ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 13, 2012

Watumishi wa Idara ya Misitu wanusurika kuuawa na majangiri


Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki
Dk. Felician Kilahama



Watumishi  wawili  wa Idara ya Misitu  waliokuwa  doria katika msitu  wa asili  wa Shengena ulioko wilayani Same mkoani  Kilimanjaro,  wamenusurika kuuawa baada ya kuzingirwa  na  kundi  la watu  wanachiimba madini  katika msitu huo.

Kaimu Mkuu  wa hifadhi  ya msitu huo, Halifayo   Ngoma, amesema watumishi hao walikumbwa na mkasa huo mwanzoni mwa wiki hii baada yakukutana na kundi la watu zaidi ya 50 na kuwazingira.

Ngoma alifafanua kuwa watumishi hao  walifanikiwa kutoroka na kujiokoa na janga hilo.


Aidha, Ngoma pamoja na kuiomba  kuiomba serikali kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili  kwa kuongeza watumishi na vitendea kazi, alisema  hili ni tukio la pili la kushambuliwa na  majangili  hao  ambao  wamefanya uharibifu mkubwa katika vyanzo vya maji  ambavyo asilimia kubwa vimeharibiwa na kemikali  zinazotumika kutafuta madini hayo.

Alisema kuwa mara ya kwanza majangili hao  walishawashambulia kwa kuwarushia mishale na wamesisitiza umuhimu wa serikali kuchukua tahadhari kabla ya hatari kwani hali ni mbaya.

Akizungumza baada ya kutembelea na kujionea uharibifu  mkubwa wa mazingira, Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Dk. Felician  Kilahama, pamoja na kuitaka kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Hai kuwatafuta wote wanaotishia maisha ya watumishi hao,  amekiri kuwa hali katika msitu huo ni mbaya na kwamba sasa watalazimika kuchukua maamuzi magumu.

“Hatuwezi kuendelea kuangalia mambo haya yanatokea, ni lazima hatua zichukuliwe na ikibidi  hata maamuzi magumu kwani vitendo hivi sasa havivumiliki,” alisema Kilahama.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Hermani Kapufi, na Mwenyekiti wa Halmashauri  ya Wilaya ya Same,  Christopher Irira  pamoja na kutoa mapendekezo mbalimbali  yanayolenga kudhibiti vitendohivyo,  wamesema wameshaanza kuwatafuta.
CHANZO: NIPASHE

No comments: