Diwani wa Kata ya Makongo (Chadema), Deusdedit Jacob Mtiro.
Na Haruni Sanchawa
ILIKUWA kama sinema pale Diwani wa Kata ya Makongo (Chadema), Deusdedit Jacob Mtiro alipoongoza kundi la vijana waponda kokoto kubomoa sehemu ya nyumba ya Katibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Kata ya Makongo, Judith Lungato Stambuli Ijumaa iliyopita nyumbani kwake Mlalakua, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Katika tafrani hiyo kiongozi huyo licha ya kuvunjiwa sehemu ya nyumba yake na kuchaniwa gauni na mtandio, habari za kipolisi zinasema Diwani Mtiro anatuhumiwa kwenda na wahuni kwa kiongozi huyo ambapo alipigwa na kusababisha mali zake kadhaa kuibiwa kutokana na vurugu kubwa iliyozuka.
Habari ambazo polisi wanazo ni kwamba mali alizoibiwa kiongozi huyo ni simu aina ya Blackberry yenye thamani ya shilingi 350,000, nguo aina ya dera na vitenge vyenye thamani kubwa, saa ya mkononi na nondo kadhaa zilizokuwa kwenye nyumba ya mama huyo.
Mwandishi wetu aliambiwa na kiongozi mmoja wa polisi kuwa tayari Diwani Mtiro amefunguliwa jalada Kituo cha Polisi Chuo Kikuu cha Mlimani lenye namba UD/RB/4045/2012 (Shambulio la mwili).
Akizungumza na mwandishi wetu, Bi Stambuli alisema sehemu iliyosababisha ashambuliwe hakujenga hivi karibuni bali imejengwa miaka zaidi ya miwili iliyopita na wala haikuwa na usumbufu wowote kwa raia.
“Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wangu aliwahi kusuluhisha suala hili baada ya watu wenye roho mbaya kuvunja, wakaamriwa wajenge, tukiwa polisi alikiri kufanya kosa na wakaamua kunijengea kwa gharama zao, nilishangaa kuona Diwani Mtiro anakuja na kunibomolea tena bila hata notisi, ” alisema katibu huyo.
Baadhi ya wananchi wa Mlalakua akiwemo mzee Kariakoo, walisema kitendo alichofanyiwa mwanamke huyo ni cha kinyama na siasa imeingizwa, “Hakuna sehemu ilikuwa nadhifu kama hii kwani mvua ikinyesha watu walikuwa hawakanyagi tope.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela alipopigiwa simu alisema hajapata taarifa ya tukio hilo na akaahidi kufuatilia.
No comments:
Post a Comment