ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 7, 2012

Pongezi mawaziri kufanya ngumu dhidi ya uzembe


Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
JUZI Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe juzi alichukua uamuzi mgumu wa kutengua uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Paul Chizi kutokana na kuteuliwa bila kufuata taratibu zinazotakiwa na badala yake akamteua rubani wa siku nyingi ndani ya shirika hilo, Kapteni Lusajo Lazaro kukaimu nafasi hiyo. 

Waziri Mwakyembe alichukua uamuzi huo kutokana na taratibu za uteuzi kwa wafanyakazi wa umma kutokufuatwa wakati wa kumteua Chizi.

Kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Omari Nundu Chizi aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Community Airline wakati taratibu zinasema, mtu anayetakiwa kukaimu nafasi hiyo anatakiwa kutoka miongoni mwa wafanyakazi wa ndani ya shirika ua taasisi.

Kabla ya kuchukua hatua hiyo, hivi karibuni Waziri Mwakyembe aliahidi kuuondoa uongozi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kutokana na kushindwa kuwajibika ipasavyo ikiwamo uzembe unasababisha treni treni kufanya safari zake.

Mbali ya Mwakyembe, waziri mwingine ambaye ameonyesha kuchukua maamuzi magumu ni wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda ambaye alitangaza kumuondoa kazini Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege.

Ekelege anatuhumiwa kuwa taasisi anayoiongoza iliweka vituo hewa vya kukagulia magari nje ya nchi hivyo kuifanya Serikali kukosa mapato.

Waziri mwingine ambaye ameonyesha msimamo mkali katika wizara yake ni wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki ambaye alianza kutekeleza kwa vitendo kauli yake ya kuisafisha Idara ya Wanyamapori baada ya kuwasimamisha kazi wakurugenzi wanne na askari 28 wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kupisha uchunguzi wa kuuawa kwa faru wawili na kung’olewa pembe.

Faru hao ni miongoni mwa watano ambao Rais Jakaya Kikwete aliwapokea kutika Afrika Kusini, Mei 21, 2010, lakini Desemba 21, mwaka huo faru dume aitwaye George aliuawa na pembe zake zilinaswa Mwanza.

Naye Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo Mei 20, mwaka huu alitembelea ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) jijini Dar es Salaam na kupewa majina ya vigogo waliopo wizarani kwake na waliopo ndani ya shirika hilo ambao wanahujumu.   

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi naye amechukua hatua ya kuunda Tume ya kuchunguza kashfa ya utoaji vibali bandia kwa wageni katika Idara ya Uhamiaji nchini.

Kutokana na hatua hizo za kijasiri, sisi tunawapongeza kwa dhati mawaziri hao kwa kuchukua uamuzi huo mgumu wa kusafisha wizara zao tangu Rais alipowateua kushika nyadhifa hizo kuanzia Mei 4, mwaka huu alipotangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Tunaamini kwamba hilo ndilo jukumu la mawaziri  kuhakikisha kuwa serikali inalinda mali za umma na kuwapatia wananchi wake maisha bora.

Ni vyema mawaziri wengine wakaige mfano wa mawaziri hao kwa kuchukua maamuzi mazito ya kusafisha wizara zao ili kukabiliana na utendaji mbovu na ufisadi uliokithiri miongoni mwa watendaji wa ngazi za juu serikalini. 

Tunajua kabisa hivi sasa ndani ya wizara nyingi nchini kumejaa mchwa watu ambao wanatafuna mali za umma, licha ya kelele zinazopigwa na baadhi ya watu wanaochukizwa na tabia hiyo inayodidimiza maendeleo ya taifa letu ambalo asilimia kubwa ya wananchi wake wametopea kwa umasikini.

Haiwezekani mawaziri waendelee kulea watu ambao wajulikana kabisa kuwa wanajihusisha na kuhujumu raslimali za nchi akaachwa tu, vinginevyo atakuwa anashirikiana nao au ni mzembe.

Tunadhani sasa umefika wakati mawaziri na watendaji wengine serikali watimize wajibu wao wa kuhakikisha kuwa wanadhibiti wezi, wahujumu uchumi na wazembe katika maeneo yao.


Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Tunawataka watumishi wa serikali kama Dk. Harrison.Kwenye wizi, rushwa, uteuzi wenye kukiuka misingi iliyowekwa na taasisi, shirika au baba na mama wa nchi(katiba)waingilie kati. Kiongozi shupavu hawaogopi waalifu, na kumbuka Tanzania haitaki viongozi wanyonge(weak).

Wahusika (suspects) kiguu na njia, wapelekwe mahakamani kujibu shutuma, na wakiwa na hatia njia ni moja; keko, segerea au sehemu nyingine ya correction. Waziri umetushika. Kazi ya "watchdog" isiachiwe chadema na upinzania peke yake hata ccm wapenda nchi yao wana jukumu hili kwani hata nyinyi tumewachagua. Tanzania ni yetu wote tuijenge na kuilinda kusudi tufikie lengo letu ya kuwa na TEKNOLOGIA yetu wenyewe.

Nafasi ya Tazania kuendelea na fortune tuliyonayo kuendelea, sky is a limit.