ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 2, 2012

SMZ yahofia Uamsho kuvuruga uchumi


Serikali ya Umoja wa Kitaifa, (SUK) ipo katika hatari ya kushindwa kujiendesha na kutoa huduma za jamii kwa wananchi wake kama vitendo vya vurugu vitaendelea kujitokeza katika mjadala wa mabadiliko ya Katiba mpya ya Muugano.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, siku moja baada ya Jeshi la Polisi Zanzibar, kuzuia Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara dini ya Kiislamu kufanya mhadhara katika viwanja vya Lumumba kutokana na sababu za kiusalama.
Akifungua mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Watu wenye Ulemavu wa Akili Zanzibar (ZAPDD) huko Maisara, Waziri Aboud alisema Serikali itashindwa kujiendesha na kutoa huduma za jamii kama amani ya Zanzibar itatoweka kutokana na vitendo vya vurugu vinavyoendelea kujitokeza vya kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema Zanzibar inategemea sekta ya Utalii katika pato lake la taifa na bila ya kuwepo amani hakuna mtalii atakaye tembelea visiwani humo.
Aidha alisema sekta hiyo imekuwa ikichangia asilimi 25 ya pato la Taifa asilimia 80 ni ya fedha za kigeni ambapo karibu watu 44,000 wananufaika na sekta hiyo wakiwemo wavuvi, wafungaji na wafanyabiashara Zanzibar.
Alisema viongozi wa vyama vya siasa na dini wanajukumu kubwa la kudumisha hali ya amani wakati huu wa mjadala wa mabadiliko ya Katiba na kama kuna watu wana matatizo yao watumie njia za mazungumzo kuyamaliza.

Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema watalii wanaotembelea Zanzibar wanakuja kutokana na kuimarika kwa mazingira ya amani na Umoja wa Kitaifa tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Novemba mwaka 2010.
Alisema sera za ubaguzi wa dini au siasa zina madhara makubwa katika umoja wa kitaifa na kuwataka viongozi wa dini na vyama vya siasa Zanzibar kujifundisha juu ya madhara ya ubaguzi kwa mataifa ya Rwanda na Burundi baada ya watu wengi kupoteza maisha kutokana na matatizo ya ubaguzi wa ukabila.
Waziri Aboud alisema wananchi wa Zanzibar ni mfano katika bara la Afrika kwa ustaarabu na uvumilivu kidini na kisiasa na kuwataka viongozi wa dini kuendelea kulinda amani na umoja wa kitaifa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: