ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 1, 2012

Moyo wa huruma huwa chanzo cha usaliti



TUMEKUTANA tena kujuzana machache kuhusu maisha yetu ya kila siku. Sasa hivi kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja, limekuwa jambo la kawaida, ndoa zimeingia katika migogoro mingi, nyingine kutokana na mdudu huyu ‘kukosa uaminifu’.
Kona hii kama kawaida imefanya uchunguzi wa kina na kugundua sababu kubwa ya uhusiano mwingi kuwa na migogoro ni kukosa uaminifu. Nitamzungumzia mwanamke ambaye ndiye aliye kwenye hatari kubwa katika mapenzi.
Moyo wa huruma umekuwa tatizo kwa wanawake wengi ambao wamo ndani ya uhusiano unaowafanya wajidhalilishe kwa huruma yao.
Huruma hiyo ipo vipi?
Katika dunia hii, wapo watu wenye mioyo ya woga pale wanapojua mwanamke aliyempenda ni mke wa mtu, lakini wengine wamekuwa tofauti, wao hupenda wake za watu kwa kuamini huwa hawana gharama kubwa kwa vile kila kitu wanapata kwa waume zao.
Wao wanaume gharama yao inakuwa ni ndogo, wanaweza kuhonga mara moja na kujilia kwa muda mrefu bure.
Wengi huamini mwanamke asiye na mtu maalumu, huyaendesha maisha yake kupitia mwili wake, kila kukicha haishi mizinga. Watu kama hawa huwa king’ang’anizi, hata kama utamueleza kuwa umeolewa, bado atakufuata huku akikueleza kilio chake, umpe hata mara moja ili tu autulize moyo wake, akidai amekuwa akiteseka kila anapokuona.
Mtu wa aina hii huwa si mkali, ni mpole, mwenye uso wa kinyonge, mwenye kujua kubembeleza kwa maneno matamu kuliko hata mumewe. Kwa vile mwanamke ameumbwa kwa roho ya huruma, hujikuta akimuonea huruma mtu ambaye kila kukicha haachi kumlilia.
Mwanamke huamini anachoelezwa ni kweli. Naye bila kutumia akili, hujikuta akijiuliza kwani akimpa mara moja kuna nini? Kwa vile uaminifu ameuweka pembeni basi hukubali kuisaliti ndoa yake na kuutoa mwili wake kwa mtu mwingine.
Moyo wa huruma umekuwa tatizo kubwa kwa wanawake wengi kushindwa kusimamia heshima ya ndoa au uhusiano wao kwa kuamini hawawezi kuwa sehemu ya mateso ya mtu kwa tendo la dakika tano, wanasahau tendo lile linaweza kuwaharibia maisha yao yote na kuonekana hawafai mbele ya jamii.
Hii pia ipo kwa wasichana wengi mtaani kuitwa mama huruma kwa sababu hiyo.
Ukifuatwa na king’ang’anizi ufanyeje?
Umemueleza kuwa umeolewa lakini bado anaendelea kukusumbua, amini huyo ni adui yako namba moja, hata kama atatoa machozi ya damu, hana tofauti na shetani anayemuingiza mwanadamu kwenye matatizo lakini akishaharibikiwa, humkimbia.
Siku zote iheshimu ndoa yako, muonee huruma anayekutunza, si huyu muongo ambaye kazi yake ni kuharibu ndoa za watu na kujisifu kijiweni katembea na wake za watu wengi.
Sifa kubwa ya mwanamke ni kujitambua, kwamba kwa nini yupo pale na kwa nini hayupo kwa mwingine. Ukipata jibu basi hutakuwa na roho ya huruma kwa mharibifu.
Mchukie mwanaume yeyote anayejua umeolewa lakini anakung’ang’ania. Usimpe nafasi, kama siku ya kwanza ulisimama kumsikiliza na ukasikia upuuzi wake, bado kesho unasimama naye tena, lazima utakuwa una pepo la ngono anayekunyemelea.
Ni kosa mke wa mtu kusimama na mtu kuanza kubishana juu ya mapenzi, jibu ni moja, nimeolewa, basi. Usiongeze neno wala kusimama kumsikiliza tena.
Tukutane wiki ijayo...
Mwandishi: Ally Mbetu

www,globalpublishers.info

1 comment:

Anonymous said...

utafikiri unaongea na mimi unanijua nini, kuna mkaka amenililia sana ana mke nami nimeolewa kosa langu naliona sasa kusikiliza na kubishana nae kuhusu mapenzi kumbe jibu ni moja tu Nimeolewa shukrani kaka Ally Mbetu