ATLETICO FC ya Burundi imeendeleza ubabe kwenye mechi za
Kundi C, za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, baada ya
leo kuwafunga mabao 5-0 Waw El Salaam kutoka Sudan.
Waw Salaam waliofungwa na Yanga 7-1, sasa rasmi wameaga
mashindano hayo baada ya kupoteza mechi zote tatu, ya kwanza wakifungwa 7-0 na
APR ya Rwanda.
Kwa matokeo hayo, sasa Atletico inaendelea kuongoza Kundi C,
kwa pointi zake saba, baada ya kucheza mechi tatu, kushinda mbili na kutoa sare
moja, wakati APR ya Rwanda inashika nafasi ya pili kwa pointi zake nne na Yanga
ni ya tatu kwa pointi zake tatu, huku Waw Salaam ambayo haina pointi na imemaliza
mechi zake.
Kesho Yanga na APR watahitimisha michezo ya kundi hilo,
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi inayotarajiwa kuwa kali na ya kusisimua.
Katika Kundi B, Tusker ya Kenya, imetoka sare ya bila kufungana
na Mafunzo ya Zanzibar, hivyo kulifanya kundi hilo, ambalo kuna Azam FC pia lizidi
kuwa gumu. Keshokutwa Tusker na Azam FC zitakamilisha mechi za kundi hilo
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, katika mchezo ambao timu itakayoshinda moja kwa
moja itaungana na Mafunzo kutinga Robo Fainali.
Hatima ya Mafunzo kucheza au kutocheza Robo Fainali
inashikiliwa na mechi hiyo, kwani iwapo timu hizo zitatoka sare ya kuanzia
mabao 2-2 zitakwenda zote Nane Bora na wawakilishi wa Zanzibar watarejea nyumbani.
Mechi za Kundi A, zilichezwa jana na mabingwa wa Tanzania
Bara, Simba SC walijiweka kwenye nafasi nzuri ya kwenda Robo Fainali, baada ya kuichapa
Ports ya Djibouti mabao 3-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shujaa wa Simba katika mchezo huo, alikuwa mshambuliaji mpya
kutoka Ruvu Shooting ya Pwani, Abdallah Juma aliyeingia kuchukua nafasi ya Amri
Kiemba mwanzoni mwa kipindi cha pili aliyefunga mabao mawili dakika za 60 na 73
na Felix Mumba Sunzu Jr. aliyefunga moja kwa penalti dakika ya 64
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika bila nyavu za
Ports kutikisika, na katika kipindi hicho Sunzu, mshambuliaji wa kimataifa wa
Zambia, alipoteza nafasi tatu za wazi mno, za kufunga mabao akiwa amebaki yeye
na kipa, Kalid Ali Moursal.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mserbia, Milovan Cirkovick
kipindi cha pili kuwaingiza Juma Nyosso kuchukua nafasi ya Haruna Shamte,
Abdallah Juma aliyechukua nafasi ya Kiemba na baadaye Uhuru Suleiman kuchukua
nafasi ya Haruna Moshi ‘Boban’ yaliisaidia Simba.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi tatu baada ya
kucheza mechi mbili na sasa inashika nafasi ya tatu kwenye Kundi A, nyuma ya
URA yenye pointi sita na AS Vita yenye pointi tatu na wastani mzuri wa mabao.
Simba itamaliza na AS Vita ya DRC, mechi ambayo itakuwa kali kwa sababu timu
zote zina pointi sawa.
Katika mchezo wa awali uliotangulia wa kundi hilo, URA ya
Uganda, ilikuwa timu ya kwanza kufuzu Robo Fainali ya baada ya kuichapa mabao
3-1, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam jioni hii.
Mabao ya URA yaliwekwa kimiani na Sula Bagala mawili na
Robert Ssentongo, wakati la kufutia machozi la Vita, inayofundishwa na kocha w
zamani wa Yanga, Raul Jean Pierre Shungu lilifungwa na Mutombo Kazadi.
No comments:
Post a Comment