
Mzamiaji Muhsin Salum Muddy aliyepoteza fahamu na kushindwa kufanya kazi ya uokoaji wa watu waliopata ajali ya meli ya Mv Skagit,akiwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Miongoni mwa wazamiaji walioshindwa kufanya kazi ya uokoaji baada ya meli ya Mv Skagit kuzama katika eneo la Chumbe na Dar es Salaam wiki iliyopita ni Muhsin Salum Muddy .
Mzamiaji huyo anasema baada ya kupinduka meli hiyo alipoteza fahamu wakati wa zoezi la kuwaokoa watu waliopata ajali hiyo.
“Sikujitambua mie, na sijui nimefikaje hospitalini hapa maana nafungua macho ndio najiona nipo katika kitanda na nimefunikwa blanketi, ninachokijua mie ni kwamba niliingia katika boti ya polisi kwenda kuwaokoa watu waliopata ajali” alisimulia kijana huyo na kuongeza:
“Pamoja na kwenda kuwaokoa walionusurika katika boti na kuchukua maiti nilikuwa na kamera kwa ajili ya kupiga picha lakini nikashindwa kufanya kazi zote kutokana na hali ya hewa ilivyokuwa mbaya” alisema.
Kushindwa kufanya kazi kwa Muddy kulitokana na mawimbi makali baharini ambayo yalisababisha boti za uokoaji kushindwa kutulia kufanya kazi hiyo, ambapo waokoaji wengine walikumbwa na mkasa kama wa kwake na wengine kujeruhiwa vibaya.
“Tuliondoka Bandari ya Malindi saa 9:30 jioni na tukafika kule saa 12 na baada ya nusu saa ndio tukawa tunaziona maiti zikielea na watu waliokuwa hai wakiomba msaada wa kuokolewa huku wakihangaika sana na kuonyesha kuchoka, wengine tayari walishakunywa maji mengi na kuhitaji msaada lakini haikuwa rahisi kufanya kazi hiyo” alisema.
Kutokana na hali ya bahari kuchafuka sana, baadhi ya vyombo vililazimika kurudi bila kufanya uokoaji, ambapo Muddy alisema wenzake wengi waliokuwa ndani ya boti walitapika sana na kuishiwa nguvu.
Akisimulia tukio lililomkuta kijana anayekadiriwa kuwa na miaka 30, alisema wakati wakikaribia kufika eneo la ajali chombo walichokuwa wamepanda kilipigwa na mawimbi makali na yeye kupatwa na kichefuchefu na hatimaye kutapika na kuishiwa nguvu kabisa.
Alisema wakati yeye akiwa taabani aliwaona wazamiaji wenzake wakitapika sana huku maiti na miili ya watu wanaotaka kusaidiwa wakiwa wanaonekana karibu na boti za uokoaji zilizojitokeza kufanya kazi hiyo huku baadhi ya maiti zikizagaa baharini.
Alisema wakati giza likiingia boti yao ilipigwa na wimbi kali na kuvunja taa za kuwasaidia katika zoezi la uokoaji, na kufanya kazi hiyo kuwa ngumu zaidi.
“Baada ya hilo wimbi kubwa sana kupiga katika chombo chetu na kuvunja taa iliyokuwa ina mwanga mkali shughuli zote zikavurugika na hapo sikuweza kujitambua na najiona nipo hapa hospitalini …najiuliza nimefikaje” alihoji Kijana huyo ambaye ni mzamiaji wa kujitolea.
Alisema eneo ambalo ajali imetokea ni karibu zaidi na Dar es salaam kuliko Zanzibar, lakini anashindwa kupata majibu kwa nini boti za uokoaji za Dar es salaam hazikujulishwa mapema ili ziweze kutoa msaada.
“Boti yetu ni miongoni mwa boti zilizofika mwanzo katika eneo la tukio, tukio limetokea unaiona Wazo Hill Dare s salaam sasa tunajiuliza kwa nini boti za uokoaji zimetoka masafa marefu Zanzibar wakati zingeweza kutoka Dar es salaam na kusaidia?” alihoji tena Muddy ambaye pia ni msanii wa maigizo.
Muddy alifika bandarini mapema baada ya kupata taarifa za kuzama kwa meli hiyo, alikuwa ni miongoni mwa vijana waliojitolea kwenda kusaidia kwa kushirikiana na wazamiaji wengine kutoka Vikosi tofauti vya Ulinzi na Usalama.
Aliingia kwa bahati katika boti ya uokoaji ya polisi na kuanza safari ya kwenda baharini ambapo hali ya hewa ilikuwa mbaya kutokana na mawimbi na upepo mkali.
Baadhi ya wazamiaji wakiwamo waandishi wa habari walitakiwa kujitolea kuwaokoa watu waliopatwa na maafa, lakini wengi wao walishindwa kufika karibu na tukio kusaidia kuokoa kutokana hali ya mawimbi kupiga kwa kasi na baadhi ya waokoaji kuanza kuokolewa wao.
“Mtu yeyote anayeweza kuogelea na kutoa msaada wa uokoaji tunamuomba apande juu ya meli ili twende eneo la tukio tuanze kazi” Maofisa waKikosi Maalum cha Kupambana na Magendo( KMKM) walisikika wakisema bandarini hapo majira ya saa 11 jioni.
Taarifa za tukio la kuzama kwa boti ya Mv Skagit zilianza kusambaa majira ya saa 7:30 lakini harakati za uokoaji zilichelewa kuanza licha ya viongozi wa juu kupata taarifa hizo mapema.
Waandishi wa Habari na wananchi walishuhudia harakati za uokoaji saa 11 jioni huku wazamiaji wakihangaika kutafuta mafuta ili kukimbilia katika eneo hilo.
Kuchelewa kwa zoezi la uokoaji kuliwafanya wananchi kuilaumu serikali na watendaji kwa uzembe na kushindwa kuimarisha huduma za uokoaji nchini licha ya kutokea ajali za majini mara kwa mara.
Wakijitetea mbele ya Waandishi wa Habari, Mawaziri wanaohusika na masuala ya Uchukuzi, Hamad Masoud Hamad (Zanzibar) na Dk Harison Mwakyembe (Tanzania Bara) walisema tukio la kuzama kwa meli hiyo lilikuwa la ghafla na hakukuwapo na muda wa kufanya juhudi za uokoaji.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment