Jeshi la Polisi mkoani hapa limetumia
magari yake kuziba barabara kwa lengo la kumdhibiti Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kufanya mkutano wake wa hadhara,
aliotarajia kuufanya katika Kijiji cha Mang’onyi.
Kufuataia hali hiyo, Lissu juzi alilazimika kubaki kijiji jirani na
Mwau zaidi ya saa nne baada ya jeshi hilo ‘kupaki’ magari yake kwa ajili
ya kufunga barabara ya kwenda eneo alilopanga kufanya mkutano huo.
Jeshi hilo lilipanga magari yake barabarani na askari wenye silaha
umbali wa kilomita tano, kabla ya kuingia Kijiji cha Mang’onyi, eneo
ambalo Lissu alipanga kufanya mkutano wa hadhara.
Hata hivyo, Lissu alilaani kitendo hicho, kwa madai kuwa kinawanyima
wananchi haki ya kukutana na mbunge wao, kwa ajili ya kumweleza matatizo
mbalimbali yanayowakabili.
Kamanda wa Polisi Mkoa Singida, Linus Sinzumswa, alisema hatua hiyo
ilichukuliwa, baada ya Lissu kunyimwa kibali cha kufanyia mkutano katika
Kijiji hicho, kutokana na sababu za usalama.
Sinzumwa alifafanua kuwa, licha ya mbunge huyo kuomba kibali cha
kufanya mkutano wa hadhara, lakini alinyimwa kutokana na kuonyesha
dalili za uwepo wa uvunjifu wa amani.
Kufuatia tukio hilo, Sinzumwa alisema kuwa Polisi inawashikilia watu
watano kwa mahojiano zaidi kutokana na tuhuma za kujaribu kukusanyika
eneo la mkutano usio na kibali.
Baadhi ya wananchi wamelalamikia jeshi la polisi kuanza kujihusisha na
masuala ya siasa, badala ya kufanya kazi ya ulinzi ikiwemo kuulinda
mkutano huo uweze kufanyika katika hali ya amani na utulivu, kuliko
kumzuia mbunge wao bila sababu za msingi.
No comments:
Post a Comment