ANGALIA LIVE NEWS
Friday, June 15, 2012
Sadiq aitaka Taifa Stars kushinda Maputo
Sosthenes Nyoni
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiq amewataka wachezaji wa timu ya taifa 'Taifa Stars' kuhakikisha wanapambana kufa na kupona ili waiangamize Msumbuji katika pambano lao litakalopigwa keshokutwa.
Kikosi cha Taifa Stars kimeondoka nchini alfajiri ya leo kuelekea Maputo, Msumbiji tayari kwa mechi hiyo ya marudiano ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazopigwa mwakani nchini Afrika Kusini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi Bendera ya Taifa kwa msafara wa timu hiyo, Sadiq alisema anaamini kwa kiwango cha hivi sasa cha timu hiyo uwezekano wa kuifunga Msumbuji ni mkubwa, lakini akawataka wachezaji wa timu hiyo kujituma kwa kutambua taifa liko nyuma yao.
Alisema Watanzania wameanza kuwa na imani na timu hiyo na uthibitisho ni jinsi walivyofurika kwa wingi uwanjani kwenye mechi dhidi ya Gambia, ambapo Taifa Stars ilishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na mabeki Shomari Kapombe na Erasto Nyoni.
Sadick aliwasifu wachezaji wa timu hiyo kwa kuonyesha kiwango bora dhidi ya Gambia Jumapili iliyopita na kuwataka wasibweteke ili waendelee kudumu na kucheza katika kiwango hicho.
“Mlicheza vizuri dhidi ya Gambia, naomba muendelee kuonyesha kiwango kama kile, mkibweteka na kuona mmeishajua mtakosea,”alisema Sadiq.
Alisema anaamini wanakwenda Msumbiji kwa lengo moja tu la ushindi na kuongeza kuwa kitendo cha kuwakabidhi bendera ya taifa kinamaanisha wakapambane kufa au kupona ili washinde.
Naye, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga aliwataka wachezaji wa timu hiyo kufanya kila linalowezekana washinde mchezo huo na kusonga mbele.
Tenga alisifu kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo dhidi ya Gambia na kusema kwamba kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi alishuhudia misafara ya mashabiki wakiwa na ngoma ya mdundiko wakiishangilia timu hiyo kuelekea kwenye Makao Makuu ya shirikisho hilo.
“Mnakwenda kucheza mechi muhimu sana, kama mlivyojituma mlipocheza na Gambia hivyo hivyo fanyeni mtakapocheza na Msumbiji,”alisema Tenga.
Naye kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen alisema wamefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo na kuahidi ushindi.
Kwa upande wake, nahodha wa timu hiyo, Juma Kaseja aliwaomba Watanzania waiunge mkono timu hiyo kama walivyofanya kwenye mechi dhidi ya Gambia.
Mechi dhidi ya Msumbuji itakuwa mtihani wa nne wa Kim ambaye alianza kibarua chake kwa suluhu 0-0 dhidi ya Malawi na kufuatia na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Ivory Coast, kisha akaisambaratisha Gambia mabao 2-1 katika pambano la kusaka nafasi ya kufuzu kushiriki fainali za mataifa ya Afrika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment