Mwakyembe kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa jitihada zake katika kusimamia sheria hasa za usalama barabarani na kuahidi kuwa kikosi cha usalama barabarani kitampa ushirikiano na kutekeleza maagizo yote atakayotoa.
Kwa upande wa wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya ziara hiyo walimwomba Waziri huyo kufanya ziara nyingine kituoni hapo hasa nyakati za usiku na kushuhudia hali ya giza lililopo katika kituo hicho.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Hongera sana Mh.waziri Mwakyembe kwa kazi nzuri unayoifanya,inabidi viongozi wengine waige mfano wako,sio wanakaa tu maofisini na kwenye magari ya kifahari na kula pesa zetu bure,Hivyo ndivyo kiongozi anatakiwa afanye kazi yake ili alete maendeleo ya nchi.
Post a Comment