WAKATI vitendo vya uhalifu vikizidi kuongezeka sehemu mbalimbali
nchini, sasa silaha kutoka nchi jirani zinadaiwa kuingia kwa wingi na
kuuzwa mitaani na baadhi yake kubadilishwa na mahindi, Mwananchi
Jumapili limegundua.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa,
kutokana na kushamiri kwa biashara hiyo ya silaha nchini, bunduki moja
aina ya Short Machine Gun (SMG) sasa inauzwa kati ya Sh300,000 hadi
Sh500,000, huku bunduki aina ya AK 47 ikiuzwa kwa Sh700,000 hadi Sh1
milioni.
Wakati vijiji kadhaa mkoani Tabora vilipokumbwa na uhaba
wa chakula, bunduki aina ya SMG katika Kijiji cha Usinge wilayani
Urambo zilibadilishwa kwa gunia moja la mahindi, huku AK 47
ilibadilishwa kwa magunia mawili ya mahindi.
Uchunguzi wa muda mrefu uliofanywa mikoa
mbalimbali iliyopo mipakani umebaini kuwa, mtandao huo wa uingizaji
silaha ni mkubwa na unawashirikisha matajiri na baadhi ya askari polisi
wasiokuwa waaminifu.
Silaha hizo huingizwa nchini kupitia mkoani
Kigoma, mpakani mwa Rwanda, Kenya, na Burundi kwa kutumia njia
mbalimbali ikiwamo, magari, pikipiki na boti kupitia Ziwa Victoria
pamoja na baiskeli ambapo bunduki hizo hufungwa kama mzigo ya kawaida.
Chanzo
kimoja cha uhakika kililiambia Mwananchi Jumapili kuwa eneo la Usinge
ndiyo kituo kikuu cha kupokelea silaha kutoka Burundi na Rwanda ambazo
husambazwa mikoa mbalimbali nchini.

No comments:
Post a Comment