ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 18, 2012

Uamsho wapigwa mabomu Zanzibar


Kamishna wa Polisi Zanzibar,
Mussa Ali Mussa



Wiki kadhaa baada ya Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumuki), kufanya mihadhara iliyosababisha uvunjifu wa amani visiwani hapa na kulazimu Jeshi la Polisi kutumia mabomu kuwatawanya, hali kama hiyo imetokea tena jana.

Jeshi hilo limetumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Jumuki waliokuwa wakielekea katika jimbo la Donge ambako walikuwa na mhadhara katika msikiti mmojawapo, katika mwendelezo wa mikutano yao ya kutaka Zanzibar kujitenda ndani ya Muungano.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema wafuasi hao walikuwa wamejipakia katika magari wakitokea Mkoa wa Mjini Magharibi na kuelekea Mkoa wa Kaskazini Unguja, kabla ya kuzuiwa na kutakiwa warudi walipotoka.


Alisema kwamba Jeshi la polisi lilipokea barua ya Mkuu wa Mkoa ya kuizuia Jumuiya hiyo kufanya mihadhara katika jimbo hilo kutokana na wananchi wake kupinga misikiti kutumika kwa shughuli za kisiasa.

"Polisi imefanikiwa kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani na walianza kutawanywa baada ya kufika katika eneo la Mahonda. Tunawaomba wananchi kujiepusha na vitendo vya kuashiria uvunjifu wa amani," alisema Kamishna Musa.

Taarifa zinaeleza kwamba watu kadhaa wanashikiliwa kutokana na tukio la jana baada ya polisi kuzima mkutano huo.

Katika eneo la Mahonda ambako polisi walizima maandamano, ilielezwa kwamba barabara hiyo ilifungwa kwa muda baada ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kuweka kizuizi kwenye eneo hilo kwa nia ya kuwazuia wafuasi wa uamsho waliokuwa wanaelekea Dole.

Wakati Polisi wakipiga mabomu, wafuasi hao walikuwa wakinawa uso kwa maji huku wakibishana na polisi kwa maneno wakitaka wawaruhusu waelekee kwenye mkutano.

Hata hivyo, Polisi waliwazidi nguvu wafuasi hao ambao walilazimika kurudi mjini na kusitisha kuelekea kwenye mihadhara huko Dole.

Tukio hilo limekuja siku chache tangu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, kupiga marufuku mikusanyiko, maandamano na mihadhara isiyokuwa na kibali cha Serikali, kufuatia vurugu zilizotokea Mei 26, na kusababisha makanisa na baa kuchomwa moto Zanzibar.

Machafuko makubwa yaliibuka mwishoni mwa mwezi uliopita visiwani humo na kusababisha makanisa kuchomwa huku Watanzania wenye asili ya Bara wanaoishi na kufanya kazi Zanzibar wakitakiwa kuondoka visiwani humo.

Vurugu hizo zilidaiwa kufanywa na watu wasiofahamika, lakini wakiaminika kuwa ni wafuasi wa kundi la kidini la uamsho kwa madai ya kupinga Muungano na kuitaka Zanzibar ijiondoe kwenye Muungano.

Chanzo cha vurugu hizo kilielezwa ni wafuasi wa kundi hilo kupinga kitendo cha kukamatwa kwa kiongozi wao, Mussa Juma kwa kosa la kufanya maandamano bila kibali cha polisi ambapo walihamasishana kwenda Kituo cha Polisi Madema, kilichoko Wilaya ya Mjini Magharibi wakiwa na silaha za jadi jambo lililowafanya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.


CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Mbona kuna baadhi ya mambo hamkuyaandika kwamba kuna watu amba .o walikwenda kupigwa mabomu ya machozi ndani ya msikiti wakiwemo kina mama na watoto?????????????????