ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 28, 2012

Simba wamng'ang'ania Yondani

Clara Alphonce
KLABU ya Simba imeendelea kumng'ang'ania beki wake, Kelvin Yondani licha ya kuachana na timu hiyo na kwenda kujiunga na Yanga.

Hatua ya Simba kumng'ang'ania mchezaji huyo ni baada ya kutangaza wachezaji iliyowaacha akiwemo kipa wa akiba. Ally Mustapha 'Barthez', beki raia wa Uganda, Derick Walulya, mashambuliaji raia wa Ivory Coast, Gervais Kago na Juma Jabu.

Beki mwingine ambaye ametangazwa kuachwa ni Salum Kanoni ambaye hata hivyo, mkataba wake umebakisha siku mbili kumalizika.

Wachezaji ambao klabu hiyo inakusudia kuwatoa kwa mkopo ni Rajab Isihaka, Salum Machaku, Haruna Shamte na Shija Mkina. Mkina bado anacheza kwa mkopo Kagera Sugar.


Mwishoni mwa wiki, baadhi ya wadau wa Simba walikuwa wakihaha kutaka kumrejesha mchezaji huyo kundini baada ya kuanza mazoezi Yanga Ijumaa iliyopita lakini mwanzoni mwa wiki hii, Mwananchi ilitonywa na chanzo cha habari kikisema kuwa baadhi ya watu wanaohusika na usajili wameamua kuachana na mchezaji huyo.

Chanzo kimoja ndani ya klabu ya Simba, kilipasha kuwa uamuzi wa Yondani kwenda Yanga ni sahihi kwani uzembe wa viongozi ndiyo uliosababisha yote hayo kutokea.

"Mchezaji alikuwa akiwaambia juu ya mkataba wake, viongozi wako kimya, akisafiri na timu ya Taifa akirudi anawakumbusha lakini kimya, tumerudi na Simba kutoka Setif, Algeria akawakumbusha, tumetoka Al Shandy kote kimya, sasa uamuzi wake ni sahihi," kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alikaririwa akisema kuwa Simba haitamwacha mchezaji huyo kwa kuwa ni mchezaji wake halali na itamtangaza katika orodha yake ya mwisho Juni 30. 

Alisema: "Yondani ni mchezaji halali wa Simba aliye na mkataba hadi Mei 31, 2014 mkataba ulioongezwa Desemba 23, 2011 ikiwa ni sehemu ya kuundeleza mkataba wa awali uliokuwa unaisha Mei 31, 2012."

Yondani ambaye tayari amevuta 'fungu' kutoka kwa Yanga, alisema juzi kuwa hawezi kurudi nyuma na uamuzi wake ni sahihi kwenda klabu hiyo ya Jangwani.

"Mimi nimesajili Yanga na nimeshachukua changu...mpira ni maisha yangu na isitoshe haya ni maisha na siwezi kuchezea bahati yangu. Mimi nimeshaamua kuchezea Yanga na nataka Simba wajue hivyo," alisema Yondani akizungumza na kipindi cha Sports Extra cha Clouds TV katikati ya wiki hii.

Akizungumza jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Boniface Wambura alikiri kupokea majina ya wachezaji walioachwa na Simba huku likikosekana jina la Yondani.

Mbali na Simba, wageni wa Ligi Kuu, Polisi Morogoro imeacha wachezaji 17 wakati Tanzania Prisons ambayo nayo imepanda Ligi Kuu imeacha wachezaji 11.
 
Walioachwa na Tanzania Prisons ni Adam Mtumwa, Dickson Oswald, Exavery Mapunda, Ismail Selemani, Lwitiko Joseph, Mbega Daffa, Mwamba Mkumbwa, Mussa Kidodo, Rajab Ally, Richard Mwakalinga na Sweetbert Ajiro.

Polisi Morogoro imewaacha Abdul Ibadi, Ally Moshi, Benedict Kitangita, Hassan Kodo, Hussein Lutaweangu, Hussein Sheikh, Juma Maboga, Mafwimbo Lutty na Makungu Slim.

Pia wamo Mbaraka Masenga, Method Andrew, Moses Mtitu, Ramadhan Kilumbanga, Ramadhan Toyoyo, Said Kawambwa, Salum Juma na Thobias John.
 
Kwa upande wa Azam FC, imewasilisha majina ya wachezaji watatu iliyoamua kukatisha mkataba wao ambao ni Tumba Swedi, Mau Bofu na Sino Augustino.

Kagera Sugar imewaacha Cassian Ponera, Hamis Msafiri, Hussein Swedi, Ibrahim Mamba, Martin Muganyizi, Mike Katende, Moses Musome, Msafiri Davo, Said Ahmed, Said Dilunga, Steven Mazanda na Yona Ndabila.

Alisema uhamisho wa wachezaji kwa msimu huu ulianza Juni 15 mwaka huu na utamalizika Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuanza wachezaji (kwa wasio wa Ligi Kuu) ni kati ya Juni 15 na 30 mwaka huu. 

Wambura alisema kuwa klabu za Ligi Kuu kutangaza wachezaji watakaositishiwa mikataba yao ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu na usajili wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu.


Mwananchi

No comments: