Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa akiongea na wananchi wake (hawapo pichani).
Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Mheshimwa Zitto Kabwe akiunguruma.
James Millya aliyehama CCM na Kujiunga na CHADEMA hivi karibuni akiwasha moto kwenye mkutano wa hadhara mkoani Iringa.

Nyomi ya watu waliohudhuria mkutano huo.
----
Magamba yavuliwa watu wamiminika toka Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Katika mkutano huu Mh. Msigwa alichukua maoni na maswali toka kwa wananchi ili kwenda kuwawakilisha vyema wananchi waliomtuma bungeni hasa katika bunge hili la bajeti.
Mh. Zitto akihutubia mkutano uliohudhiliwa na mamia ya wakazi wa Manispaa ya Iringa katika viwanja vya Kihesa Sokoni, Naibu Katibu Mkuu huyo wa Chadema ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha, alisema bajeti iliyosomwa bungeni, inaonyesha wazi kwamba serikali imeshindwa kujali wananchi maskini badala yake inajali matajiri.
“Jumatatu tutaenda kuwakatalia bajeti yao, hatutaikubali kamwe! bajeti hii imeshindwa kudhibiti mfumko wa bei ambao umepaa kwa kasi hadi kufikia asilimia 18.7 toka asilimia 6.6, iliyokuwepo wakati bajeti iliposomwa mwaka jana,” alisema Kabwe.
Alisema vitu vinavyofanya maisha ya Watanzania kuwa magumu ni mfumuko wa bei ya chakula ambao ni asilimia 25 na nishati ambayo ni asilimia 27, huku serikali ikishindwa kudhibiti hali hiyo kwa kuandaa bajeti inayoshindwa kutekeleza ahadi zake.
Alisema bunge lilipitisha mpango wa maendeleo wa taifa uliotaka asilimia 35 ya mapato ya ndani, yatengwe kwa ajili ya bajeti ya maendeleo jambo ambalo limekuwa kinyume na bajeti iliyosomwa ambayo, imetengewa asilimia sifuri, kwa ajili ya mpango huo.
“Tutahoji kwa nini serikali imeshindwa kutenga asilimia 35 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mpango huu, kwa nini inafanya vitu kinyume cha sheria na kutenga asilimia sifuri?... jambo hili hatutakubaliana nalo,” alisema Zitto.
Alidai kuwa hali halisi ilivyo sasa ni kwamba, Mtanzania anatumia asimilia 48 kwa ajili ya kununua chakula, asilimia tisa kwa ajili ya nishati hali ambayo ni hatari.
Alidai kuwa, kwa mujibu wa bajeti hiyo, shughuli zote zitaendeshwa kwa fedha za mkopo na misaada toka kwa wahisani huku akidai kuwa, kwa mwaka huu serikali itakopa shilingi trioni tano, huku deni la sasa likiwa trioni 22.
“Trioni 22 ni deni kubwa ambalo linafanya kila kichwa cha Mtanzania kudaiwa shilingi laki 4.18, fedha ambayo ni kubwa kuliko hali halisi ya Mtanzania,” alisema.
Alidai kuwa tatizo sio kukopa isipokuwa tatizo ni pale ambapo serikali inakopa kwa ajili ya anasa kama mafuta ya mabenzi, na kulipana posho.
Picha na Habari na Mh.Mchungaji Peter Msigwa
Mbunge wa Iringa Mjini
(CHADEMA)



No comments:
Post a Comment