ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 2, 2012

MUHUSIKA WA USAFIRISHAJI WA WAHAMIAJI HARAMU ADAKWA JIJINI ARUSHA



Na Mwandishi Wetu,Arusha.

IDARA ya Uhamiaji mkoani Arusha, inamshikilia mtu mmoja anayehusishwa na biashara ya kusafirisha wahamiaji haramu waliokamatwa katika Msitu wa Chitego, Dodoma ambapo miongoni mwao 45 walipoteza maisha kwa kukosa hewa katika lori walilokuwemo.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa mtu huyo (jina linahifadhiwa), amekuwa akifanya biashara hiyo kwa kusafirisha wahamiaji kutoka Ethiopia na Somalia kupitia nchini kwa muda mrefu.

Hata hivyo, taarifa zinadai kwamba tayari kumekuwa na njama za chini kwa chini zinazosukwa kwa ustadi mkubwa na baadhi ya maofisa wa idara hiyo mkoani hapa, kutaka kumwachia mtuhumiwa huyo.

Kukamatwa kwa raia huyo kumekuja wakati Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini, Pereira Ame Silima akisema kwamba kitendo cha kusafirisha wahamiaji haramu nchini kimekuwa ni mchezo wa kawaida, kwani Watanzania ndiyo wanaowasaidia kuwasafirisha kutoka Nairobi kupitia Arusha na mara nyingi hupita usiku katika njia za panya.

Vyanzo vya habari vimelieleza gazeti hili kuwa mtuhumiwa huyo ambaye ni raia wa nchi jirani ya Kenya alikamatwa Juni 25 mwaka huu wilayani Longido akiwa katika harakati za kusafirisha wahamiaji haramu wengine kutokea nchi jirani ya Kenya.

Vyanzo hivyo vimedai kuwa mtuhumiwa huyo mara baada ya kukamatwa al
ifikishwa moja kwa moja katika makao makuu ya Idara ya Uhamiaji mkoani Arusha huku lori alilokuwa ndani yake likipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Vyanzo hivyo, vilienda mbali zaidi na kubainisha kwamba mtuhumiwa huyo na washirika wake wamekuwa wakilipwa Dola3,000 za Marekani kwa kila raia wanayemsafirisha ambapo kazi hiyo imekuwa ikiwashirikisha baadhi ya vigogo wa Idara ya Uhamiaji.

“Wamekuwa wakilipwa Dola 3,000 kwa kila kichwa, kazi hiyo inafanywa kwa umakini mkubwa na hata maofisa wa uhamiaji wanahusika, kwa mfano wakiwa njiani wanawasafirisha hao wahamiaji haramu, endapo ikigundulika kwenye lori kuna mtu kafa anamweka chini ya gari na kukanyagwa ili ijulikane aligongwa na gari kupoteza ushahidi,” kilisema chanzo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini ya kwamba baadhi ya maofisa wa uhamiaji mkoani hapa waliwaambia washirika wa mtuhumiwa huyo kwamba wanapaswa kutoa Sh40 milioni ili aweze kuachiwa kitendo kilichozua mabishano makali baina ya pande mbili.

Pia uchunguzi huo umebaini ya kwamba mara baada ya mabishano hayo washirika hao waliomba kupunguziwa kiasi hicho cha fedha na ndipo maofisa hao wa uhamiaji waliwaambia watoe Sh25 milioni kitendo kilichoafikiwa na pande mbili.

Mkuu wa Idara ya Uhamiaji mkoani Arusha, Daniel Namomba alikiri taarifa za kushikiliwa kwa raia huyo na kusema kwamba wamemshikilia akiwa na wenzake watatu.

Lakini alikanusha madai ya kutaka kuachiwa kwa njia za rushwa na kusisitiza kwamba bado wanafanya uchunguzi.

“Ni kweli tunamshikilia, wako wanne jumla na bado tunalifanyia kazi tukikamilisha uchunguzi tutakupeni taarifa kamili, sisi hatujabaini chochote kuhusu tuhuma za rushwa,” alisema huku akikataa kutaja sababu ya kukamatwa kwa raia hao.

Hata hivyo, uchunguzi wetu ulibaini kuwa washirika hao walikuwa na Sh20 milioni na walikuwa wakizunguka jijini Arusha kwa kutumia gari aina ya Noah wakifanya juhudi za kujazia Sh5 milioni ili kukamilisha kiasi chote na kukiwasilisha mbele ya maofisa hao.

Kaimu mkuu wa idara hiyo mkoani hapa, Johannes Msumule alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akikataa kulizungumzia kwa undani kwa madai kwamba suala hilo ni nyeti na linashughulikiwa na vyombo mbalimbali vya usalama nchini.

Wakati huo huo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani hapa chini ya Kamanda wake, Mbengwa Kasumambuto ameliambia gazeti hili kwamba wamejitosa kuchunguza tukio hilo baada ya kupokea taarifa za wingu la rushwa kutanda ndani ya sakata hilo.

No comments: