ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 20, 2012

KIUNGO WA YANGA ANAEFANYA VIZURI KATIKA TIMU HIYO AKUTWA NA KASHIFA

IMEBAINIKA kuwa kiungo wa Yanga, Omega Sande Seme, anatumia jina hilo ambalo siyo lake na kwamba alilinunua ili kupata nafasi ya kushiriki katika michuano ya Copa Coca Cola mwaka 2006, kisha baadaye kujiunga na Tanzania Soccer Academy kabla ya kutua Jangwani.
Kijana mwenye jina la Omega Sande Seme amezungumza na Championi Ijumaa na hivi ndivyo anavyotiririka:
“Nilizaliwa mwaka 1988 Kijiji cha Mloo, Mbeya na kupata elimu yangu ya msingi na sekondari mkoani hapo. Mwaka 2006 nilishiriki katika michuano ya vijana, Copa Coca Cola, nikiwa mchezaji wa timu ya Shule ya Sekondari ya Mloo, nakumbuka (Marcio) Maximo alikuwepo wakati wa kuchagua vipaji.
“Baada ya kushiriki tuliambiwa tusubiri majina ya watakaoteuliwa kwenda Dar, jina langu lilitoka lakini sikuitwa kwenye msafara, matokeo yake nikasikia kuna mtu anaitwa Omega Sande Seme kutoka katika vijana wa Mbeya wakati mimi mwenyewe sikujulishwa chochote, nilipoenda kuuliza shuleni sikupata jibu la kueleweka.


“Nikaamua nimalize masomo ndiyo nifuatilie. Baadaye nikagundua kuwa aliyetumia jina langu ndiyo ambaye yupo Yanga, jina lake halisi anaitwa Yusto Anyandwile Kalota, baba yake ni Anyandwile Kalota Kilembe.
“Huyo Omega (Yusto) wa Yanga, alizaliwa Zambia na amekulia kule, hakuwahi kusoma huku Tanzania. Binafsi sikuendelea kucheza mpira ila inaniuma kuona mtu anatumia jina langu (anatoa vyeti vya shule vikiwa na jina la Omega Sande Seme). Nataka alifute au anilipe fidia ya milioni 100 kwa kuwa amefaidika sana kupitia jina langu,” alisema Omega.
Championi Ijumaa lilipowasiliana na mama mzazi wa Omega (siyo wa Yanga), ambaye alijitambulisha kwa jina la Sophia John Mboya au Mama Omega mkazi wa Mloo, Mbeya alisema:
“Inaniuma sana mwanangu kudhulumiwa haki yake, kuna kipindi baba wa huyo anayejiita Omega (wa Yanga) alikuja kwangu lakini hatukuelewana kwa kuwa nilikuwa nina hasira sana. Nawajua ukoo wao wote, huyo baba alimzaa mtoto wake Zambia na hakuwahi kusoma huku,” alisema mama Omega.
Gazeti hili lilipomtafuta Omega wa Yanga alisema: “Ni kweli nilinunua jina la mtu, lakini haikuwa kosa langu kwa kuwa nilikuwa chini ya uangalizi wa watu wengine, nilikubali ili nicheze soka, nipo tayari kukutana na huyo mtu (Omega halisi) ili kuzungumza naye na tuyamalize.”

No comments: