Editha Majura, Bagamoyo na Fidelis Butahe, Dodoma
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amesema utaratibu wa sasa wa mbunge kuwa waziri haufai na badala yake amependekeza Katiba Mpya itamke kuwa atatoka nje ya Bunge.
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amesema utaratibu wa sasa wa mbunge kuwa waziri haufai na badala yake amependekeza Katiba Mpya itamke kuwa atatoka nje ya Bunge.
Hii ni kauli ya kwanza katika siku za hivi karibuni kutolewa na waziri ambaye yupo katika Serikali iliyopo madarakani.
Dk Kawambwa alisema hayo jana wakati akitoa maoni yake kama raia kwenye Kituo cha Vigwaza, Pwani wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikichukua maoni ya wananchi.
Dk Kawambwa alisema hayo jana wakati akitoa maoni yake kama raia kwenye Kituo cha Vigwaza, Pwani wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikichukua maoni ya wananchi.
Baada ya kutoa maoni yake, Mjumbe wa Tume hiyo, Ally Salehe alitaka kujua msimamo wa Dk Kawambwa kuhusu mbunge kuteuliwa kuwa waziri jambo linalipingwa na watu wengi.
“Tumechukua maoni ya wananchi tangu Mafia mpaka hapa Bagamoyo, wengi wanafikiri kwamba mbunge hastahili kuwa waziri wewe una maoni gani juu ya hilo?” aliuliza Salehe.
Waziri Kawambwa alijibu: “Ni kweli jambo hilo ni tatizo na wananchi wengi wanalifahamu, hususan wa Bagamoyo wanalifahamu zaidi kwani tangu nichaguliwe kuwa mbunge niliteuliwa kuwa waziri. Nadhani mbunge akiteuliwa kuwa waziri, nafasi yake ya ubunge apewe mtu mwingine au Rais awe huru kuteua waziri nje ya Bunge. Nayazungumza haya kutokana na uzoefu nilioupata kutokana na ubunge wangu Bagamoyo na waziri katika wizara tofauti.”
Akijibu swali kuhusu ukomo wa kuongoza kwa viongozi wa ngazi za tofauti na urais, Dk Kawambwa alisema ni vizuri nao wakawekewa ukomo na ikibidi iwe miaka mitano.
“Kuna wabunge mle ndani mpaka nawaonea wivu, wamekaa majimboni mwao kwa miaka 35 hadi 40, angalau iwe kwa awamu tatu, isiwe Rais ana ukomo, lakini wabunge na mawaziri wanaendelea kupokezana vijiti bila ukomo,” alisema Dk Kawambwa.
Kiongozi wa tume hiyo katika Mkoa wa Pwani, Profesa Mwesiga Baregu alipohoji msimamo wa waziri huyo kuhusu ukubwa wa Baraza la Mawaziri baada ya wananchi wengi kutaka lipunguzwe na sambamba na idadi ya wizara.
Akijibu hilo, Dk Kawambwa alisema: “Kwa mawazo yangu binafsi na kwa uzoefu wangu ninashauri suala hilo lisiingizwe kwenye Katiba na aachiwe Rais achague idadi ya watu atakaotaka wamsaidie kutekeleza majukumu yake.”
Akitoa mfano, alisema alipokuwa Waziri wa Miundombinu, aliongoza wizara hiyo peke yake tofauti na sasa ambapo imegawanywa kuwa ya Ujenzi na kuongozwa na Dk John Magufuli na Uchukuzi inayoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe.
“Nilipokuwa Waziri wa Miundombinu nilihenya sana nikawa hata familia siioni, lakini sasa kuna mawaziri mawili pamoja na manaibu wao,” alisema.
Dk Kawambwa aliunga mkono maoni ya wananchi wanaotaka masomo ya dini yaingizwe kwenye mitalaa ya elimu kuanzia shule ya msingi hadi sekondari... “Hata mimi ningeweza kupendekeza Katiba itamke hivyo ingawa Serikali haina dini, lakini ijenge mazingira mazuri kwa wananchi wake kuabudu. Ikifanikiwa katika hilo itapata watu wenye maadili mema.”
Mbali ya Kawambwa, mtu mwingine aliyependekeza mawaziri wasiwe wabunge ni aliyekuwa Mbunge wa Arumeru, Piniel Ole Saitabau (70) ambaye amesema kitendo cha Rais kuteua wabunge kuwa mawaziri ndicho kinachochea rushwa katika chaguzi kwa kuwa wagombea hutoa fedha kwa lengo la kushinda ubunge na kuteuliwa kuwa mawaziri.
Akitoa maoni yake kuhusu Katiba Mpya mbele ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Wilaya ya Kongwa, Dodoma juzi, Saitabau ambaye alikuwa mbunge kuanzia mwaka 1980 hadi 1990 alisema hiyo itasaidia hata mawaziri waliovuliwa madaraka kwa tuhuma za rushwa kutopokewa kishujaa katika majimbo yao.
Alisema waziri au mbunge atakayebainika kutafuna mali ya umma, Katiba Mpya iwe na kipengele kitakachowafanya waliobainika kufilisiwa mali zao na kufungwa maisha.
Saitabau ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa na Rombo alisema: “Rushwa imekithiri katika chaguzi nchini kwa kuwa wagombea ubunge wanakuwa na matumaini makubwa kwamba wakichaguliwa kuwa wabunge, wanaweza kuwa mawaziri.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment